pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Waendesha ‘bodaboda’ wamuua polisi


Waendesha pikipiki maarufu ‘bodaboda’ wa Kijiji cha Ngwinde Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wamemuua Polisi, Konstebo Yohana baada ya kumpiga na gongo kichwani, muda mfupi baada ya polisi huyo kumuua mwenzao, Makisio Nganyuni (25) kwa kumpiga risasi kwenye paji la uso.
Tukio hilo lilitokea jana saa 5 asubuhi katika barabara kuu iendayo Tunduru, Masasi baada ya waendesha pikipiki hao zaidi ya sita kumvamia askari pamoja na mwenzake, Venance Kamugisha waliokuwa katika pikipiki ya polisi.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Deus Nsimeki alisema polisi hao walikuwa katika mizunguko ya kawaida, walipofika katika Kijiji cha Ngwinde walikutana na Katibu wa CCM wa kijiji hicho, Shaban Ngae ambapo walianza kuzungumza naye.

“Wakati wakizungumza lilitokea kundi la waendesha pikipiki (bodaboda) zaidi ya sita wakiwa wamepakizana, walipowakaribia walianza kurushiana maneno na polisi,” alisema na kuongeza;

“Baadaye watu hao walianza kurusha mawe ndipo polisi hao walipoanza kupiga risasi za moto juu, lakini walipozidiwa walianza kuwashambulia watu hao, ambapo risasi moja ilimpata Nganyuni.”

Baada ya kijana huyo kupigwa risasi hiyo na kufa papohapo, wananchi hao walianza kumshambulia Konstebo Yohana kwa kumpiga gongo kichwani. Alikufa palepale.

“Wakati hayo yakitokea Kamugisha alipigwa mpaka akapoteza fahamu, wananchi waliokuwa eneo hilo walimchukua na kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Songea,” alisema Nsimeki.

chanzo Mwananchi

0 comments:

Post a Comment