Shrikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezindua rasmi Mpango wa Maendeleo
wa Mpira wa Miguu (Technical Development Plan- TDP) wa 2013-2016 ambao
pamoja na mambo mengine unahusisha kutazama upya mfumo wa mashindano na
kuunda kanda kwa ajili ya kusimamia maendeleo.
Uzinduzi
huo umefanywa leo (Aprili 4 mwaka huu) na Rais wa TFF, Leodegar Tenga
katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa
na washirika mbalimbali wakiwemo wachezaji, viongozi wa mpira wa miguu,
Serikali, klabu na Wahariri wa Michezo.
Rais
Tenga amesema mpango huo unafuatia ule wa 2004-2007, na 2008-2012
ambayo ilitengenezwa kwa msaada wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA). Mpango wa sasa umetengenezwa na TFF kwa kufuata mpango
mfano (standard plan) wa FIFA.
Amesema
mpango wa sasa ni wa kiufundi zaidi kwa vile umelenga kuendeleza mpira
wa miguu, kwani iliyotangulia ilihusisha zaidi kutengeneza muundo wa
TFF, kazi ambayo imekamilika kwani sasa shirikisho lina vyombo
mbalimbali vya kusimamia mchezo huo.
“Wakati
ule tulikuwa na Ligi Kuu tu, lakini tumeongeza mashindano ya aina
mbalimbali kama U17, U20, Kombe la Taifa na sasa michuano ya Copa
Coca-Cola itakuwa ya U15. Pia tukatengeneza Kanuni za Fedha, kilichomo
katika mpango wa sasa ni kujenga mpira. Chombo (TFF) tayari kipo,”
amesema.
Rais
Tenga amesema TFF imefika hapa kutokana na watu kujitolea ambapo
ametaka moyo huo uendelezwe, lakini akasisitiza washirika wote kuwa na
mpango huo na kuusoma kwani umetokana na maoni yao ambapo kila mmoja ana
kazi ya kufanya katika mpango huo.
“Naomba
washirika wote wasome mpango huu. Kama mtu una mawazo zaidi baada ya
kusoma, toa maoni yako. Mpango huu si Msahafu, utabadilika kutokana na
maoni ya watu. Kama una mawazo zaidi, toa maoni yako kwa lengo la
kujenga, isiwe kazi ya kulaumu tu kuwa mpango una upungufu. Mabadiliko
yanafanyika kutokana na mawazo mapya,” amesema.
Amesema
maendeleo ya mpira wa miguu ni mchakato mrefu, kwa hiyo unahitaji
ushiriki wa watu kutokana na ukweli kuwa uongozi wa mpira wa miguu
Tanzania bado ni wa kujitolea.
Rais
Tenga amesema ahadi ya TFF ni kushirikiana na washirika mbalimbali
kuhakikisha kuna maendeleo kwa faida ya mpira wa miguu wenyewe na nchi
kwa ujumla.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment