Kaunti ya Lamu ilikuwa eneo ambalo mashambulizi mengine mabaya kabisa
yalitokea mwishoni mwa wiki na ambayo al-Shabaab inadai kuhusika, jambo
ambalo lilisababisha maofisa wa huko kuweka marufuku ya kutotembea
nyakati za usiku kwenye eneo hilo kujaribu kuidhibiti hali ya usalama.
Mnamo Ijumaa (tarehe 18 Julai), watu wenye silaha walilirushia risasi
basi moja lililokuwa likisafiri kutoka Mombasa kwenda Lamu karibu na
mji wa Witu, umbali wa kilomita 50 kutokea kisiwa cha Lamu.
Polisi wanashuku kwamba watu hao wenye silaha walitumia gari
waliyoiteka aina ya Toyota Probox kuziba njia kabla ya kulishambulia
basi hilo, na kisha gari la polisi ambalo lilifika kwenye eneo la tukio,
na kuwaua watu saba na kuwajeruhi wengine tisa.
"Majira ya saa 1:00 magharibi, basi linalobeba abiria 45 la Tahmeed
lilimiminiwa risasi," Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Miiri Njega, aliiambia
Sabahi. "Tunasikitika sana kwamba madereva wa basi hilo na gari ya
Probox na muuguzi mmoja aliyekuwa akifanya kazi hospitali ya Hindi
waliuawa."
Watu hao wenye silaha pia waliwauwa maafisa wanne wa polisi
waliokimbilia kwenye eneo la tukio, alisema Njenga. "Polisi mmoja
alijeruhiwa tumboni na wanane wengine wamelazwa kwenye hospitali
mbalimbali wakiuguza majeraha."
Al-Shabaab ilidai hapo hapo kuhusika na mashambulizi hayo, ikisema
kwamba kundi hilo "lilikuwa tayari kutenda au kushambulia popote
inapolazimika ndani ya Kenya."
"Mashambulizi haya ni jibu la wazi kwa madai ya uongo ya serikali ya
Kenya kwamba wameimarisha ulinzi kwenye eneo hilo," msemaji wa kijeshi
wa al-Shabaab, Abdulaziz Abu Musab, aliliambia shirika la habari la AFP.
Lakini Njenga aliyakanusha madai kwamba mashambulizi haya ya karibuni
kabisa yanakwenda kinyume na kauli ya serikali kwamba ulinzi
umeimarishwa kwenye eneo hilo.
"Ukweli kwamba maafisa wetu wanne wa polisi waliuawa na wengine
wawili kujeruhiwa ni ushahidi wa kutosha kwamba tumeimarisha uwepo wa
maafisa wa usalama Lamu," aliiambia Sabahi.
"Kuwepo kwa polisi kulizuia mauaji zaidi," alisema, akiongeza kwamba
serikali ilikuwa haiondoi uwezekano kwamba makundi mengine yanaweza kuwa
yamehusika na mashambulizi hayo.
Amri ya kutotoka nje yakumbana na upinzani
Kufuatia mashambulizi hayo, Mkuu wa Polisi David Kimaiyo alitoa amri
ya kupiga marufuku watu kutoka nje kuanzia saa 12:30 magharibi hadi saa
12:30 asubuhi kwa mwezi mmoja kuanzia Jumapili (tarehe 20 Julai).
Hata hivyo, amri hiyo ya kutotoka nje ilikumbana na upinzani kutoka
kwa Baraza Kuu la Waislamu nchini Kenya (SUPKEM) na Kiongozi na Walio
wengi Bungeni, Aden Duale, wakihoji kwamba itawaathiri Waislamu
wanaofunga Ramadhani.
"Wiki hii ni miongoni mwa wiki muhimu kabisa kwenye mwezi mtukufu wa
Ramadhani ambapo Waislamu ulimwenguni kote wanajikaza kuswali, kuomba na
kutubu," Duale aliliambia gazeti la The Standard la Kenya. "Tumemuambia
[mkuu wa polisi] kuiondoa sehemu fulani ya marufuku hiyo na kuiweka tu
barabara kuu na sio mijini ambako harakati za kidini zinaendelea."
Katibu Mkuu wa SUPKEM, Adan Wachu, alisema ingawa anaamini kuwa
serikali iliweka amri hiyo kwa nia njema, masuala kadhaa
hayakuzingatiwa.
"[Kimaiyo] anahitajika kuisitisha marufuku yake ya kutotoka nje hadi
mwishoni mwa Ramadhani ili kuwawezesha Waislamu kwenye eneo hilo kuabudu
kwa uhuru kwani inaathiri na kuingilia haki na uhuru wao," alisema
Wachu.
Ilipofika Jumatatu jioni, Kimaiyo alitangaza kuwa amri hiyo ya
kutotoka nje italegezwa ili kuwakubalia wakaazi wanaofunga Ramadhani
kuhudhuria sala za usiku.
“Kiufundi, amri ya kutotoka nje utatekelezwa isipokuwa wakati wa sala za [usiku],” Duale aliiambia Sabahi.
“Polisi watafunzwa wakati wa sala ili yeyote atayepatikana katikati
ya sala hizo atajibu mwenyewe anachofanya,” alisema, akiongezea kuwa
waumi wa dini ya Kiislamu wamehimizwa kushirikiana na vikosi vya usalama
ili kufanya siku za mwisho wa Ramadhani kuwe wa amani.
Gibson Waweru, ambaye ni daktari wa maabara kwenye kliniki moja ya
Kongowea iliyo umbali wa kilomita 30 kutoka Mpeketoni, alisema marufuku
hiyo inawafaidisha tu wahalifu wanaotaka kupandikiza hofu miongoni mwa
wakaazi na kuumiza uchumi wa eneo hilo.
"Ni jambo lisilo na mantiki kwa serikali kutuamuru kukaa ndani kuanzia saa 12:30 magharibi ambapo watu wenye silaha wamewashambulia watu kwenye majumba yao," alisema, akiongeza kwamba vikosi vya usalama lazima vibadili mbinu zao ili viweze kuwa na ufanisi.
"Kuna maafisa kibao wa usalama tunaowaona, lakini wanaweza kutabirika
kirahisi kwenye operesheni zao," alisema. "Wanatembea kwa makundi kwa
wakati mmoja na maeneo wanayoyawacha yanakuwa rahisi kushambuliwa."
Kufyatua risasi kiholela mjini Mombasa
Wakati huo huo siku ya Jumapili, watu wasiopungua wanne waliuawa na
wanane kujeruhiwa katika kitongoji cha Soweto cha mjini Mombasa katika
shambulio lililofanywa na watu wenye silaha waliokuwa wakiendesha
pikipiki, kwa mujibu wa vyanzo vya kitabibu.
Mkuu wa polisi wa Mombasa Robert Kitur aliiambia AFP kuwa utambulisho
wa wauaji bado haujajulikana na hakuna kikundi kilichodai kuhusika.
Joshua Mutua, mwenye umri wa miaka 44, ambaye kazi yake ni kuhamisha
fedha katika kioski cha M-pesa, alisema alimuona mtu mmoja mwenye
aliyejifunika akishuka kutoka kwa pikipiki huku akionesha kile
kilichoonekana kama bunduki ya kushambulia ya AK-47.
"Nilidhani alikuwa askari lakini alipoanza kufyatua risasi kiholela,
nilijificha ndani ya duka langu," aliiambia Sabahi. "Niliweza kuwasikia
watu waliochanganyikiwa wakipiga kelele na kukimbia."
Wakati bunduki ziliponyamaza, Mutua alisema alichungulia kwenye pengo
katika duka lake na kuona mtu wenye umri wa kati ambaye kabla alimuuzia
muda wa maongezi akiwa amepigwa risasi katika mguu na amelala katika
bwawa la damu.
"Alikuwa anaugua kwa maumivu lakini hakuna aliyethubutu kutoa msaada
moja kwa hofu kwamba wauaji walikuwa wanasubiri watu waje juu," alisema.
