Hakika; Baada ya dhiki faraja” Msemo huu wa
Waswahili sasa una maana kubwa kwa Menas Mbunda Andoya, mzalendo wa
Tanzania aliyebuni mradi wa umeme wa maporomoko ya maji takriban miaka
13 iliyopita.
Wazo la Mtanzania huyo kuanzisha mradi huo
lilimfanya akumbane na vikwazo mbalimbali ikiwamo kufukuzwa kama kuku na
watu katika ofisi zao huku akipigwa vita kila kona.
Hata hivyo, Andoya ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Kampuni ya Andoya Hydro Electric Power Co. Ltd (AHEPO), hakuchoka wala
kukata tamaa, bali aliendelea kuwa jasiri, hatimaye mradi wake mkubwa wa
umeme wa maporomoko ya maji alioubuni mwaka 2000 umezaa matunda, badaa
ya kufanikiwa kuwasha umeme kwa majaribio.
Ukibahatika kuonana naye Andoya(56),
anavyofahamika na wengi ambaye ni mzaliwa wa Wilaya ya Mbinga, mkoani
Ruvuma akiwa ni mtoto wa tatu kati ya saba, akiwa pia mume na baba wa
watoto watatu wa kiume. Kitabia ni mcheshi, mwenye busara na mtu
anayejiamini.
Kwa maelezo yake anasema kuwa alikuwa na hamu
kubwa kuona anafanikiwa kuhakikisha siku moja anatimiza ndoto yake na
Watanzania wenzake wanapata huduma ya umeme na kufa akiwa na faraja la
kutimiza lengo hilo.
Anasema kuwa madhumuni ya mradi huo ni kuzalisha
umeme MW 1 na kuunganishwa kwa wateja wa awali 922 kati ya 3,835 katika
Vijiji vya Lifakara, Kilimani na Mbangamao na ziada kuuzwa Tanesco
ukilenga kupata umeme kwa njia endelevu na nafuu.
Andoya anasema kuwa tayari ujenzi wa njia za
kusafirisha umeme kutoka Mbinga hadi Kituo cha Uzalishaji na usambazaji
katika Vijiji vya Lifakara, Kilimani na Mbangamao umekamilka.
Anaeleza kuwa maandalizi wa ujenzi wa bwawa,
mfereji wa maji na nyumba ya mashine yamekamilika na ujenzi utaanza
kipindi kifupi kijacho.
Anadokeza kuwa awali madhumuni yake yalikuwa
kutumia nguvu ya maji kuendesha mashine za kukoboa na kusaga nafaka ili
kupunguza gharama kwa wananchi wa vijiji vya jirani kwa kutoa huduma
hiyo kwa bei nafuu na kuinua maisha yao, ambapo mradi huo ulianza kwa
jina la Nguvu ya Maji Partinership.
Anabainisha kuwa mwaka 2005 Kampuni ya Andoya
Hydroelectric Power Co Ltd ilisajiliwa na upembuzi yakinifu wa mradi
ulikamilika, hatimaye taarifa ya upembuzi yakinifu na mchanganuo wa
mradi ulipitiwa na wataalamu mbalimbali wa taasisi za Serikali ikiwamo
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
NEMC, Ewera na wataalamu kutoka Benki ya Dunia na wote kuafiki kuwa
kiasi cha MW 1 kinaweza kupatika katika maporomoko hayo ya Mto Mtandasi.
Andoya anasema kuwa kufikia Novemba 2012, mradi
huo ulifanikiwa kupata vibali na fedha za kutekeleza, ukiwa katika hatua
mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa njia ya usafirishaji wa umeme yenye
urefu wa kilomita 14 kwa kiwango HT kutoka Kituo cha Umeme cha Mbangamao
hadi Makao Mkuu ya Wilaya, ili kuunganisha na gridi ya Tanesco pamoja
na Vijiji vya Lifakara (2 km), Kilimani (4 km) na Mbangamao (4 km).
Anaitaja awamu ya pili kuwa ni ujenzi wa njia za
kusambaza umeme kwa wateja. Andoya anafafanua kuwa gharama za ujenzi wa
mradi huo ni Sh 4.5 bilioni, ambapo asilimia 30 zilichangwa kutoka mtaji
wa Kampuni ya Andoya Hydro Electric Power Co. Ltd (AHEPO), asilimia 70
ni mkopo kutoka Benki ya CRDB, mkopo wa benki ya Dunia kupitia Serikali
na taasisi zake ikiwamo (REA) chini ya mpango wa Tanzania Energy
Development and Access Project (TEDAP), ambapo pia Unido wameahidi
kuchangia Dola 250,000 za Marekani.
