Dar es Salaam. Serikali imesema inazo
taarifa za kuwapo wageni wanaotafuta ardhi nchini, kwa kutumia mbinu ya
kuoa au kuolewa na Watanzania.
Hayo yalibainishwa juzi na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, wakati akitoa salamu kwenye tamasha la Pasaka, lililofanyika
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Siku hizi kuna mbinu inayotumiwa na wageni kwamba
ukitaka kupata ardhi nchini kwa urahisi, basi uoe Mtanzania au uoelewe
na Mtanzania. Hili hatutalikubali kamwe,” alisema Pinda.
Pinda alikuwa akijibu tahadhari iliyotolewa na
waandaaji wa tamasha hilo, Msama Promotions, kuhusu ugawaji ardhi kwa
watu wasio Watanzania, kutokana na mkataba wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC).
Akitoa tahadhari hiyo, Onesmo Ndegi
alitahadharisha Serikali kuwa makini na suala la ardhi katika jumuiya,
kwa sababu kuna raia wa nje wamekuwa wakijipenyeza na kupata ardhi
nchini.
“Tunaomba ardhi itazamwe kwa jicho la ziada. Watu
wanajipenyeza kinyemela wakiinyemelea ardhi yetu, tunaomba mtulindie
ardhi,” alisema Ndegi.
Pia, Ndegi alishauri Serikali ipambane na kile
alichokiita kikundi cha watu wachache, wanaotaka kuvuruga amani chini ya
mwamvuli wa kidini kinachojipanga kwa kazi maalumu.
“Serikali imaanishe kupambana na watu hawa, nasi tuone matokeo na tutaiponegeza. Viongozi wa dini tunawaombea,” alisema Ndegi.
Hata hivyo, Pinda alisema Serikali ina macho ya
ziada kwa suala la ardhi na kwamba, hakuna mgeni anayeweza kupewa ardhi
kwa njia za ujanjaujanja isipokuwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment