Dodoma. Hata baada ya Wajumbe wa Bunge Maalumu
kugawiwa nakala za Hati ya Muungano, Tundu Lissu, ameendelea
kung’ang’ana kuwa haipo, ni feki.
Akizungumza kwenye Viwanja vya Bunge mjini hapa
mara baada ya nakala kugawiwa bungeni, Lissu ambaye aliibua hoja hiyo
alisema; “Hivi hawa wanamghiribu nani? Nasema hiyo hati haikuwahi hata
kupelekwa Umoja wa Mataifa.”
Alisema saini iliyo kwenye hati hiyo ni tofauti na
zilizo kwenye hati ya Mabadiliko ya Kwanza ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba ya 10 ya Juni 1965, Hati ya Muswada wa Sheria ya Udhibiti wa
Fedha za kigeni na Sheria ya kugawa ardhi kwa Wazanzibari ambazo zote
zinafanana.
Lissu alisema kwa miaka 50 haikuwahi kuonyeshwa,
wala haikuwahi kuwa UN na hata Zanzibar hawana. Alisema walishuhudia
Benard Membe (Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) akisema
iko UN, jambo alilosema ni kudanganyana tu.
Alisema nyaraka kama hizo, mkataba wa Uhuru
zinatakiwa kuwekwa Makumbusho ya Taifa kwa kuwa ni nyaraka wazi
zinazotakiwa kuona na kila anayetaka, kwa rahisi.
“Marekani ilipata uhuru zaidi ya miaka 200, lakini
kila nyaraka za uhuru zinaonekana kwa rahisi siyo hapa...mambo
yanafanyika chini kwa chini, utadhani biashara haramu,” alisema.
Baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu wamembeza Lissu
kwa hoja hiyo wakisema hatua ya nakala zake kufikishwa bungeni ni sawa
na kumfunga bao la kisigino na kuhoji watazungumza nini baada ya hati
kupatikana.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment