pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Aliye muua Dkt Mvungi apandishwa kizimbani

Dar es Salaam. Mshtakiwa George Mulungu (28) mkazi wa Vingunguti amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka la kumuua kwa kukusudia aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi.
Mulungu alisomewa shtaka la mauaji ya kukusudia juzi na Wakili wa Serikali, Charles Anindo ambaye pia alimwomba Hakimu Mkazi, Geni Dudu kuwa mshtakiwa huyo Januari 30, 2014, aunganishwe na wenzake 10 wanaokabiliwa na kesi hiyo.
Hakimu Dudu alikubaliana na ombi hilo na kuiahirisha kesi hiyo hadi Januari 30, 2014 ambapo mshtakiwa huyo ataunganishwa na wenzake Chibago Magozi (32) mfanyabiashara na mkazi wa Vingunguti Machinjioni, John Mayunga (56) mfanyabiashara na mkazi wa Kiwalani na Juma Kangungu (29) mkazi wa Vingunguti.
Wengine ni aliyekuwa mlinzi wa marehemu Dk Mvungi, Longishu Losingo (29) na Masunga Makenza (40) dereva na mkazi wa Kitunda, Paulo Mdonondo (30) Mkazi wa Tabata Darajani, Mianda Mlewa (40) mkazi wa Vingunguti, Zacharia Msese (33) mkazi wa Buguruni, Msungwa Matonya (30) mkazi wa Vingunguti na Ahmad Kitabu (30) mkazi wa Mwananyamala wilayani Kinondoni na kufanya idadi ya washtakiwa hao kufikia 11.
Awali akiwasomea hati ya mashtaka washtakiwa hao, Wakili wa Serikali, Aida Kisumo alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja Novemba 3, mwaka 2013, walifanya kosa hilo la mauaji ya kukusudia kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria na Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kisumo alidai kuwa siku ya tukio, katika eneo la Msakuzi Kiswegere lililopo eneo la Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua kwa kukusudia Dk Sengondo Mvungi ambaye ni Mjumbe wa Tume ya Katiba Mpya.

0 comments:

Post a Comment