pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Vietnam kuleta simu za kisasa Tanzania

Vietnam kuleta simu za kisasa
KAMPUNI ya Viettel ya Vietnam, inakusudia kuingia katika soko la simu la Tanzania kwa kuleta simu za kisasa zenye uwezo mkubwa (smart phone) kwa bei ya chini katika miaka mitano ijayo kuanzia 2020.
Kampuni hiyo, ilimweleza hayo Rais Jakaya Kikwete juzi, kuwa itateremsha kwa kiasi kikubwa bei ya simu za kawaida na smart phone, ili kuwezesha kila Mtanzania kuzinunua.
Rais Kikwete alielezwa hayo akiwa ziarani nchini humo, ambapo kampuni hiyo iliahidi pia kusambaza mawasiliano ya internet kwa kila kijiji nchini na kwa taasisi za umma kama vile shule, hospitali, vituo vya polisi, zitapatiwa huduma hiyo bila malipo yoyote.
Rais Kikwete aliambiwa habari hiyo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Simu ya Viettel wakati alipotembelea makao makuu yake yaliyopo mjini Hanoi. Mwenyekiti wa kampuni hiyo ya umma inayomilikiwa na Jeshi la Vietnam,  Nguyen Manh Hung alimwambia Rais Kikwete kuwa Viettel inakusudia kumwezesha kila Mtanzania kumiliki smart phone kwa kupunguza bei ya simu hiyo na pia huduma muhimu kama vile ile ya internet.
Alisema kuwa kampuni yake inapanga kupunguza bei ya simu za kawaida hadi kufikia dola za Marekani 15, sawa na sh. 25,000 na kupunguza ile bei ya smart phone hadi kufikia dola za Marekani 40, sawa na sh.65,000.
“Tunataka kuifanya bei ya kununua smart phone kuwa mara 10 chini ya bei ya kununua kompyuta. Tunasukudia pia kupunguza bei ya matumizi ya simu kuwa dola moja tu ya Marekani, sawa na sh. 1,600, kwa watu wa kawaida kwa mwezi na kwa wale ambao wanatumia simu kwa huduma nyingi zaidi watalipa dola za Merakani 50, sawa na sh. 78,000 kwa mwezi,” alisema Hung.
Amesema kuwa ndani ya miaka mitatu tokea kampuni hiyo kuanza shughuli zake katika Tanzania, kiasi cha vijiji 4,000 ambavyo kwa sasa havina mawasiliano vitapatiwa huduma hiyo katika awamu ya kwanza.
Rais Kikwete pia alishuhudia utiaji saini wa makubaliano katika usafiri wa majini (Marine Transport) ambao umetiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kwa niaba ya Tanzania  na Waziri wa Usafirishaji wa Vietnam, Dinh Li Thang kwa niaba ya nchi yake.

0 comments:

Post a Comment