Anasema kuwa Kampuni ya AHEPO imeshapanda miti ya asili 101,920
kwenye eneo la mradi, pamoja na miti ya matunda na kuanzisha shamba la
miti la mfano lenye miti 85,920 kama shamba darasa, huku kando ya
barabara ya urefu wa km 1.5 kuelekea eneo la mradi kukipandwa miti ya
miembe.
Akieleza matarajio ya mradi anasema “Unatarajia
kukamilika Julai, 2014 kwa kufunga mashine moja ya KW 500, ambapo kwa
kushirikiana na halmashauri ya Mbinga tunatarajia kukuza ulimaji wa
Alizeti, kuunda vikundi vya kinamama na kampuni itatoa nyumba na ufundi
wa ufungaji mashine za kukamua mafuta ya alizeti.”
“Kwa kushirikiana na shirika la mapadri wa Vicent
tunatarajia kuanziasha kituo cha mawasiliano makao makuu ya kata -
Mbangamao. Mazungumzo na Shirika la mapadri wa Vicent yamekamilika
ambapo watachangia kompyuta na ufundishaji. Kituo hicho kitawawesha
wananchi wote kupata habari, mafunzo ya kutumia kompyuta kwa
mawasiliano,” alisema Andoya.
Andoya anaongeza kuwa kampuni yake inatarajia
kufanya upembuzi yakinifu katika maeneo ya Kingirikiti na Makulukulu
katika Mto Lumeme, Wilaya Mpya ya Nyasa, ambako mashine za kusaga na
kukoboa kwa nguvu ya maji zimefungwa, ili kuzalisha umeme, pia
kuhamasisha na kuelimisha wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji na
mazingira.
Faida za mradi
Mjasiriamali huyo anaweka wazi kuwa mradi
utakapokamilika utaokoa zaidi ya Sh560 milioni kwa mwaka, ambazo
zingetumika kununulia mafuta kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme ikiwa
pamoja na wananchi kupata fursa za kujiajiri kwa kuanzisha shughuli
mbalimbali za kuongeza kipato kwa kufungua viwanda vidogovidogo,
kuongeza thamani ya mazao yao kwa kusindika na kufungua biashara
mbalimbali.
Anaongeza kuwa mradi huo wa umeme pia utawezesha
utoaji wa huduma za afya na elimu kuwa bora zaidi kwa kutumia vifaa
vinavyotumia umeme, ikiwa pamoja na maabara katika zahanati na
sekondari, pia kuwezesha matumizi ya kompyuta mashuleni.
Aidha, mradi huo utaongeza mapato ya wananchi wa
vijiji husika kutokana na kuokoa fedha zilizokuwa zikitumika kununua
mafuta, betri na kuni kwa ajili ya kumulikia na kupikia.
Anazitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni
kampuni yake kushindwa kujenga njia ya kusafirisha umeme kufika maeneo
mawili muhimu kwa kukosa uwezo wa kifedha. Maeneo hayo ni pamoja na
Gereza Kuu la Wilaya la Mkwaya na kijiji chake Km 9.5 ambapo kuna nyumba
za watumishi 60, wakazi 1,200, pia Kiwanda cha Kumenya Kahawa Mbichi,
mashine za kusaga na kukoboa, zahanati, shule ya msingi na sekondari.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye
mradi huo katika Kijiji cha Lifakara, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema
hatua hiyo ni nzuri na inaleta matumaini kwa taifa, hivyo ni vyema
wananchi wamuunge mkono kwa kushirikiana naye kwa karibu pindi mradi
utakapoanza kwani watapata faida kubwa na utasaidia Wilaya ya Mbinga.
Anasema mwaka 2008 Serikali ilipitisha sheria ya
kuruhusu mtu yeyote mwenye uwezo wa kubuni na kuanzisha mradi wa umeme
wa jua, maji au upepo na kusambaza kwa wateja kwa kuusafirisha kwenda
mahali popote baada ya kutimiza masharti na kanuni zilizowekwa na wizara
ya nishati.
“Nimefarijika sana kuona Tanzania imepata
mwekezaji mzalendo ambaye ataweza kuwasaidia Watanzania wenzake kupata
umeme wa uhakika kwa kutumia maporomoko ya maji,”alisema PindaNaye Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stevin Masele anasema mradi huo
umeendeshwa kwa mujibu wa kanuni, sheria za nishati na unatambuliwa na
wizara, REA pamoja na Tanesco na kwamba wanaendelea kushauriana na
Andoya namna bora ya kuendesha mradi huo
0 comments:
Post a Comment