pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

MKOA WA KAGERA WAANDALIWA KUWA KITOVU CHA BIASHARA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Daktari Shaban Mwinjaka Aliye Nyuma ya Mike Akifafanua Jambo Katika Mkutano na Wadau na Wajasiliamali Mkoani Kagera.

 Picha ya Pamoja Baada ya Kumalizika Mkutano na Wadau Kwenye Mazingira ya Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera.




Wizara ya Viwanda na Biashara yauandaa Mkoa wa Kagera kuwa kitovu cha biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ili wajasiliamali pamoja na wasafirishaji kutoka mkoa huu na Tanzania nzima kunufaika katika kufanya  biashara kwenye mazingira mazuri.
Ili kuweka mazingira mazuri ya biashara  na kuwaandaa wajasiliamali na wafanyabiashara  kufanya biashara katika nchi za Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda na Biashara  imefanya mkutano wa wadau  na wajasiliamali  mkoani Kagera ulioongozwa na Naibu Katibu wa Wizara hiyo Daktari Shaban Mwinjaka.
Dhumuni kubwa la wizara hiyo kufanya mkutano wa wadau  katika mkoa wa Kagera ilikuwa ni kuwajengea uwezo wajasiliamali na wafanyabiashara wa mkoa wa Kagera kuona uwezekano wa upatikanaji wa fulsa zaidi za kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pia kuwajengea uwezo wajasiliamali na wafanyabiashara ili wazalishe bidhaa zitakazokidhi na kufikia viwango vya kimataifa kwa kukusudia  ushindani katika masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Vilevile kuwaongezea ujuzi na uelewa wa uzalishaji na undeshaji wa biashara pia utafutaji wa masoko zaidi.
Naibu Katibu Mkuu Daktari Shaban Mwinjaka  aliwaeleza wadau kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara imeanza  kufanya mikutano ya wadau kwa kuanza na Kanda ya Ziwa hususani mkoa wa Kagera  ili kuhakikisha wafanya biashara wananwezeshwa kifulsa  na wanafanya biashara mpaka Sudani Kusini.
Wizara ya Viwanda na Biashara  imeamua kujenga soko kubwa la Kimataifa katika mpaka wa Tanzania na Uganda (Mtukula) litakalojumuisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na nchi nyingine.  Aidha soko  hilo litakalokuwa na viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani ya bidhaa kabla ya kuuzwa ili kukidhi ushindani na kuongeza ajira kwa watanzania.
“Tumeanza kufanya mikutano na wadau katika Mkoa wa Kagera ili wizara yetu ieleweke kwa wadau pia kuondoa utamaduni wa mazoea ya siku zote yaliyozoeleka katika jamii kuwa wizara inafanya kazi na wafanyabiashara wakubwa na viwanda vikubwa tu.” Aliongeza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biasha, Daktari Shaban Mwinjaka.
Aidha kwa upande wa wadau na wafanyabiashara waliohudhuria katika mkutano huo waliiomba Wizara ikishirikiana na uongozi wa Mkoa kuhakikisha wanaondoa vikwazo vya biashara mfano beria ambazo ni tisa  kutoka Bukoba mjini mpaka Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda ili uwepo urahisi katika kusafirsha bidhaa zao.
Naye Katibu Tawala Mkoa Bw. Nassor Mnambila aliishukuru Wizara ya Biashara na Viwanda kwa kufanya mikutano hiyo ambayo ni muhimu sana katika kuwajengea uwezo wajasiliamali na wafanya biashara. Pia aliwahakikishia wadau kuwa atashirikiana na Idara mbalimbali za serikali zinazohusika kujadili uwezekano wa kupunguza beria ili kurahisisha fulsa za biashara  katika mkoa.
Imeandliwa na:
Sylvester Raphael
AFISA HABARI MKOA
KAGERA @ 2013
chanzo: bukobawadau

0 comments:

Post a Comment