WANACHAMA
wa klabu ya Yanga wameuomba uongozi wao wamchangie kulipa deni
mshambuliaji wao, Mrisho Ngasa, baada ya kukopa katika moja ya benki
hapa nchini kuwalipa Simba.
Ngasa alikopa sh milioni 45 katika moja ya benki ambayo haikutajwa
jina, kwa ajili ya kulipa deni la Simba, baada ya kugundulika kumwaga
wino sehemu mbili na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumfungia mechi sita na kutakiwa
kulipa fedha hizo.
Akizungumza katika mkutano wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika
ukumbi wa PTA Sabasaba jijini Dar es Salaam juzi, mmoja wa wanachama
kutoka Tawi la Makumbusho, alitoa hoja hiyo kwa uongozi ili litembezwe
bakuli kumchangia nyota huyo.
“Jamani ni fedheha kwa klabu kubwa kama Yanga kuona wachezaji wetu
wanaadhirika, maana Ngasa mpaka sasa anadaiwa fedha na benki, hivyo basi
naomba viongozi mpitishe mchango kwa wanachama ili tumchangie deni
hilo,” alisema mwanachama huyo.
Baada ya kauli hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga,
alisema mwanachama yeyote mwenye nia ya kumchangia Ngasa, aende Ofisi za
Katibu Mkuu wa Yanga ili aweze kutoa mchango wake.
“Tunahitaji wanachama wenye hekima na moyo wa kujitolea kama wewe,
ukitaka kumchangia nenda ofisi ya katibu peleka mchango wako,” alisema
Sanga.
Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga kinatarajiwa kurejea nchini
kesho kutoka Uturuki walikokuwa wameweka kambi ya wiki mbili.
credit, Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment