
Askari saba kutoka nchini
Uganda wakiwa na bunduki ambazo idadi yake haijafahamika, wamevamia eneo
la Mutukula, mkoani Kagera, na kuanza kufyatua risasi ovyo.Hali hiyo
ilizua hofu na kusababisha tafrani kubwa miongoni mwa wakazi wa eneo
hilo.
Habari kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa askari hao waliokuwa
wamevalia kiraia, walifanya uvamizi huo majira ya saa 11:00 jioni, kwa
kile kilichodaiwa kuwa walikuwa wakiwatafuta watuhumiwa wa wizi wa
pikipiki.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo waliozungumza na NIPASHE kwa nyakati
tofauti, walisema katika tafrani hiyo, wananchi wawili raia wa Tanzania,
ambao majina yao hayajapatikana, walijeruhiwa kwa risasi.
Kwa mujibu wa habari hizo, kati ya majeruhi hao, mmoja anadaiwa kujeruhiwa kwenye kiganja na mwingine mguuni.
Habari hizo zinaeleza kuwa baada ya wananchi kuona wenzao wamejeruhiwa, walianza kupambana na askari hao.
Hali hiyo inadaiwa kusababisha baadhi ya askari hao kukimbia na kuvuka mpaka kuingia nchini kwao.
Hata hivyo, imeelezwa kwamba mmoja kati ya askari hao w aUganda,
alizingirwa na wananchi ambao walikuwa tayari kujichukulia sheria
mkononi.
Walisema baada ya askari huyo kuhofia kuuawa na wananchi, alikimbia
na kujisalimisha katika Kituo cha Polisi kilichoko Mutukula upande wa
Tanzania ambapo alikamatwa na kuwekwa rumande.
Askari huyo ambaye jina lake halijafahamika hadi sasa, bado anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kagera kwa mahojiano zaidi.
Aidha, habari zaidi zilidai kuwa askari waliokimbia na kuingia Uganda waliwakamata raia wawili wa Tanzania na kuondoka nao.
Kwa mujibu wa habari hizo, ufuatiliaji wa kujua waliokamatwa na kuchukuliwa na askari hao ni akina nani unaendelea.
Hata hivyo, wananchi wanaoishi Mutukula walidai kuwa siyo mara ya
kwanza askari kutoka Uganda kuvamia eneo hilo na kukamata Watanzania
wanaoishi mpakani na kuondoka nao bila kushirikisha polisi wa Tanzania.
“Huu siyo utaratibu. Ni ubabe. Hata kama kuna Watanzania wanawahisi
kuhusika na uhalifu katika nchi yao, inabidi wafuate utaratibu kwa
kutoa taarifa ili askari wa Tanzania washiriki kuwatafuta wahalifu
husika,” alisema mwananchi mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa.
Kwa mujibu wa wananchi hao, askari walioingia nchini na kufanya
tukio hilo ni askari polisi kutoka eneo la Mbarari nchini Uganda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga, alipoulizwa na
waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na tukio hilo,
alithibitisha, lakini akasema yeye hana mamlaka ya kulizungumzia zaidi
mpaka apate ruhusa kutoka Makao Makuu ya Polisi.
“Hili ni suala la kiusalama linalohusisha nchi na nchi, siwezi
kulizungumzia zaidi, tunachokifanya kama kamati ya ulinzi na usalama ya
mkoa tunaandaa taarifa tuitume polisi makao makuu, wenyewe ndiyo
wataamua kama ni kuniruhusu mimi nizungumze au wazungumze wao makao
makuu,” alisema Kamanda Mayunga.
Kamanda huyo alisema kuwa kwa kawaida masuala yanayohusu nchi na
nchi serikali huwa inakuwa makini sana kuyazungumzia, hivyo subira
inahitajika ili watoe taarifa iliyo sahihi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu jijini Dar es Salaam, Advera
Senso, alipoulizwa na NIPASHE jana, alisema kinachopfanywa na jeshi
hilo kwa sasa ni kuchunguza kujua ilikuwaje askari hao watoke Uganda na
kuingia Tanzania bila kuwaarifu polisi wenzao wa Tanzania.
“Tunahitaji kufanya hivyo ili kila nchi ijiridhishe. Hilo ndilo
suala la msingi ki-nchi na kisera. Na hiyo ndiyo maana ya kuwapo
Interpol (Polisi wa Kimataifa). Tuna ushirikiano,” alisema Senso.
Hata hivyo, alisema baada ya undani wa suala hilo kujulikana, taarifa zitatolewa na jeshi hilo ngazi ya mkoa (Kagera).
0 comments:
Post a Comment