Zanzibar. Mtuhumiwa wa mauaji ya Padri Evaristus
Mushi, Omar Mussa Makame (35) mkazi wa Mwanakwerekwe mjini hapa
amefikishwa Mahakama Kuu kwa tuhuma za mauaji ya kiongozi huyo wa dini.
Makame aliyegombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi
kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Rahaleo mwaka 2010
alifikishwa mbele ya Jaji Mkusa Sepetu jana.
Awali mtuhumiwa huyo alikuwa afikishwe mahakamani
Jumanne iliyopita, lakini ilishindikana baada ya ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashitaka (DPP) Zanzibar kuinyima kibali Polisi kumfikisha mahakamani.
Haikujulikana sababu ya uamuzi huo kwani
Mkurugenzi wa Mashtaka, Ibrahim Mzee Ibrahim na Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa walitupiana mpira kila mmoja akitaka mwenzake
ndiye ataje sababu hizo.
Viongozi hao wote jana hawakupatikana kueleza
hatua hii mpya ya kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo imekuja baada ya
uamuzi wa aina gani.
Wakili wa Serikali, Abdallah Issa Mgongo alidai
mbele ya Jaji Sepetu kuwa mshtakiwa aliua kwa makusudi Februari 17,
mwaka huu eneo la Beit el Rass Wilaya ya Magharibi Zanzibar.
Mgongo alidai tendo hilo ni kosa kwa mujibu wa vifungu 196 na 197 sheria namba (6) za mwaka 2004 ya sheria za Zanzibar.
“Omar Mussa Makame unashitakiwa kwa kosa la kumuua
kwa makusudi Padre Evarist Mushi siku ya tarehe 17/02/2013 mnamo saa
12:50 za asubuhi,” alidai Wakili Mgongo.
Makame alikataa kosa hilo la mauaji na wakili wa
Serikali aliiomba Mahakama kumrudisha rumande mtuhumiwa hadi hapo
ushahidi utakapokamilika.
Upande wa utetezi wakili wa kujitegemea, Abdallah
Juma aliiomba Mahakama iamuru ushahidi ukamilike baada ya wiki mbili ili
kesi iweze kusikilizwa.
“Kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa
ni kwamba ushahidi umekamilika nashangaa leo (jana) wakili wa Serikali
anasema kwamba bado haujakamilika,” alidai Juma.
Baada ya maombi hayo, Jaji Sepetu alikubaliana na
upande wa utetezi na kuwataka mawakili wa Serikali kuharakisha kupeleka
ushahidi ili kesi ianze kusikilizwa. Kesi hiyo imepangwa Aprili 18,
mwaka huu katika mahakama hiyo.
Mapema Wakili wa upande wa utetezi, Abdallah Juma aliomba
mahakama kuanza kusikilizwa ombi lao ambalo walilipeleka Machi 28, mwaka
huu ambalo lilitaka kujua kwa nini mteja wao amewekwa ndani kipindi
kirefu bila kupelekwa mahakamani.
“Mheshimiwa Jaji kwa heshima yako naomba kwanza
tungesikiliza ombi letu halafu tukaja kwenye kesi kwani naona moja
inaweza kuharibu nyingine,” alidai Wakili Juma.
Baada ya maombi hayo, Jaji Sepetu alisema hivyo ni vitu viwili tofauti na mahakama haiwezi kukubaliana na maombi hayo.
Jumatano Mahakama Kuu Zanzibar iliamuru kuletwa
mahakamani kwa mtuhumiwa wa mauaji ya Padri Evaristus Mushi, Jumatatu
ili kuweza kusikiliza shauri lililofunguliwa na mawakili wa upande wa
mlalamikiwa la kutokufikishwa mahakamani kwa mteja wao, Makame.
Kampuni ya Uwakili ya AJM Solicitors and Advocate
iliwasilisha Mahakama Kuu ya Zanzibar maombi ya Habeas Corpus chini ya
kifungu cha 390 cha Sheria ya Makosa ya Jinai sura ya 7 ya mwaka 2007
inayomtaka mtu anayemshikilia mtu mwingine au chombo chochote bila
kumfikisha mahakamani kwa saa 24 aieleze mahakama sababu za kumshikilia
mtu bila kumfikisha mahakamani au amwachie huru.
Ombi hilo lilikuwa kwa Jaji Mkusa ambaye jana alisikiliza kesi ya kufikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa huyo.
Padre Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi Februari
17, mwaka huu wakati akienda kuongoza ibada ya Jumapili katika Kanisa la
Mtakatifu Teresia lililopo Beit el Raas nje kidogo ya mjini hapa.
mwananchi
mwananchi
0 comments:
Post a Comment