pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Sababu za kumg'oa Meya Bukoba hizi hapa...!

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory AmaniHATIMAYE ukweli umedhihirika. Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Ludovick Utouh imethibitisha habari zilizoripotiwa na gazeti hili tangu Mei 2012, kuhusu miradi ya kifisadi iliyokuwa ikitekelezwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.
Kufuatia ripoti hiyo, Meya Amani amekubali kutekeleza agizo la serikali la kujiuzulu wadhifa wake, huku aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Hamis Kaputa, Mhandisi Steven Nzihirwa na Mhasibu wa Halmashauri, Hamdun Ulomy wakivuliwa madaraka yao.
Akiwasilisha ripoti yake jana mbele ya madiwani mjini Bukoba, Utouh alisema kuwa ukaguzi umebaini miradi ilitekelezwa kinyume cha taratibu bila Baraza la Madiwani na Wizara ya Tamisemi kushirikishwa.
Kwa hatua hiyo, mgogoro uliodumu zaidi ya mwaka mmoja kati ya Meya Amani na baadhi ya madiwani wake, akiwemo Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki utakuwa umefikia ukomo.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupitia viongozi wake wa wilaya na mkoa wakiwemo madiwani, ndio waasisi wa hoja hiyo kwenye mikutano ya hadhara na vikao vya baraza.
Baadaye waliungwa mkono na CUF huku wenzao wa CCM wakiwabeza, lakini hatimaye Kagasheki alitambua hoja yao na kuwashawishi wenzake kusimamia tuhuma hizo.
CCM kupitia viongozi wake wakuu wa kitaifa, akiwemo Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, walijaribu kuingilia kati kuwashawishi madiwani wao wajiondoe kwenye tuhuma dhidi ya meya huyo, lakini ilishindikana.
Katika kutanzua mgogoro huo baada ya hali kuwa mbaya pale uongozi wa chama mkoa kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa, Fabian Massawe walipowavua uanachama madiwani hao, Kamati Kuu ya Taifa iliomba serikali imuagize CAG akague miradi hiyo.
Oktoba 30, 2013, CAG na timu yake walianza ukaguzi wa miradi hiyo katika maeneo mbalimbali, kazi ambayo waliikamilisha na hatimaye kutoa ripoti yao jana.
Katika kile kilichoonekana kama jaribio la mkuu wa mkoa kutaka kumnasua meya, mapema wiki hii aliitisha kikao na madiwani wanaompinga Amani mbele ya viongozi wa dini na wazee akidai anataka wasuluhishwe.
Hata hivyo, mkakati huo ulipingwa na madiwani hao, huku CCM ikimshtaki Massawe kwa Rais Kikwete akidaiwa kuwa chanzo cha mgogoro huo kutokana na maslahi binafsi.
CAG katika ripoti yake kuhusu uwekezaji wenye shaka kwenye kituo cha kuosha magari, alisema zabuni haikuwa shindanishi na kwamba ilikuwa kinyume cha taratibu.
Alisema kuwa waliosaini mkataba huo ni Kaputa aliyekuwa mkurugenzi kabla ya kuhamishiwa mkoani Mbeya na Amani huku wakijua ilikuwa ni makosa kufanya hivyo bila idhini ya kikao cha madiwani.
Utouh alifafanua kuwa Kampuni husika ya ASEC iliyofanya kazi hiyo haijasajiliwa na Msajili wa makampuni (Brela) na hailipi kodi TRA.
Kuhusu tuhuma za upimaji na ugawaji wa viwanja, ripoti ilibaini kuwa kati ya wananchi 800 waliotakiwa kugawiwa viwanja, 300 tu ndio waliogawawia kutokana na migogoro ya viwanja kimila.
“Manispaa ilingia makubaliano na Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) kupima viwanja 5,000 kwa kugawana faida ya asilimia 50 kwa 50.
“Mkataba huo ulisainiwa na Kaimu Meya, Ngalinda, kwa upande wa manispaa bila kupata idhini ya Baraza la Madiwani na mkopo huo ulichukuliwa bila kupata ridhaa ya waziri mwenye dhamana,” alisema.
Alisema kuwa mradi huo gharama za faida zilikuwa zinabadilika kila mara na walikusudia kupata sh bilioni 1.2 ila ziliongezeka hadi kufikia sh bilioni 4.8, lakini zilizoonekana kwa CAG ni sh bilioni 4.6, kwa hiyo milioni 200 hazijulikani zilipo.
Utouh aliongeza kuwa kuhusu tuhuma za matengenezo ya barabara mpya, Manispaa ya Bukoba iliingia mkataba na mkandarasi aitwaye Kajuna Investment wa sh milioni 138.
Alisema kuwa mkandarasi huyo alilipwa fedha za dharura ambazo hazikuwa na nyaraka, hivyo malipo hayo yaliongezwa hadi kufikia sh milioni 227 kwa kutumia barua iliyosainiwa tofauti na ile ya awali.
“Malipo hayo hayakuwa na idhini ya mkandarsi wa serikali na yalikuwa kinyume na kanuni za manunuzi ya umma,” alisema.
Utouh katika tuhuma za mradi wa ujenzi wa soko kuu la mjini Bukoba, alisema walibaini kuwa utaratibu haukupata idhini ya madiwani ya kumlipa mkandarasi mshauri, OGM Consultant sh milioni 789.
Kwamba meya Amani pia aliwaita madiwani na kuwaeleza kuwa mkandarasi anahitaji sh milioni 590, jambo ambalo mmoja wa madiwani wa Kata ya Kitendagulo, Samwel Ruhangisa, alikataa pale pale kwenye kikao.
CAG ameagiza kuwa kampuni hiyo ya OGM irudishe sh milioni 33 zilizotumika kinyume na mkataba.
“Sh milioni 200 zilizotumika kumpatia OGM Consultant ya Dar es Salaam hazikufuata utaratibu kutolewa na mkataba mwingine uliosainiwa kinyume cha sheria na OGM ni sh milioni 700 ambapo madiwani waliambiwa ni milioni 400 na kampuni hiyo hailipi kodi TRA,” alisema.
Kwa mujibu wa Utouh, OGM haikuwa kwenye orodha ya walioomba zabuni ya kufanya kazi ya ukandarasi ushauri katika ujenzi wa soko kuu, lakini alionekana kwenye orodha baadaye ya waliolipwa.
“Makandarasi wote waliolipwa fedha hizo walikuwa hawalipi kodi TRA, hivyo mamlaka ina haki ya kuwadai hizo kodi,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa kituo cha mabasi Bukoba, CAG alisema mradi huu haukutangazwa kwenye gazeti la serikali, lakini walipata mkandarasi na kumlipa fedha za kazi hiyo kinyume na taratibu za serikali.
“Gazeti lililotangaza tenda hiyo halikupatikana, pia timu ya ukaguzi ilitembelea eneo la kazi na kubaini kuwa mkandarasi alilipwa fedha nyingi tofauti na kazi aliyoifanya,” alisema.
Pia ulikuwepo mradi wa maji ambapo kila kata iliyopangwa kuwekwa mradi wa maji ilitakiwa kuchangia asilimia 2, kwamba tuhuma za kata ya meya  kupendelewa zilikuwa za uongo.
Kuhusu tuhuma za uuzwaji viwanja vya wazi, ripoti ilisema kuwa mkataba wa kununua kiwanja kinacholalamikiwa haukufuata taratibu za ununuzi.
Eneo hilo ndiko limejengwa bweni la sekondari ya Peace inayomilikiwa na meya. Katika hilo, CAG alisema walipendekeza kuundwa kwa timu maalumu kuchunguza tuhuma hizo kwani katika eneo hilo hawakufikia mwisho.
“Ujenzi wa barabara za lami kwenye kata ya meya tofauti na fedha zilizoombwa, ilibainika kuwa manispaa iliomba sh milioni 30 kukarabati barabaraba hiyo, lakini Tamisemi ilitoa milioni 300 na walipohojiwa walisema hilo ni la kawaida, hivyo tuhuma hizo ni uongo,” alisema.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa bwawa, alisema kuwa haukuwahi kujadiliwa na Baraza la Madiwani, kwamba ulikuwa ni mradi wa wajanja tu.
Pia Utouh aliongeza kuwa suala la wafanyabiashara  wa soko kuu kutolipa kodi, manispaa imekosa mapato sh milioni 256 kutokana na chanzo hicho.
Juu ya matumizi ya gari lenye namba za usajili SM 4663, ilibainika kuwa limekuwa likiegeshwa katika ofisi ya Radio Kasibante inayomilikiwa na Kagasheki.
“Kumbukumbu za TRA zinaonyesha kuwa ni mali ya halmashauri, lakini alipohojiwa Kagasheki alidai kuwa alinunua kwa fedha zake. Halmashauri haina kumbukumbu zozote juu ya gari hilo.
“Tunapendekeza lirejeshwe kwenye halmashauri kama Kagasheki ataona ni manufaa kwa wananchi, lakini kama haitawezekana basi gari hilo libadilishiwe usajili ili lionekbnane ni la kiraia,” alisema.
Kuhusu uteuzi wa wakala wenye upendeleo kwenye ushuru wa mabasi, alisema kuwa zabuni ya aliyepata rufaa ilitenguliwa kwani haikuwa imesajiliwa na mamlaka husika.
Kwamba alibadilisha jina na kuomba tena kisha kupata, huku muombaji aliyeomba kwa tozo ya juu akinyimwa. Hivyo, manispaa ilifanya upendeleo na kukosa sh milioni 46 kwa mwaka.
Suala la posho kwa madiwani katika safari ya mafunzo nje ya wilaya nalo liliguswa ambapo madiwani wawili waliolipwa sh 400,000 kila mmoja hawakusafiri, lakini fedha hizo hazikurudishwa manispaa.
Kuhusu deni katika uwanja wa mpira wa Kaitaba, ulikarabatiwa na Kiwanda cha sukari Kagera kwa madai ya kurejeshewa fedha zake.
Utouh alisema kuwa sehemu ya fedha hazijarudishwa, na hivyo wanapendekeza kufanya muafaka na kiwanda au zitafutwe fedha za kulipa deni.
Baada ya Utouh kukamilisha ripoti yake, Naibu Waziri wa Tamisemi, Agrey Mwanri, kwa niaba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisoma maagizo ya serikali kufuatia taarifa hiyo.
Alisema kuwa serikali inamwagiza meya Amani awe amejiuzulu wadhifa wake ndani ya siku saba ama asubiri kung’olewa na madiwani kwa kupigiwa kura ya kukosa imani naye.
Pia Mwanri alitangaza kuwavua madaraka aliyekuwa mkurugenzi wa manispaa hiyo, Kaputa, mhadisi wa halmashauri, Nzihirwa na mhasibu, Ulomy na kutaka watendaji wengine wa chini wachukuliwe hatua.
Muda mfupi baada ya maagizo hayo, Amani alitangaza kuachia ngazi huku mji wa Bukoba ukilipuka kwa furaha za wananchi wengi na baadhi ya wafuasi wa meya wakionekana kupigwa na bumbuwazi.

0 comments:

Post a Comment