Na Saidi
Mkabakuli
Wakazi
wa mikoa ya kusini ikiwemo Mtwara, Lindi, na Ruvuma inatarajiwa kupata
hospitali ya kisasa ya rufaa itakayojengwa katika eneo la Mikindani, nje kidogo
ya mkoa wa Mtwara katika lengo la kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unakuwa
shirikishi na kuendelea kuboresha huduma za jamii hususan na afya katika mikoa
hiyo.
Hayo
yamesemwa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Ligula, Dkt. Shaibu
Maarifa wakati akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na Timu ya Ukaguzi wa
Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipofanya ziara ya
ukaguzi wa maendeleo ya katika mkoa huo.
“Mradi
wa hospitali ya Rufaa ya Mtwara umelenga kutoa huduma za rufaa kwa kanda ya kusini
hususan mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma, hospitali hii itakapokamilika
inategemewa kuchukua wagonjwa wa nje na ndani watakaohudumiwa kwenye vitengo
mbalimbali vinavyojitosheleza kwa vifaa na wataalamu, “ alisema Dkt. Maarifa.
Kwa
mujibu wa taarifa za awali mradi ulianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2012/13
kwa fedha za Serikali zinazotolewa kupitia ngazi ya wizara ambapo mpaka sasa
ujenzi wa uzio kuzunguka eneo hilo umekamilika.
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo, mmoja wa viongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo
kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri alisema kuwa serikali inatambua umuhimu wa
suala la afya kwa wakazi wa mikoa ya kusini, na akatoa wito kwa uongozi wa mkoa
kuzingatia na kusimamia matumizi sahihi ya fedha za serikali katika mradi huo.
“Madhumuni
ya mradi ni mazuri hivyo mkoa kupitia wizara kuweka msukumo kwa kuhakikisha
mradi unakamilika na kutelezwa kwani utachangia kuboresha huduma za afya katika
maeneo ya kusini na kupunguzia wananchi mzigo wa gharama kwa kufuata hospitali
zilizo mbali na mikoa yao,” alisema Bibi Mwanri ambaye ni Naibu Katibu Mtendaji
anayeshughulikia Huduma za Jamii na Maendeleo ya Idadi ya Watu.
Kwa
mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16) eneo
la afya ni kipaumbele cha nne cha mkakati kwa lengo la kuongeza maendeleo ya
rasilimali watu na ujuzi ambapo Mpango unahimiza kuwekeza katika elimu hasa
katika elimu ya juu na vyuo vya huduma za afya na uongezaji ubora na
upatikanaji wa huduma hizo katika kujenga nguvu kazi itakayoleta maendeleo ya
kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.
Serikali
imeaandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ukiwa na lengo la kuwa na mfumo
madhubuti wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo la Dira ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa
kati ifikapo mwaka 2025.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya
Mkoa wa Mtwara, Ligula, Dkt. Shaibu Maarifa (katikati) akizungumza na Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilimpotembelea Ofisini kwake. Kushoto ni
viongozi wa Timu hiyo, Prof. Longinus Rutasitara (Kushoto) na Bibi Florence
Mwanri (Wapili kulia).
Mganga Mkuu wa Hospitali ya
Mkoa wa Mtwara, Ligula, Dkt. Shaibu Maarifa akisisitiza jambo wakati wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilimpotembelea Ofisini kwake.
Mthamini Mkuu wa Ardhi wa
Mkoa wa Mtwara, Bw. Abdallah Komba (aliyeinama) akiwaelekeza namna ya hospitali
ya rufaa ya mkoa huo itakavyokuwa wakati Timu ya
Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
ilipotembelea mradi huo.
Mmoja wa viongozi wa Timu
Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi
Florence Mwanri (Kushoto) akizungumza wakati timu yake ilipofanya ziara ya
kujionea maendeleo ya maandalizi ya awali ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Timu Ukaguzi wa Miradi ya
Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ikiongozwa kujionea maendeleo
ya maandalizi ya awali ya ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara na
Mthamini Mkuu wa Ardhi wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Abdallah Komba (Wapili kulia
aliyenyanyua mkono).
Sehemu ya uzio unaozunguka
eneo likalojengwa Hospitali mpya ya rufaa mkoani Mtwara.
Picha na Saidi Mkabakuli
0 comments:
Post a Comment