Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametoa siku 30 kwa mmiliki
wa jengo la ghorofa 16, lililopo Mtaa wa Indira Gandhi katikati ya jiji,
Ally Raza kulibomoa jengo hilo baada ya kubainika alilijenga chini ya
kiwango.
Kadhalika Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira
imeiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, kufanya uchunguzi wa ubora
wa majengo mengine matano yanayomilikiwa na Raza ambaye pia ni mmiliki
wa jengo lingine la ghoroga 16 lililoporomoka wiki iliyopita jijini Dar
es Salaam kama yako katika viwango vinavyokidhi.
Jengo hilo lililoporomoka lilisababisha vifo vya watu 36, majeruhi 17 na uharibifu wa mali ikiwamo magari linamilikiwa na Raza.
Jengo hilo lilikuwa likijengwa na Kampuni ya Lucky
Construction Limited ambayo ni mali ya Diwani wa Kata ya Goba (CCM)
Wilaya ya Kinondoni, Ibrahim Kisoki ambaye pia alijenga jengo jingine
jirani na la awali, imetolewa amri ya kufanyika kwa utafiti kubaini kama
limekidhi viwango.
Profesa Tibaijuka akizungumza mbele ya Kamati hiyo
walipofanya ziara katika jengo hilo jana, alisema uchunguzi wa awali wa
kuporomoka kwa jengo hilo umebaini kuwa jengo lililoko mkabala, pia
lilijengwa chini ya viwango.
“Ninaagiza jengo hilo kuwa libomolewe ndani ya
siku 30 kwa gharama za mmiliki na akikaidi atalipishwa faini ya asilimia
mbili ya gharama ya kuendeleza pasipokuwa na kibali kwa kila siku hadi
atakapotekeleza agizo hilo,” alisema Profesa Tibaijuka na kuongeza;
“Makazi haya yanatakiwa kujengwa majengo
yasiyozidi ghorofa 10, lakini katika hili ghorofa ambalo linatakiwa
kubomolewa kwanza kiutaalamu halikuzingatia vigezo kutokana na kujengwa
kwenye kiwanja chenye mita 150 ambacho ni kidogo.”
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli
alisema kuna taarifa kwamba mmiliki wa jengo anamiliki majengo mengine
ambayo hivi sasa yanakaliwa na watu pia yamezua hofu, hivyo yanatakiwa
kufanyiwa uchunguzi.
“Kutokana na majengo yake mawili ambayo
tayari yameleta utata kwa kuonekana kujengwa chini ya viwango, hivyo
tunataka majengo mengine anayomiliki, Manispaa ya Ilala iyafanyie
uchunguzi mapema ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea,” alisema
Lembeli.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
Mazingira, Dk Terezya Huvisa amewataka watu wanaotaka kujenga majengo
yenye zaidi ya ghorofa sita kufika ofisini kwake kupata vibali vya
ujenzi.
“Mtu yeyote anayetaka kujenga jengo zaidi ya
ghorofa sita anatakiwa kuomba kibali wizarani na wao kupitia Baraza la
Taifa la Mazingira (NEMC) watatoa kibali cha kujengwa au kutojengwa
kutokana na uchunguzi wa sehemu husika,” alisema Dk Huvisa
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment