WAKATI vyombo mbali mbali zikiendelea na jitihada
za kuwaelimisha wananchi juu ya madhara ya kujichukulia sheria mkononi
hali hiyo bado ni tete mkoani Mbeya.
Hali hiyo imezidi kujitokeza baada ya Wananchi wenye
hasira kali wa Mwasanga Ivumwe jijini Mbeya kumpiga na kumchoma moto
mwananchi mmoja ambaye jina lake halikupatikana mara moja wakimtuhumu
kwa Wizi wa Ng’ombe mmoja na ndama.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo ameuambia mtandao
huu kuwa tukio hilo lilitokea mapema leo asubuhi ambapo chanzo ni wizi
wa Ng’ombe wa Kongoro Mwakitalima mkazi wa Isyesye kata ya Ilomba.
Alisema Ng’ombe huyo aliibiwa jana majira ya usiku
ambapo mzee huyo alitoa taarifa kwa majirani ambao asubuhi walijihimu
kutafuta ambapo walipofika maeneo ya Ivumwe walikutana na mwendesha boda boda ambaye aliwaambia amekutana na mtu akiwa anaswaga hiyo mifugo.
Alisema baada ya kusikia hivyo waliamua kuanza
kumfukuzia wakitumia bodaboda na ndipo walipofika eneo la Mwasanga
relini walimkuta mtuhumiwa akiwa na hao Ng’ombe.
Alisema Wananchi mbali mbali walikusanyika na kuanza
kumshushia kipigo kutokana na eneo hilo kukithiri kwa wizi wa mifugo
lakini baada ya kipigo hicho mtuhumiwa alionekana kuwa ngangari jambo
lililowatia hasira na kuamua kumchoma moto.
Shuhuda huyo aliendelea kusema baada ya kuanza kumchoma
lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida mtu huyo hakuweza kukata roho
hadi alipookolewa na Askari wa jeshi la polisi walipofika eneo la tukio.
Hadi tunaingia mtamboni hakuna taarifa zilizothibitisha kama mtuhumiwa huyo bado yuko hai ama amepoteza maisha.
CREDIT: MBEYA YETU
0 comments:
Post a Comment