pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

MASHEIKH WA UAMSHO HURU KATIKA KESI ILIYOKUWA IKIWAKABILI

Khamisuu Abdallah na Madina Issa
MAHAKAMA ya wilaya Mwanakwerekwe imewaachia huru watu sita wanaoshukiwa kuwa ni wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislaam Zanzibar (JUMIKI) baada ya kuwaona hawana hatia.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Ame Msaraka Pinja wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe ambae ndie aliekuwa akisikiliza kesi hiyo.

Akitoa hukumu  alisema mashahidi wanne wa upande wa mashitaka pamoja na washitakiwa wenyewe walithibitisha kuwa katika mkusanyiko wao hawakua wakizungumzia mambo ya dini bali walikuwa wakizungumzia muungano.

"Mahakama baada ya kupitia jalada hili kwa uhakika imeona washitakiwa hawa hawana hatia na inawaachia huru kwa sababu kosa waliloshitakiwa halikuwa likihitaji kibali kutoka kwa Mufti kwani walikuwa wakizungumzia mambo ya Muungano, lakini haki ya rufaa imetolewa kwa siku 30 kwa asieridhika na hukumu hii," alisema.

Awali ilidaiwa washitakiwa hao wote kwa pamoja walifanya mihadhara ya kiislamu bila ya kibali cha Mufti kinyume na kifungu cha 6 (1) (4) cha kanuni za kuidhinisha na kuratibu mhadhara zilizotengenezwa chini ya kifungu cha 15 (1) cha sheria namba 9 ya mwaka 2001 na kifungu cha 10 (1) (c) na kifungu cha 14 (2) vya sheria namba 9 ya mwaka 2001 sheria za Zanzibar.
Ilifahamishwa kuwa bila ya halali Mei 26 mwaka jana majira ya saa 3:30 za asubuhi katika viwanja vya skuli ya Lumumba wilaya ya mjini Unguja, washitakiwa hao walifanya mihadhara ya kislamu bila ya kuwa na kibali cha Mufti wa Zanzibar.

Washitakiwa hao ni Mussa Juma Issa,Farid Had Ahmed, Haji Sadifa Haji,Suleiman Juma Suleiman, Fikirini Majaliwa Fikirini na Abdallah Said Ali.
zanzinews

0 comments:

Post a Comment