pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Wafuasi wa Ponda watupwa jela




WAFUASI 52 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya maandamano haramu, wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila mmoja.

Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana, baada ya wafuasi hao kukutwa na hatia kwa makosa matatu kati ya manne yaliyokuwa yakiwakabili. Hata hivyo watakaa jela kwa mwaka mmoja kutokana na adhabu zote kwenda kwa pamoja.

Hata hivyo aliyekuwa mshtakiwa wa 48, Waziri Omar Toy, aliachiwa huru baada ya Mahakama kuridhika kwamba hana hatia kutokana upande wa mashtaka kushindwa kuthitibisha madai dhidi yake.

Baada ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo kusoma hukumu hiyo, ilizuka tafranwi miongoni mwa ndugu wa washtakiwa hao ambapo wengine waliangua vilio na wengine kuanguka na kujigaragaza chini.

Mwanamke ambaye ni ndugu wa washtakiwa hao, alionekana kama mtu “aliyepandwa mashetani” na kutaka kumvamia askari wa kike ambaye katika kujihami alimpiga ngumi, kisha watu wakafanikiwa kumdhibiti kumshika.

Hakimu Fimbo katika hukumu hiyo alisema baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za pande zote pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo ameridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka matatu dhidi ya washtakiwa hao.

Hata hivyo, Hakimu Fimbo alisema kuwa katika shtaka la uchochezi lililokuwa likiwakabili washtakiwa wanne, upande wa mashtaka umeshindwa kulithibitisha.

“Mahakama imeridhika na ushahidi uliwasilishwa na upande wa mashtaka kuwa umethibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa wote isipokuwa mshtakiwa wa 48,” alisema Hakimu Fimbo na kuongeza:

“Hivyo Mahakama imewatia hatiani washtakiwa wote isipokuwa mshtakiwa wa 48, katika shtaka la kwanza, la pili na la tatu na katika shtaka la nne, Mahakama imeona kuwa washtakiwa hawana hatia.”

Washtakiwa walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama za kutenda makosa, kufanya maandamano yaliyozuiwa na Polisi na kwa pamoja kufanya mikusanyiko haramu na kusababisha uvunjifu wa amani.

Akitoa adhabu kwa washtakiwa hao baada ya kuwatia hatiani, Hakimu Fimbo alisema: “Nimezingatia kuwa karibu kila mshtakiwa ana majukumu ya kifamilia na kwa kuzingatia `nature’ (asili) ya mashtaka.”

Aliongeza: “Katika kosa la kwanza ninawahukumu kifungo cha mwaka mmoja jela na kosa la pili pia mwaka mmoja jela na tatu mwaka mmoja jela. Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja.”
CHANZO MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment