MABWENI saba ya
wavulana wa Shule ya Sekondari Ivumwe, mkoani hapa, inayomilikiwa na
Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), yameteketea kwa moto na kuteketeza vifaa mbalimbali vya wanafunzi wa shule hiyo.
Moto huo ulizuka jana majira kati ya saa tatu na nne asubuhi wakati wanafunzi hao wakiwa madarasani kuendelea na masomo yao.
Akitoa taarifa mbele ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi taifa, Abdallah Majura Bulembo, aliyefika mkoani hapa kujionea janga hilo, Mkuu wa shule hiyo, Emmery Muhondwa, alisema mbali na kuteketeza mabweni hayo, hakuna madhara ya kibinadamu.
Mwalimu Muhondwa alisema moto huo uliteketeza vitanda 93, magodoro 186, mashuka 372, blanketi 186, mabegi 186, matranker 186 pamoja na vitabu na madaftari, vyote vikiwa na jumla ya thamani ya sh milioni 30.
“Katika kukabiliana na hali hiyo, tumewahamishia wanafunzi katika madarasa yaliyokuwa yanatumiwa na kidato cha sita ili walale humo, tumeazima magodoro 169 kutoka Shule ya Sekondari ya Loleza na tunawasiliana na wazazi ili wawanunulie nguo za kushindia na za shule huku tukiendelea kukarabati mabweni,’’ alisema Mwalimu Muhondwa.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo taifa, Bulembo, aliwapa pole wanafunzi na kuwataka wawe wavumilivu katika kipindi hiki.
Pia alitoa mchango aliouita wa dharura wa sh milioni tatu kwa ajili ya ukarabati wa mabweni na mahitaji mengine ya haraka na kuahidi kuwashirikisha wadau wengine wa elimu ili kuwasaidia wanafunzi hao.
Mbali na mchango huo, alitoa tamko kuzitaka shule zote zinazomilikiwa na jumuiya hiyo kuwa na bima ya moto.
“Kuanzia sasa, suala la bima ya moto ni la lazima kwa shule zote za jumuiya ya wazazi wa CCM. Baraza Kuu tutakutana kwa dharura mjini Dodoma Mei 17, mwaka huu na tutakachokipata tutakileta haraka kwenu ili kusaidia janga hili la moto,’’ alisema Bulembo.
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Dk. Victoria Kanama, alimshukuru mwenyekiti huyo kwa mchango wake.
“Tutahakikisha tunakarabati mabweni haya ndani ya mwezi mmoja na kufanya jitihada za kuongeza ufanisi wa ufaulu katika shule yetu,” alisema Dk. Kanama.
Ivumwe, ni kati ya shule zenye sifa ya kufaulisha ambapo katika mtihani wa utamilifu (Mock), kidato cha sita mwaka huu, shule hiyo imeshika nafasi ya pili kati ya shule 26 zilizokuwa na watahiniwa 30 Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
0 comments:
Post a Comment