Na Nuzulack Dausen na Deborah Ngajilo.
Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji
nchini imewakamata watu watatu wanaotuhumiwa kujihusisha na utengenezaji
wa vibali bandia vya ukazi kwa wageni wanaishi nchini.
Watu hao walikamatwa hivi karibuni wakiwa na
vibali bandia 14 vya ukazi vya daraja B ambavyo kama vingekuwa halali,
thamani yake ingekuwa Sh46 milioni.
Watu hao pia walikamatwa na vifaa vinavyotumika katika kughushi vyeti na nyaraka mbalimbali.
Hali kadhalika, mihuri bandia 56 ya taasisi mbalimbali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Kaimu Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Mbaraka Bajenga alisema
jitihada za kuwakamata watu hao zilianza baada ya kugundua kuwepo kwa
vibali vingi bandia vinavyomilikiwa na raia wa kigeni, bila wao wenyewe
kujua.
Alisema Machi 19, mwaka huu, idara ilifanikiwa
kumkamata mtuhumiwa mmoja ambaye baadaye alisaidia kukamatwa kwa
watuhumiwa wengine wawili.
“Watua hawa ni hatari sana, tumewakamata wakiwa na
vibali bandia 14 vya ukazi daraja B, stika za bima kwa ajili ya magari,
vyeti vya kifo, uzazi na ndoa, stakabadhi za malipo ya Serikali na
mihuri 56 na nyaraka nyingine nyingi,” alisema Bajenga.
Alisema mihuri bandia iliyokamatwa kuwa ni mmoja
wa Idara ya Uhamiaji, saba ya TRA, saba mingine ya Benki ya CRDB, minne
ya Benki ya NBC na muhuri mmoja wenye nembo ya Taifa.
Mingine ni muhuri mmoja wa mkurugenzi wa
biashara za ndani, mmoja wa msajili msaidizi wa ndoa, mitatu ya Manispaa
ya Ilala na mitatu ya Manispaa ya Temeke, minne ya Manispaa ya
Kinondoni na mmoja wa Benki ya Exim.
Bajenga aliwataka raia pamoja na wageni wote nchini kufanya uhakiki wa vibali vya ukazi ili kuepukana na adha.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment