SERIKALI imesema itajenga makaburi ya mashekhe wawili maarufu,
yaliyodaiwa kubomolewa na Mgambo wa jiji la Dar es Salaam katika
operesheni ya usafi inayoendelea.
Katika operesheni hiyo, mgambo hao walidaiwa kuvunja makaburi ya
Tambaza yaliyopo Upanga jijini Dar es Salaam, yakiwemo ya Shekhe Yahya
Hussein na Shekhe Kassim bin Juma.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alisema baada ya
tukio hilo, walifuatilia na kubaini matingatinga yaliyotumika kubomoa
makaburi hayakuwa yanayotumiwa na jiji.
“Awali familia za mashekhe hao zilieleza kutaka kugharamia
ujenzi wa makaburi hayo, lakini sisi kama serikali tumeona tuyajenge na
kuwaomba watuachie sisi,” alisema.
Alisema baada ya kuvunjwa kwa makaburi hayo, walichobaini ni kuwa
kuna uwezekano jumuia ya wamiliki wa vibanda vilivyopo karibu na
makaburi hayo, wanatengeneza njama ili kuzorotesha operesheni hiyo.
Alisema kuna watu wachochezi waliotumia makaburi ya viongozi hao ili
familia zao zichukie serikali. Alisema pale kuna makaburi mengi, kwa
nini yabomolewe ya viongozi pekee.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa alisema serikali haiwezi kujenga uzio katika
makaburi hayo, kama familia za viongozi hao zilivyoomba, kwani
wakifanya hivyo itabidi kujenga uzio makaburi yote mkoani humo, ambayo
ni mengi.
“Ni vema kwa kutumia taasisi yao kujenga uzio, kwani serikali
ikifanya hivyo itatumia gharama kubwa lakini mimi kama Sadiki
nitaangalia namna ya kusaidia ombi hilo,” alisema.
Awali, mtoto wa marehemu Shekhe Yahya Hussein, Hassan Yahya Hussein
alisema familia hizo mbili zimeumizwa na kitendo hicho na kuomba
serikali iwasake na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika.
Alisema dawa ya kuepukana na matatizo kama hayo ni kujenga uzio
katika makaburi hayo. Alisisitiza kuwa watajenga makaburi ya wazazi wao
kwa gharama zao wenyewe.
Katika tukio hilo, familia inayomiliki eneo hilo la makaburi
ililalamikia kitendo hicho na kusema kimefanyika usiku bila taarifa, na
maeneo mengine hayahusiki na operesheni hiyo.
Msemaji wa familia hiyo, Msakala Tambaza alisema mgambo wa operesheni
hiyo walipofika hapo, waliwaambia wamiliki wakae umbali wa mita 100 na
dhahiri hao ndio walioharibu makaburi hayo.
Alitoa wito kwa serikali kuwalipa gharama za uharibifu wa makaburi na sehemu zilizobomolewa zisizohusika, walipwe gharama.
0 comments:
Post a Comment