pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Bosi wa Fastjet kizimbani




 

MENEJA wa Wafanyakazi wa Ndani ya Ndege wa Kampuni ya Fastjet, Emma Donovan, alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, kujibu shtaka linalomkabili la kutoa lugha ya matusi.
Emma (40) alipandishwa kizimbani jana na kusomewa shtaka hilo na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, mbele ya Hakimu Joyce Minde. Katuga alidai Machi 19, mwaka huu, Emma alimtolea lugha ya matusi, Samson Itinde, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Emma alikana shtaka hilo, ambapo Katuga alidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe kwa usikilizwaji wa awali.
Hakimu Joyce alisema kuwa dhamana ya mshtakiwa iko wazi lakini kwa kuzingatia vigezo vya dhamana vitakavyotolewa kwa kuwa mshtakiwa ni raia wa kigeni.
Alitaja masharti ya dhamana kuwa mshtakiwa kuwasilisha hati yake ya kusafiria au kutoa fedha taslim sh milioni tano na pia awe na wadhamini wawili ambao ni Watanzania. Kutokana na uamuzi huo, kulijitokeza hali ya sintofahamu mahakamani hapo hususan kutoka kwa wadhamini wawili ambao ni Watanzania waliokuwa wanataka kumdhamini Emma.
Hilo lilisababishwa na wadhamini kushindwa kujibu kwa ufasaha baadhi ya maswali waliyokuwa wanaulizwa na hakimu Joyce ikiwemo kutaja majina ya mwenyekiti wa serikali yake ya mtaa na balozi wa nyumba kumi.
Hata hivyo, baada ya dakika 10, watu hao waliweza kupata majina ya watu hao ambao awali walikuwa hawawafahamu majina yao kwa madai kuwa huwa hawashindi majumbani kwao kwa muda mrefu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 9 ili kupangwa tarehe ya kuanza kwa usikilizwaji wa awali.





chanzo Tanzania daima

0 comments:

Post a Comment