Kyerwa. Diwani wa Kata ya Mabila,
Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera, anatuhumiwa kufanya mauaji ya
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyakatete, Danes Damian na Msaidizi wake,
Johnson Damian wakidaiwa kufungiwa kwenye nyumba yake na kuteswa kabla
ya kufariki.
Mauaji hayo yalitokea Machi 13, mwaka huu baada
ya viongozi hao kutekwa wakiwa shambani na kundi la watu akiwatuhumu
kuhusika na kifo cha mtoto wa diwani huyo, kilichotokea mwaka jana.
Kijana aliyeshuhudia utekaji huo, Kamugisha Damian
alidai siku hiyo jioni akiwa na Danes wakichimba viazi, ghafla
walivamiwa na kundi la vijana lililoongozwa na diwani ambaye alitoa amri
wakamatwe naye akaambiwa alale kifudifudi.
Katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja, watu sita
wameuawa kijiji hicho cha Omukagando, mauaji yanayodaiwa kufanywa na
kundi linalojiita ‘Hakuna Kulala’.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi
alithibitisha kuwapo kwa mauaji hayo na kwamba, diwani huyo anasakwa
baada ya kutoroka na gari lake akiwa na baadhi ya vijana anaodaiwa
kushirikiana nao.
Alitaja tukio hilo kama la kikatili na juhudi za
polisi kumnasa diwani huyo na kundi lake, hazijafanikiwa baada ya
kutorokea sehemu isiyojulikana. Ofisa Mtendaji Kata ya Mabila, Herman
Leonard alisema alipigiwa simu na diwani akimtaka afike ofisini kupokea
watuhumiwa aliodai anawatafuta muda mrefu.
chanzo mwananchi
0 comments:
Post a Comment