pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Vitambulisho vya Taifa kutumika uchaguzi ujao

VITAMBULISHO vya Taifa huenda vikatumika katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Rose Mdami wakati akitoa maelezo kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa bungeni mjini hapa katika hafla ya kumkabidhi kiongozi huyo wa Bunge kitambulisho chake cha taifa.
Mdami alisema tayari mamlaka hiyo imechukua taarifa za wapigakura kutoka kwenye kanzidata ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuzichakata na kuna uwezekano mkubwa vitambulisho vya taifa vikatumika katika uchaguzi ujao na kuirahisishia kazi tume hiyo kufanikisha uchaguzi huo wa Rais, Wabunge na Madiwani.
"Vitambulisho tunavyovitoa sasa vina saini ya mtu husika, hivyo vitatumika benki. Tumewashirikisha pia NEC ambao wametupa 'database' (kanzidata) yao, tumezichakata na tunaendelea na taratibu ili ikiwezekana Vitambulisho vya Taifa vitumike katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 badala ya vile vya tume," alisema Mdami.
Akishukuru, Ndugai aliipongeza mamlaka hiyo kwa kuwa na mipango mizuri, lakini akaishauri serikali kuweka sharti kuzilazimisha benki kutoruhusu mtu kufungua akaunti bila kuwa na kitambulisho cha taifa.
Spika pia alihoji sababu za Nida kuwa na vitambulisho vyenye rangi tatu tofauti na kujibiwa na Mdami kuwa kitambulisho cha kwanza ni cha raia mzawa, cha pili cha raia wa kigeni anayeishi nchi na cha mwisho kwa ajili ya wakimbizi.
"Kwa sasa si rahisi mkimbizi kujichanganya mitaani huko na kupatiwa kitambulisho cha taifa. Tunashirikiana na Tamisemi kuhakikisha hakuna udanganyifu tena. Mtu anayejaza fomu ya kupatiwa kitambulisho anatakiwa kupitia vipengele 72 ambavyo si rahisi kuvighushi kama si mzawa," alisema Mdami.

0 comments:

Post a Comment