MWANDISHI wa habari mkongwe, Maurus Sichalwe, amefariki dunia jana
nyumbani kwake Mwananyamala Kanisani, Dar es Salaam akiwa na umri wa
miaka 83.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Benedict Sichalwe, ilieleza kuwa Maurus alikuwa akisumbuliwa na saratani ya tumbo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Maurus alianza kufanya kazi mwaka 1952,
katika magazeti ya Nationalist na kufanya kazi ndani na nje ya Tanzania
ikiwa ni pamoja na All Radio India, mjini New Delhi, India katika miaka
ya mwanzoni ya 1960.
Pia kwa zaidi ya miaka 20 alifanya kazi katika kampuni za magazeti ya
Standard na Nation hadi kufikia cheo cha Naibu Mhariri Mtendaji wa
gazeti la Taifa Leo.
Baada ya kurejea nchini Desemba 1983, alifanya kazi katika kampuni ya
magazeti ya CCM, Uhuru na Mzalendo kwa miaka nane (1984 – 1992).
Mwaka 1992, alihamia Kampuni ya Business Times katika maandalizi ya
kuanzishwa kwa gazeti la kwanza la kila siku binafsi kwa lugha ya
Kiswahili, Majira. Lakini alikaa kwa muda mfupi kabla ya kuhamia katika
gazeti la kwanza la michezo la Dimba.
Akiwa msanifu habari wa gazeti la Dimba, alidumu na kampuni hiyo
iliyoanza kuchapisha magazeti ya Rai, Mtanzania, Bingwa, na The African
kwa zaidi ya miaka 15 hadi alipostaafu. Marehemu ameacha watoto tisa na
wajukuu 16.
Mungu alilaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
0 comments:
Post a Comment