Adaiwa kuipa CCM zabuni ya kupanua bandari
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtuhumu Waziri
wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kuwa amefanya yale aliyoyakataa
kwenye Kampuni ya Richmond, licha ya wakati huo kujidai anajua kufuata
taratibu.
CHADEMA imefichua kuwa Dk. Mwakyembe amekiuka sheria ya manunuzi ya
umma katika mradi wa upanuzi wa bandari kavu unaofanyika katika eneo la
Sukita, Tabata jijini Dar es Salaam.
Siri hiyo ilifichuliwa na Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa
CHADEMA, Benson Kigaila alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam kabla ya kuanza kwa vikao vya Kamati Kuu ya
chama hicho.
Kigaila alidai kuwa Dk. Mwakyembe ni mnafiki, kwani yale aliyoyakataa
wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati teule ya Richmond ambapo ripoti yake
ilisababisha Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa ajiuzulu, leo
ameyafanya.
“Alilaumu kuwa Richmond ilipewa zabuni bila kuwa na vigezo, bila
kufanyiwa upembuzi yakinifu, tena bila zabuni husika kutangazwa.
Hili ni eneo la SUKITA linamilikiwa na CCM na lipo maeneo ya barabara ya Kawawa na Mandela,” alisema.
Alisema mradi huu utatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya CCM
inayoitwa Jitegemee Trading Company na TPA kwa gharama ya mabilioni ya
shilingi.
Kigaila alidai kuwa katika mwaka ujao wa fedha 2013/2014 Mamlaka ya
Bandari (TPA) itailipa CCM sh bilioni 10 na kwamba tayari fedha hizo
zimetengwa katika bajeti ya serikali.
Kampuni ya SUKITA ilisajiliwa Machi 15, 1978 na Jitegemee Trading Company Limited ilisajiliwa mwaka 1997.
Wakurugenzi wa Jitegemee ni Sam Mapande, Peter Machunde na Diwani wa
CCM Kata ya Hananasif, wilayani Kinondoni, Abbas Tarimba. Mapande, ndiye
mwanasheria aliyehakiki fomu za Jakaya Kikwete katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010.
“Kwanza mradi huu unaotaka kufanywa na Mwakyembe kwa kutumia kivuli
cha TPA haukufanyiwa tathimini, upembuzi yakinifu kiuchumi sawa sawa na
ilivyokuwa kwa kampuni ya kitapeli ya Richmond,” alisema Kigaila.
Aliongeza kuwa mradi huu haukufanyiwa uchanganuzi wa kiuchumi ili
kubaini pamoja na kulipa sh bilioni 10 ya plot kabla ya kujengwa kwa
mradi.
“Mradi huu wa Mwakyembe na chama chake haukufuata sheria ya manunuzi
ya umma (PPRA). Hakukuwa na zabuni iliyotangazwa wala ushindani kwa
makampuni na mashirika mengine yenye sifa,” alisisitiza.
Kigaila aliongeza kuwa nyaraka zilizopo TPA zinaonyesha kuwa tangu
mwaka 2010, Bodi ya Bandari ilipokea maombi kutoka Manispaa ya Temeke ya
kutaka kufanya ubia wa eneo la maegesho, ambapo walitenga eneo huko
Kurasini, karibu kabisa na bandari.
Alisema kuwa wazo hilo halijafanyiwa kazi, badala yake Mwakyembe amekuja na mradi wake.
Kigaila alisema vyanzo vyao ndani ya serikali na CCM vinasema mjumbe
mmoja wa Bodi ya TPA alihoji kwanini shirika linaingiza fedha hizo
kwenye mradi huu katika eneo la SUKITA, lakini mkurugenzi wa bandari
alijibu: “Huu ni mradi wa chama tawala, hivyo ni muhimu tukau-sapport”.
Alihoji kama Mwakyembe, serikali na CCM hawaoni umuhimu wa kutumia
fedha hizo kuimarisha bandari zilizopo kwenye maeneo ya maziwa kama vile
Kigoma, Mwanza, Rukwa na Musoma ikiwa ni kujiweka sawa kwenye ukanda wa
biashara na ukuaji wa soko la Afrika Mashariki.
Alisema kuwa siku zote CCM na serikali yake wamekuwa wakijifanya
kuwaonea huruma Watanzania na kuwataka wahame mabondeni, lakini hao hao
wanatumia mabilioni ya shilingi na kuyaingiza katika bonde la Msimbazi,
ambako kuna hatari kubwa ya mvua kusomba magari na makontena ya wateja
wa TPA.
“Lakini ukiangalia hii ripoti, utaona kuwa kuna miradi mikubwa 35
ambayo imeombewa fedha si kwa sababu ya kuiendeleza, bali ni kukusanya
fedha za kutafuta urais,” alidai.
Kigaila aliongeza kuwa Mwakyembe amekataa mapendekezo yaliyokuwa
yamefanywa na uongozi wa bandari kushirikiana na Manispaa ya Temeke
kupanua bandari eneo la Kurasini, badala yake ameelekeza upanuzi huo
ufanyike katika eneo la SUKITA.
“Kampuni ni ya CCM, kiwanja ni cha CCM, zabuni haikutangazwa wala
kufanya upembuzi yakinifu kwa kampuni hii kama imekidhi vigezo.
Mwakyembe atuambie ilishindanishwa na kampuni zipi na ilishinda kwa
vigezo vipi. Iweje yale aliyoyakataa kwenye Richmond ameyatenda?”
alihoji.
Kigaila amelaani tabia ya viongozi wa CCM kuanzisha miradi au kampuni
hewa wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu kwani ni kwa njia hii huchota
fedha kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi kama ilivyofanyika kwa EPA.
“Mwakyembe yupo kwenye kambi ya Samuel Sitta, wanaungana na familia ya
Jakaya Kikwete kumsaidia Bernard Membe katika kinyang’anyiro cha
uchaguzi mkuu ujao, hivyo wameamua kuanzisha miradi hii kwa njia za
kifisadi,” alisema.
Juhudi za Tanzania Daima kuzungumza na Mwakyembe au Naibu wake,
CharlesTizeba na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye
ziligonga mwamba baada ya wote kutotoa ushirikiano.
Waziri Mwakyembe simu yake iliita bila kupokelewa na hata
alipoandikiwa ujumbe mfupi (sms) hakupatikana tena hewani wakati naibu
wake, alisema: “Wewe gazeti lenu liliandika nilifukuzwa Mtwara, na sasa
unataka kunigonganisha na propaganda za CHADEMA ili upate habari ya
kuandika, sitaki gazeti lako na sikutaki wewe.”
Naye Nape alisema: “Andikeni mnavyoandika mimi nitajibu kesho kwa kuwa najua nikijibu sasa mtayaweka ndani kwa udogo.”
Alipoulizwa kwanini asitumie hiyo nafasi kujibu, alimwambia mwandishi:
“Kama hutaki kusikia yangu, basi andika ya kwako, mimi nimesema
nitajibu kesho.”
MTANZANIA
|
|
0 comments:
Post a Comment