Mutua alisema kwamba watu wengi walikuwa wanabuni sababu za shambulio
lile, lakini yeye alikuwa akitumaini kwamba al-Shabaab bado haijaeneza
"utawala wao wa kigaidi" kutoka Lamu hadi Mombasa.
"Hii itakuwa ndoto kwa sisi na jehanam utukiwa hai kwa sababu ina maana hata mji mkubwa kama Mombasa sio salama tena," alisema.
Ikiwa al-Shabaab ni kweli wako nyuma ya shambulio la karibuni la
Lamu, inaweza kumaanisha kundi limeweka mikakati ya kulenga mji wa
mwambao ili kudhoofisha uchumi wa Kenya, alisema mchanmbuzi wa masuala
ya usalama wa Kenya na mstaafu Meja wa jeshi Bashir Haji Abdullahi.
"Kaunti ya Lamu ni kitovu cha utalii kwa Kenya. Kuishambulia kaunti
hii kunavutia tahadhari ya kimataifa pia kwa sababu baadhi ya wageni
wanamiliki mali huko," aliiambia Sabahi.
"Suala lingine ni sababu za kidini," alisema. "Kaunti ya Lamu
inakaliwa na Waislamu na Wakristo karibu sawasawa. Imani mbili hizi
zimekuwa zikikaa vizuri kila mmoja na mwenzake kwa miaka mingi. Kwa
kuaznsiah mshambulizi, al-Shabaab inataka kujenga uadui kati ya dini na
kuchochea vita vya kidini ambayo vitacheza katika mikono ya kundi hili".
'Ugaidi usioweza kusimamishwa'
Yeyote aliyehuiska, Alphaus Akama, mlinzi wa kampuni binafsi ya
ulinzi mjini Mombasa mwenye umri wa miaka 32, alisema ataihamishia
familia yake kwenye kaunti ya kwao ya Kisii mwishoni mwa mwezi huu.
"Mashambulizi haya ya mara kwa mara yameshusha heshima ya serikali na
hakikisho wa vyombo vya usalama kwa wananchi wanaohofia usalama wao,"
aliiambia Sabahi. "Tunahisi kwamba ama viongozi wa serikali hawana jinsi
au nia ya kuwakabilia washambuliaji na kukomesha ghasia."
Mkaazi mwengine wa Mombasa, John Mwandeghu mwenye umri wa miaka 41 na
ambaye anafanya ya kuendesha mashine ya lifti kwenye bandari ya
Kilindini, alisema wauwaji wanashambulia wanavyotaka bila ya kuzuiwa na
vyombo vya usalama.
"Kwa kweli, mashambulizi haya dhidi ya mji wa pili kwa ukubwa nchini
Kenya yanaonesha serikali haina njia za namna ya kuushinda ugaidi wa
kushitukizia, kuzuia mashambulizi au kuwakamata wahalifu," aliiambia
Sabahi.
Margaret Katana, muuza duka kwenye duka kubwa la Tusky mjini Mombasa
na mwenye umri wa miaka 30, alisema anachanganyikiwa juu ya nani
amuamini kwani serikali inalilaumu kundi la Baraza la Jamhuri ya Mombasa
(MRC) ambapo al-Shabaab inabeba yenyewe dhamana ya mashambulizi hayo na
inayasindikiza matendo yake kwa maelezo.
"Kama raia, kwa hakika hatushughuliki na kujua nani anahusika.
Tunachokitaka ni kusikia kwamba wauaji ama wameuawa au kutiwa nguvuni na
kukomesha kuoneshana vidole na kutupiana lawama," alidai.
Katana alielezea wasiwasi wake kwamba aidha serikali imelemewa na iko
kwenye kuukana uhalisia au inarejea mikakati ya kiusalama ambayo
imeshindwa.
"Lamu haijaijua amani kwa miezi kadhaa sasa, na bado eneo hili
linapaswa kuwa salama na lenye amani kwani lina maafisa wa usalama
katika kila kipembe cha kaunti hii, huku wauaji wakiwa na uthubutu wa
kutosha kuweza kuwauwa wananchi na walinda usalama wenyewe," alisema.
"Nahofia nani anapaswa kumlinda nani?"
0 comments:
Post a Comment