Dar es Salaam, Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimejipanga kutumia Bunge la Bajeti, kumpana Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, azitoe ripoti za kamati kadhaa zilizowahi kuundwa
kufuatilia masuala elimu nchini.
Pia uongozi wa Chadema umepania kutumia nafasi hiyo kuwasilisha bungeni, nyaraka zinaonyesha jinsi Kampuni ya Jitegemee,
inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ilivyopewa mamilioni ya fedha kwa namna ya ufisadi.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio yaliyofikiwa na
Kamati Kuu ya chama hicho.
Kamati hiyo imekuwa na kikao kilichotarajiwa kumalizika juzi, lakini kimeongezwa siku zaidi.
“Kamati Kuu ya Chadema imelazimika kuongeza siku
za kukutana hadi leo (jana), tupo hapa kutokana na wingi wa agenda
zilizopo, ambazo ni pamoja na hili suala la matokeo mabaya ya kidato cha
nne na hatua ambazo Serikali imezichukua hadi sasa,” alisema Mnyika.
Alifafanua kuwa Kamati Kuu ya Chadema,
haijakubaliana na hatua ya Serikali ya kuunda tume nyingine ya
kuchunguza chanzo cha matokeo
hayo na kushindwa kumwajibisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa.
Alisema chama hicho kinatambua kwamba kumeshawahi
kuundwa kamati nyingi ikiwamo ile ya mwaka 2010 na nyingine mwaka 2011
ambazo hadi leo, Serikali haijawahi kutoa ripoti ya matokeo ya uchunguzi
kwa wananchi.
“Kamati imewataka wabunge kutumia nafasi ya Bunge
la Bajeti, kuwasilisha hoja za kumtaka Waziri Mkuu kuzitoa ripoti hizo,
kupitia Kambi ya Upinzania Bungeni inayoongozwa na Chadema,
tutahakikisha kuwa tunafanikisha lengo letu kwa kuzingatia kanuni za
Bunge,” alisema.
Viongozi wa Chadema kwa nyakati tofauti
walitangaza kufanyika kwa maandamano yaliyolenga kumshinikisha Dk
Kawambwa na Naibu wake Philipp Mulugo, kujiuzulu kutokana na matokeo
mabaya mitihani ya kidato cha nne mwaka jana.
Hata hivyo, polisi walizuia kufanyika kwa
maandamano hayo kwa maelezo kuwa tayari Serikali imeunda tume
inayoongozwa na Profesa Sifuni Mchome, kushughulikia suala hilo.
Mnyika alisema baada ya kuwasilisha hoja hizo bungeni na hatua
zinazostahili hazitachukuliwa, watalazimika kuandaa maandamano ili
kushinikiza uwajibikaji wa viongozi hao.
Aidha, Mnyika alitumia fursa hiyo kuipongeza CCM
kwa kukiri kuwa ndiyo wamiliki wa Kampuni ya Jitegemee, ambayo alidai
kwamba inatumika kwa ufisadi.
Chama hicho kimedai kuwa zipo nyaraka za Serikali
zinazothibitisha madai namna Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA) ilivyowekeana mikataba ya maegesho na kampuni hiyo.
Chadema pia imemtuhumu Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe, kuwa ametoa zabuni ya ujenzi wa bandari ya nchi kavu
kwa kampuni hiyo ya Jitegemee kinyume cha sheria za ununuzi.
0 comments:
Post a Comment