Vyama hivyo vitalazimika kufanya uamuzi katika sera tofauti za vyama vyao, kukabiliana na Sheria ya Uchaguzi, taratibu za kupata wagombea wa kuanzia ngazi ya chini hadi urais na jinsi ya kuendesha kampeni zao kabla ya kuwaendea wananchi kuwaeleza kuwa wameshajizatiti kukabiliana na chama tawala, ambacho kina mtandao karibu nchi mzima uliojengwa kwa miaka mingi.
Vyama hivyo vimeibuka na nguvu mpya baada ya kuunganishwa na hoja ya kutetea Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilielezewa kuwa ilitokana na maoni ya wananchi na hivyo kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupambana na wajumbe wa CCM kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Vyama hivyo, Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD vilisusia mchakato wa Katiba kwa kile vilichodai kuwa ni kutoridhishwa na mambo yalivyokuwa yakiendeshwa na sasa umoja wao umekwenda mbali zaidi kutaka kushirikiana kwenye chaguzi.
Kutekeleza hilo, Jumapili iliyopita wenyeviti wa vyama hivyo, Profesa Ibrahimu Lipumba (CUF), Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR- Mageuzi) na Dk Emmanuel Makaidi (NLD) walisaini makubaliano ya ushirikiano huo katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Jangwani.
Moja ya kazi ngumu inayoukabili umoja huo ni jinsi ya kumpata mgombea wa urais atakayetoa upinzani mkubwa zaidi kwa mgombea wa chama tawala na kuendelea kupunguza kura za CCM baada ya mafanikio ya mwaka 2010 ya kupunguza asilimia 20 za kura alizopata RaisJakaya Kikwete mwaka 2005.
Kazi hiyo ngumu inatokana na tofauti za kisera baina ya vyama hivyo, wagombea urais wanaoonekana kuwa na sifa na matokeo ya uchaguzi uliopita uliompa mgombea wa Chadema, Dk Willibrod Slaa asilimia 26 ya kura zote na kuweka rekodi ya upinzani kukusanya kura nyingi.
Wakati Chadema ikitegemea mtaji wa Dk Slaa, ambaye ni katibu mkuu wa Chadema, wa asilimia 26.34 ya kura za mwaka 2010, CUF imekuwa ikimsimamisha mwenyekiti wake, Prof Lipumba katika chaguzi nne zilizopita, huku NCCR-Mageuzi ikiwa na mwenyekiti wake, james Mbatia na NLD ikiwa na Makaidi.
Mbowe alisema hilo halitakuwa tatizo kubwa katika kufikia uamuzi wa mgombea urais.
“Kwanza niseme tu kuwa hapa tulipofika haikuwa rahisi sana kama watu wanavyodhani, kwa hiyo yako mengi ambayo yamefanyika kwa kujadiliana na katika mchakato huu tumejifunza mengi. Kwa hiyo taratibu zitawekwa na zitafuatwa. Kutakuwa na vigezo na mambo kama hayo,” alisema mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alipozungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki akijaribu kuonyesha kuwa wamezingatia mambo mengi kabla ya kusaini makubaliano hayo.
“Suala la mgawanyo wa nafasi za kugombea haliwezi kutugombanisha. Ushindani si jambo geni kwetu maana tumekuwa na ushindani siyo sasa tu, bali hata ndani ya vyama. Hata katika chama kimoja huwa kuna wagombea zaidi ya mmoja.”
Kauli ya Mbowe iliungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ambaye alisema ili kuondoa utata wowote unaoweza kujitokeza, kamati ya ufundi itaundwa kwa ajili ya kushughulikia masuala yote muhimu.
“Kamati hiyo itakayojumuisha vyama vyote, itatakiwa kutoa mwongozo wa nini kifanyike kulingana na masilahi na changamoto iliyopo kama inavyoelezwa katika azimio la Ukawa,” alisema Kafulila.
Uwezekano mkubwa ni Ukawa watalazimika kuamua kati ya Dk Slaa na Profesa Lipumba kwa kuwa tayari Mbatia, ambaye kwa sasa ni mbunge wa kuteuliwa, ameshaanza kampeni za kuwania ubunge wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro.
Historia ya kugombea
Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Profesa Lipumba alipata kura 418,973, ikiwa ni asilimia 6.43 ya kura zote na kushika nafasi ya tatu akiwa nyuma ya mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa aliyeibuka mshindi na Augustine Mrema.
Profesa Lipumba aliingia tena uchaguzi wa mwaka 2000 na kushika nafasi ya pili baada ya kuzoa kura 1,329,007 (sawa na asilimia 16.26) akiwa nyuma ya Mkapa na uchaguzi uliofuata alipata kura 1,327,125 (sawa na asilimia 11.68) kabla ya kushuka tena mwaka 2010 alipopata kura 695,667 (asilimia 8.06).
Dk Slaa alishangaza wengi alipoamua kutogombea ubunge mwaka 2010 baada ya Chadema kumteua kugombea urais. Mwaka huo, Dk Slaa alipata kura 2,271,941 (sawa na asilimia 26.34), matokeo ambayo yalishusha ushindi wa kishindo wa CCM wa mwaka 2005 kutoka asilimia 80.28 hadi asilimia 61.17 mwaka 2010.
Takwimu hizo na masuala mengine yatakuwa moja ya mambo ambayo Ukawa watalazimika kukuna vichwa kabla ya kumchagua mgombea wao.
Jambo ambalo litakuwa faraja kwao ni kuongezeka kwa idadi kubwa ya kura za wapinzani mwaka 2010.
Mwaka 1995 jumla ya kura za wapinzani zilikuwa 2,486,323, sawa na asilimia 38.17, lakini uchaguzi uliofuata 2000 wapinzani walipata jumla ya kura 2,309,123, sawa na asilimia 28.26 na kupungua zaidi mwaka 2005 walipopata kura 2,241,525 (sawa na asilimia 19.72. Mwaka 2010, upinzani uliibuka kwa nguvu na kusomba kura 3,121,136. Ingawa kwa asilimia, kura hizo zilikuwa asilimia 37.16 pungufu ya asilimia za uchaguzi wa 1995, idadi ya kura za wapinzani ilikuwa kubwa kwa tofauti ya zaidi ya kura 700,000, hali inayoashiria mwamko mpya kwa wapinzani.
“Kwa sasa wanatakiwa kuwa makini na propaganda za CCM, kwani ni rahisi kusambaratishwa kabla ya 2015. Hivyo wahakikishe wanapata mgombea atakayekuwa tishio kwa CCM,” alisema Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
“Ni muhimu kama wamesaini makubaliano hayo wakati kuna jambo zito mbele yao na bado kuna hofu ya kuimarika kwao.”
Pia, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Eligius Danda alionyesha wasiwasi, akisema umoja huo umejikita zaidi katika kutafuta njia ya kwenda Ikulu, akiungana na mawazo ya Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitila Mkumbo.
“Wote wanne bado nina wasiwasi na dhamira zao. Viongozi walioko kwenye fikra ya madaraka siyo viongozi sahihi kwenye vyama vya siasa,” alisema Danda.
Danda alisema ili muungano huo uwe na nguvu na kukubalika, ni lazima dhamira zao ziwe katika kushughulikia matatizo ya msingi ya wananchi, lakini siyo kujikita katika kutafuta madaraka.
Suala la mgombea urais wa Zanzibar halionekani kuwa na kikwazo kikubwa kutokana na nguvu ya CUF visiwani humo pamoja na kukubalika kwa katibu mkuu wake, Maalim Seif Sharrif hamad.
Kumalizika kwa suala la urais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar, kutafungua mlango kwa suala jingine gumu kutafutiwa ufumbuzi; wagombea wa ubunge katika majimbo, hasa ya Bara.
Vyama hivyo vimejenga ngome zake katika maeneo tofauti Bara na Zanzibar. Wakati CUF ina uhakika na viti vingi vya Zanzibar, hasa Pemba na baadhi ya mikoa ya Bara, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD vimegawana majimbo ya Bara, huku Chadema ikiongoza kwa kuwa na majimbo mengi.
Kazi ngumu itakuwa ni kuamua mgombea katika majimbo ambayo wagombea wa vyama hivyo wanapambana vikali, hasa majimbo ya Ubungo, Vunjo na Tarime.
Katika Jimbo la Ubungo, Ukawa watalazimika kufanya uamuzi kati ya mbunge wa sasa kutoka Chadema, John Mnyika na Julius Mtatiro wa CUF, wakati jimbo la Vunjo linaweza kuwa na mvutano baina ya Mbatia na John Mrema wa Chadema, ambao wameonyesha nia ya kuwania ubunge, huku CUF na Chadema wakichuana Tarime ambako jumla ya kura zao kwenye uchaguzi uliopita zingeweza kumuondoa mgombea wa CCM. Hali hiyo iko katika majimbo mengi ambayo vyama hivyo vilipambana vikali mwaka 2010.
Katika majimbo ambayo CCM ina nguvu, Ukawa wanaweza kuwa na matatizo zaidi katika kufanya uamuzi kwa kuwa yanaweza kuzua wagombea wengi kutoka vyama vinavyounda umoja huo ambao watadai kuwa ndio wanaoweza kupambana na chama hicho tawala. Mikoa kama ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Ruvuma na wilaya ambazo ziko pembezoni, CCM ina nguvu kubwa, lakini Ukawa itakuwa katika hali ngumu kufanya uamuzi wa kupata mgombea
.
0 comments:
Post a Comment