WIZARA ya Maliasili na Utalii imetuma kikosi maalumu cha askari 20
kuwasaka majangili walioua faru na kuchukua pembe zake, usiku wa
kuamkia jana katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mbali na kufanya ujangili huo, watu hao wanadaiwa kuingia katika
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakiwa na SMG tatu, saa 9 alasiri na
kuvamia basi la abiria na kisha kupora fedha na mali za wasafiri.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Waziri wa Maliasili
na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema kutokana na matukio hayo wizara kwa
kushirikiana na vyombo vya dola imechukua hatua za dharura kuagiza
msako wa majangili ndani ya hifadhi hizo.
Nyalandu alisema kuwa gari lolote linaloingia katika hifadhi hizo,
lazima lipekuliwe ikiwa ni jitihada za kuwasaka majangili hao.
Alisema hadi sasa wamepata taarifa za kuonekana kwa raia watatu wa
nchi moja mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao wanadaiwa
kuunda mtandao wa kumuua faru huyo mkubwa kuliko wote nchini.
“Serikali inawasaka kwa udi na uvumba raia hao watatu, na wananchi
wanaombwa kusaidia kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi ili kufuatilia
nyendo zao kwa karibu,” alisema.
Nyalandu alisema hadi sasa hifadhi ya Serengeti ina faru 32 huku
wale wa mradi maalumu unaosimamiwa na Rais Jakaya Kikwete wakibaki
wanne baada ya mmoja kuuawa mwaka 2012.
“Tupo katika hatua za mwisho kuandaa utaratibu wa kuwa na sheria
kali dhidi ya vitendo vya ujangili, ikiwa ni pamoja na kuweka ujangili
kama uhujumu uchumi,” alisema.
Alisema serikali bado inarekebisha kasoro zilizojitokeza katika
awamu ya kwanza ya Operesheni Tokomeza Ujangili, na kusisitiza kuwa
awamu ya pili ya operesheni hiyo itaanza hivi karibuni, lakini hawezi
kutaja tarehe kwa hofu ya kuwapa faida majangili.
Kuhusu vita ya ujangili
Nyalandu alisema vita ya kupambana na ujangili imekuwa kubwa na
majangili wamekuwa wakitafuta vikwazo kuhakikisha wanakwamisha jitihada
hizo.
“Vita hii sio yangu kama Nyalandu, vita ni ya kila mmoja kwa ajili
ya vizazi vyetu. Kama tutakubali kugawanywa tufahamu kuwa rasilimali
zetu zitakwisha, najua wapo watu wanatafuta vikwazo kuona Nyalandu
naaibika, hata wamekuwa wakipotosha baadhi ya taarifa,” alisema.
Alisema kuwa wapo watu wanaopandikiza maneno ya uongo dhidi ya
viongozi wa serikali walio mstari wa mbele kupambana na majangili.
Watatu wadakwa
Katika hatua nyingine, wiki iliyopita majangili watatu ambao ni
wakazi wa Dar es Salaam walikamatwa wakisafirisha kilo 37 za meno ya
tembo katika gari ndogo, wakitoka mkoani Iringa.
Nyalandu aliwataja waliokamatwa kuwa ni Salome Aloyce mkazi wa
Sinza, Rajabu Omari mkazi wa Kigogo na Kadili Kisanduku wa Mbezi.
Alisema kuwa watu hao walikuwa katika gari dogo aina ya Toyota
Corona mali ya Florian Elias mkazi wa jijini Dar es Salaam. Watuhumiwa
hao wanashikiliwa na polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
0 comments:
Post a Comment