Wapiganaji wa kikurdi katika mji wa Kobane nchini Syria wanaendelea
kupambana vikali na wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi linalojiita
dola la kiislamu IS huku wakisubiri kupigwa jeki na wenzao kutoka Iraq
Mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Syria Rami
Abdel Rahman amesema wanamgambo wa IS walifanya mashambulizi kutoka kila
upande wa mji wa Kobane jana jioni huku mapigano makali yakiripotiwa
kuendelea katika mji huo wa mpakani kati ya Syria na Uturuki
Wanamgambo hao wamewaleta wapiganaji zaidi kutoka Jarabulus hadi
magharibi mwa Kobane huku mashambulizi makali yakirejewa katikati mwa
mji huo kufikia mwishoni mwa jana.
IS wazidisha mashambulizi Iraq
Waasi hao wa IS pia wanaonekana kuzidisha makali ya mashambulizi yao
nchini Iraq hasa katika mji unaodhibitiwa na wakurdi wa Qara Tapah
ambapo kiasi ya watu kumi wameuawa na kusababisha maelfu ya wakaazi wa
mji huo kutoroka.
Mashambulizi hayo ya IS yanafanyika huku juhudi za jumuiya ya kimataifa
kukabiliana na kitisho hicho cha IS zikiongezeka. Mbali na Marekani
kuwadondoshea wapiganaji wa kikurdi silaha mjini Kobane hapo jana,
Uturuki imesema itawasaidia wapiganaji wa kikurdi wa Iraq.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema nchi yake
itasaidia katika kuwasaidia wapiganaji wa kundi la Peshmerga la Iraq
kuingia Syria kuelekea Kobane kuwasaidia wenzao kukabiliana na
wanamgambo wa IS.
Hata hivyo bado Uturuki imekataa kuwapa silaha na kuwaruhusu wapiganaji
wa kikurdi wa Uturuki kuvuka mpaka na kuingia Syria au Iraq kupigana.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje
wa Umoja wa Ulaya,Umoja huo umeihimiza Uturuki kufungua mipaka yake kwa
ajili ya kupelekwa kwa misaada mbali mbali kwa watu wa Kobane.
Marekani na Uturuki zawasaidia wakurdi
Akizungumzia kudondoshwa kwa silaha za aina mbali mbali Kobane kwa ajili
ya kuwahami wapiganaji wa kikurdi,waziri wa mambo ya nje wa Marekani
John Kerry amesema ni vigumu mno kulipa kundi lolote linalopigana dhidi
ya IS mgongo.
Marekani na washirika wake wamefanya mashambulizi 135 ya angani dhdi ya
IS karibu na mji wa Kobane lakini ilikuwa haijawahi kutoa silaha moja
kwa moja kwa wakurdi wanaokabiliana na IS.
Licha ya hayo, Marekani imesisitiza kuwa mkakati wake wa kukabiliana na
kundi hilo la dola la kiislamu bado linatuama zaidi nchini Iraq ambako
IS wanayadhibiti maeneo makubwa ya wasunni kaskazini na magharibi mwa
Baghdad tangu mwezi Juni mwaka huu.
Waziri mkuu wa Iraq Haidar al Abadi yuko mjini Tehran nchini Iran hii
leo kwa mazungumzo na viongozi wa Iran kuhusu vita dhidi ya IS. Waasi
hao wakijihadi wanadihibiti miji kadhaa iliyoko kilomita chache karibu
na mpaka na Iran na Tehran inaunga mkono vita dhidi yao.
0 comments:
Post a Comment