pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

MRADI WA MABASI YA MWENDO KASI KUANZA KUFANYA SAFARI ZAKE MWAKA HUU


Dar es Salaam.Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo kasi (DART) wamesema kuwa, mabasi machache ya mradi huo yataanza kutoa huduma zake kati ya Kimara hadi Kivukoni kabla ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi kukamilika, mwaka huu.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa (DART), Asteria Mlambo aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam kuwa, utekelezaji wa awamu ya kwanza unaendelea vizuri na kabla ya kukamilika mwakani, mabasi machache yataanza kufanya kazi mwaka huu.
“Mradi wa mabasi haya unatarajia kukamilika mwaka ujao, lakini juhudi zinafanyika kuhakikisha mwaka huu yanapatikana mabasi machache kuanza kutoa huduma,” alisema Mlambo.
Alisema fungu la pili ni Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo ambako kunajengwa maegesho na karakana ya mabasi kwa ajili ya kufanyia matengenezo mabasi na la tatu ni ujenzi wa kituo cha maegesho eneo la Jangwani ambapo pia kutajengwa makao makuu ya mradi kwa ajili ya masuala ya kiutawala.
Mlambo alieleza kuwa, fungu la nne ni eneo la Kivukoni ambako ujenzi wake umefikia asilimia 90, fungu la tano ni ujenzi Kituo Kikuu eneo la Kariakoo Gerezani Quarter na fungu la sita ni vituo vidogo vitakavyoshusha na kupakia abiria.
Alibainisha kuwa mpaka sasa, utekelezaji wa mradi huo upo katika kiwango cha asilimia 55 na kwamba ujenzi wa miundombinu unasimamiwa na Wakala wa Usimamiaji wa Barabara nchini (Tanroads).
“Kampuni ya ushauri ya Rebel Group kutoka Uholanzi ambayo ilishinda zabuni itasaidia kupata watoa huduma baada ya kutangazwa zabuni hiyo hapo mwezi Mei, mwaka huu,” alisema.
Alisema katika utekelezaji mradi huo, wakala ulikutana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya huduma mbalimbali zilizokuwa zinaendeshwa kando ya barabara,ambapo wakala alilazimika kuingia gharama kuviondosha.
Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo kasi ambao upo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (Tamisemi) unatekeleza mradi wa mabasi hayo ili kutatua kero ya msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment