Ligi ya mabingwa barani Ulaya , Champions League inarejea uwanjani tena
Jumanne na Jumatano wakati kukiwa na mechi kadhaa za kukata na shoka
katika viwanja mbalimbali
Kocha wa klabu ya Roma ya Italia ameahidi kuipatia Bayern Munich ya
Ujerumani makaribisho ambayo hawatayasahau, wakati mafahali hao wa
Bundesliga wakiwasili katika mji huo mkuu wa Italia kuvuruga mwanzo
mzuri wa timu hiyo , "Giallorossi" katika kampeni ya Champions League
msimu huu.
Roma ilijipasha moto kwa ajili ya pambano hilo la kesho katika kundi E
kwa kuiadhibu Chievo kwa mabao 3-0 siku ya jumamosi na licha ya ushindi
wa kishindo wa Bayern dhidi ya Werder Bremen katika Bundesliga , kocha
Garcia wa Roma anataka uwanja wao wa "Stadio Olimpico" kuwapa wenyeji
kitu cha ziada.
AS Roma wa Italia wanawakaribisha miamba wa Ujerumani Bayern Munich
Bayern inasafiri kwenda Roma ikiwa inaongoza kundi hilo baada ya kupata
ushindi mara mbili dhidi ya Manchester City na CSKA Moscow, na Roma
ilipata ushindi mnono dhidi ya CSKA na kutoka sare na Manchester City,
ikiwa inashikilia nafasi ya pili. Manchester City iko nyumbani kwa CSKA
Moscow, ambapo itacheza bila mashabiki uwanjani kutokana na adhabu
inayoikabili CSKA. Kocha wa Manchester City Manuel Pellegrini amesema
kucheza bila mashabiki hakutaisaidia timu yake katika mchezo huo muhimu
wa Champions League kesho.
Roberto di Matteo alikwisha nyanyua juu taji hilo la Champions League
mwaka 2012 akiwa kocha mlezi wa Chelsea lakini kibarua kiliota majani
katikati ya msimu wake kamili akiwa kocha wa timu hiyo. Hivi sasa
amerejea katika dimba hilo la mabingwa akiwa kocha kamili wa Schalke 04.
Di Matteo anakabiliwa na changamoto dhidi ya Sporting Lisbon kesho
nyumbani Gelsenkirchen, kabla ya kukabiliana na mwajiri wake wa zamani
Chelsea hapo Novemba 25.
Nyota wa Madrid Cristiano Ronaldo anaendelea kuzitembelea nyavu za wapinzani kama anavyotaka
Chelsea inakwaana na Maribor kesho uwanjani Stanford Bridge na inapaswa
kuwa macho na kujihadhari isije kukutwa katika usingizi, licha ya kuwa
inaoongoza katika Premier League.
Barcelona inahitaji kuepuka kuvutwa fikira zao kuelekea katika mchezo wa
watani wa jadi nchini Uhispania , El Clasico , dhidi ya Real Madrid
Jumamosi ijayo wakati watakapokutana na Ajax Amsterdam katika pambano la
Champions League kesho.
Macho yote nchini Uhispania yako katika mpambano wa vigogo vya soka la
nchi hiyo Barca ikipambana na Real Madrid , mashabiki wakitaraji kurejea
dimbani kwa mshambuliaji wa Uruguay Luis Suarez baada ya marufuku ya
kucheza kwa muda wa miezi minne kwa kumng'ata mlinzi wa Italia Giorgio
Chiellini katika mchezo wa kombe la dunia.
Lakini Real Madrid pia ina miadi na Liverpool wakati vigogo hivyo vya
soka barani Ulaya vikifufua uhasama wao siku ya Jumatano watakapokutana
uwanjani Anfield wakati Liverpool ikijaribu kuweka rekodi yao ya
asilimia 100 dhidi ya Real Madrid.
Kazi katika uwanja wa Luzhniki ambao utafanyika fainali ya kombe la
dunia mwaka 2018 inaendelea vizuri kama ilivyopangwa, amesema mkaguzi
mkuu wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Chris Unger. Hii ni tofauti
kabisa ikilinganishwa na uchelewesho ulioikumba Brazil katika ujenzi wa
viwanja kwa ajili ya fainali za kombe la dunia mwaka huu.
|
0 comments:
Post a Comment