WAZIRI
Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amenusurika kifo hivi karibuni baada ya
ndege ya shirika la Precision Air, iliyokuwa ikitoka Mwanza kwenda Dar
es Salaam kupata hitilafu ya injini.
Ndege
hiyo, ambayo iliondoka Mwanza saa 2:30 usiku, ilipata hitilafu ya
injini moja muda mfupi tu baada ya kuruka, hali iliyomlazimu rubani wa
ndege hiyo kubadili mwelekeo na kutua katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Akizungumza
na Mtanzania jana, Sumaye, ambaye alikuwa mmoja wa abiria waliokuwemo
kwenye ndege hiyo, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Sumaye
alisema kitendo cha injini kupata hitilafu, ilimlazimu rubani wa ndege
hiyo kuruka na injini moja mpaka KIA, ambako walitafutiwa ndege nyingine
ili kuendelea na safari.
Alisema
kutokana na tatizo hilo, abiria walilazimika kuondoka KIA kwa
kugawanywa kwenye ndege tofauti zilizokuwa zikielekea Dar es Salaam
ambapo Sumaye aliondoka saa 7 kasoro usiku.
Msemaji
wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bestina Magutu,
alipotafutwa ili kujua kilichotokea kwenye ndege hiyo, alisema kuwa
hakuwa na taarifa zozote za hitilafu ya ndege hiyo.
“Hebu ongea nao wenyewe, sijapata taarifa zozote mpaka sasa, nimetoka ofisini jana sikuwa na taarifa,” alisema Magutu.
Naye Mratibu wa Masoko wa Precision Air, Hilaly Mremi, alipozungumza na Mtanzania alikiri kutokea kwa hitilafu hiyo ya ndege.
“Kwa
kifupi hakuna ajali iliyotokea, hitilafu zinazotokea kwenye ndege ni za
kawaida kama ambavyo gari inaweza kuharibika na kupakiwa pembeni,” alisema Mremi.
Alisema safari za shirika hilo zinaendelea kama kawaida na kutaja namba ya ndege hiyo kuwa ni TW 415.
Ndani ya wiki hii, ndege mbili za shirika hilo zimenusurika ajali baada ya kupata hitilafu wakati zikiwa angani.
Mbali
na ndege hiyo aliyokuwemo Sumaye, ndege nyingine ya shirika hilo yenye
namba ya safari Pw 77 na ya usajili TWC, iliyokuwa ikitoka Mwanza kwenda
Kilimanjaro ilinusurika kupata ajali juzi jioni na hivyo kulazimika
kurudi na kutua kwa dharura uwanjani hapo baada ya kupata hitilafu ikiwa
angani.
Mbali
na Sumaye, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, naye aliwahi pia
kupata ajali mwaka jana akiwa kwenye ndege za shirika hilo.
Lowassa
alikuwa miongoni mwa abiria 37 waliokuwa wamesafiri na ndege hiyo
ambayo ilipasuka magurudumu manne ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa
Ndege wa Arusha.
Katika
ndege hiyo pia kulikuwa na maofisa mbalimbali wa Serikali na Jeshi la
Wananchi, ambao walikwenda kuhudhuria sherehe ya kutolewa kamisheni kwa
maofisa wa jeshi katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA).
0 comments:
Post a Comment