pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Wasomali wapewa ekari 100 kinyemela Rufiji


 



Rufiji: Watu wawili wanaodaiwa kuwa raia wenye asili ya Somalia, wamepewa ekari 100 za ardhi na Halmashauri ya Kijiji cha Chumbi C, Kata ya Chumbi, wilayani hapa bila kushirikisha wananchi wala uongozi wa wilaya.
Wakizungumza wilayani hapa juzi, baadhi ya wananchi walisema  raia hao mmoja hawezi kabisa kuzungumza Kiswahili, walikabidhiwa eneo hilo karibu na ilipokuwa Shule ya Msingi Chumbi  C.
Inadaiwa Wasomali hao wameweka kambi eneo la shule, wamekwenda Dar es Salaam kwa mapumziko ya Sikukuu ya Pasaka na wanatarajia kurejea wiki ijayo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Athuman Mtimbuko alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, alisema  hayupo tayari kuzungumza na mwandishi wa habari hizi kwa sababu ana ugomvi binafsi.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chumbi, Bakari Ngongota alipoulizwa kuhusiana na Wasomali hao, alisema amepata taarifa zao na waliofika kijijini hapo kuomba ardhi kwa ajili ya kilimo cha mtama, walipewa na halmashauri ya kijiji.
Ngongota alisema uongozi wa kijiji hicho umekuwa ukitoa ardhi ovyo bila kumpa taarifa na kwamba, mambo ya kijiji hicho yamekuwa yakifanyika kwa siri na kuahidi kufuatilia zaidi.
Ngongota alisema ameelezwa na ofisa mtendaji wa kijiji kuwa, watafanya mkutano wa kuwatambulisha Wasomali hao wiki ijayo lakini hawakutoa taarifa rasmi kwake hadi alipouliza.

0 comments:

Post a Comment