Pemba. Mbunge wa Chambani, Salim Hemed Khamis amezikwa kijijini kwake Mizingani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Sief Sharif Hamad aliongoza mamia ya wananchi kwenye mazishi hayo.
Awali, Rais Jakaya Kikwete aliongoza mamia ya
wakazi wa Dar es Salaam kuaga mwili wa Mbunge wa Chambani, Salim Hemed
Khamis (CUF) kwenye viwanja vya Karimjee, aliyefariki dunia juzi
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema Bunge
limepoteza mtu shupavu ambaye alikuwa mchangiaji mzuri kwa kutoa hoja
zenye lengo la kujenga.
Lukuvi aliwataka wananchi wa Chambani kuwa wastahimilivu wakati huu wa msiba, baada ya kuondokewa na kiongozi wao mpendwa.
Alisema licha ya kuwa mbunge wa upinzani, lakini
hoja zake zililenga kukosoa Serikali na kurekebisha na kwamba, pale
alipobaini upungufu na daima hakusita.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Mbunge wa
Mtambilem Masoud Salim alisema Serikali zote mbili na uongozi wa Bunge
wamefanya kazi mzuri kuanzia hospitali hadi maziko yake.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema chama chake kimepoteza kiongozi na mwanachama mzuri na kwamba,
itakuwa vigumu kuziba pengo hilo.
Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Spika wa Bunge,
Anne Makinda, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Edward
Lowassa na viongozi mbalimbali.
Awali, viongozi waliohudhuria kutoa heshima za
mwisho mjini Dar es Salaam, ni Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal,
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa na wabunge
mbalimbali.
Akisoma historia fupi ya marehemu Khamis, Kaimu
Katibu wa Bunge, John Joel alisema kulingana na taarifa za madaktari
alikuwa anasumbuliwa na shinikizo la damu.
chanzo mwananchi
0 comments:
Post a Comment