
Dar es Salaam. Mitandao
ya kihalifu inazidi kujiimarisha nchini na sasa kumeibuka makundi ya
wauaji wa kukodi katika mikoa ya kaskazini mwa nchi pamoja na Kanda ya
Ziwa.Mbali na mauaji ya albino na vikongwe ambayo yalipata kutikisa
katika maeneo kadhaa ya nchi, wauaji wa kukodi wanatumika kutekeleza
uhalifu huo kwa lengo la kulipiza kisasi, uporaji wa fedha, kujitanua
kibiashara au kudhulumu mali na fedhaUchunguzi wa muda mrefu uliofanywa
na gazeti hili umebaini kuwa silaha nyingi zinazotumika katika mauaji ya
kukodi yanayofanyika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, hununuliwa ama
kukodishwa kutoka Namanga upande wa Kenya.
Wauzaji
wa silaha hizo ni ama raia wa Kenya wenye asili ya Kisomali ama
wahamiaji haramu wenye asili ya Kisomali wanaoingia nchini, wakitokea
Somalia kupitia Kenya.
Uchunguzi
umebaini kuwa bunduki aina ya Submachine Gun (SMG) huuzwa kati ya Sh3
milioni hadi Sh5 milioni na bastola zikiuzwa kati ya Sh500,000 na Sh1.2
milioni.
Pamoja
na kutoka nje ya nchi, wauaji wengine wa kukodi hupatikana nchini
kulingana na aina ya mtu wa kuuawa, mazingira na ugumu wa kazi.
Kwa
Tanzania, mikoa inayoongoza kwa kuwa na wauaji wa kukodi ni Arusha na
Manyara na Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa ukiguswa kuwa jirani na mikoa
hiyo.
Akizungumza
kwa sharti la kutotajwa jina, mtoa taarifa wetu alisema alisema: “Hata
sasa ukihitaji vijana wa kazi nitakuunganisha. Jambo muhimu hakikisha
huwarushi (unawapa fedha zao), ukiwarusha lazima na wewe watakuua.”
“Yupo
rafiki yangu anayewafahamu vyema kwa sababu amewahi kuwaunganisha na
waliokuwa wakihitaji huduma yao,” alisema mtoa habari huyo.
Malipo ya kuua
“Malipo
kwa kazi hii yanaanzia kati ya Sh1 milioni na Sh5 milioni kutegemea na
uzito wa kazi husika,” alisema mtoa taarifa wetu anayeishi Arusha na
akithibitisha kwamba anafahamiana na madalali wa wauaji hao.
Alisema
mara nyingi wauaji hao hawataki kukutana na wateja moja kwa moja ili
kuepuka kutambulika, badala yake hukutana au kuwasiliana na mtu wa kati
(wakala) ambaye pia hupokea malipo na kuwakabidhi.
Hata
hivyo, uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa kiasi cha malipo kwa
mikoa ya Kanda ya Kaskazini ni kikubwa ikilinganishwa na Kanda ya Ziwa
ambako hulipwa fedha kidogo.
Vyanzo
hivyo vimedokeza malipo wanayopata katika mikoa hiyo ni Kati ya
Sh200,000 hadi Sh1 milioni kwa kuzingatia eneo husika na walikotolewa na
kwamba fedha hizo huwa ni ujira wa watu wawili au zaidi.
Katibu
wa Jumuiya ya Kuhifadhi Mila na Desturi za Mtanzania Kanda ya Ziwa,
Gambang’adi Kaliba anasema wanaokodiwa ni wale wasiokuwa na vipato,
walevi na wavuta bangi ambao wamekata tamaa ya maisha, hivyo hupewa
fedha kidogo kwa ajili ya mauaji hayo ya kikatili.
“Watu
wanalipwa Sh200,000 mpaka 500,000 kwa kuwa hawafanyi kazi wanaziona
nyingi na wamekuwa wakijulikana katika baadhi ya maeneo kwa kuwa
wakilewa hutamba na kuwa wako tayari kumwaga damu ya mtu maadam wapewe
fedha,” anasema Kaliba.
Mkoani
Mara, uchunguzi ulibaini kuwa kumekuwapo na mauaji ya aina hiyo na
kwamba malipo kwa kifo cha mtu huwa ni kati ya Sh300,000 na 500,000.
Mwanaharakati
wa Haki za Binadamu wilayani Ukerewe ambaye aliomba jina lake
lihifadhiwe anasema wanapowakamata wahusika wa mauaji, baadhi hukiri
kukodiwa kwa malipo ya Sh200,000 na kwamba idadi yao huwa ni kati ya
watu wawili au watatu.
Mifano hai
Chanzo
kimoja kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani Manyara kililiambia
gazeti hili kuwa mauaji ya mmoja wa wafanyabiashara yalifanywa kwa
kutumia mtandao huo.
Aliuawa mwaka jana wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.
“Mirerani
ndiyo umafia huo unatumika sana unajua kule ni unyama unyama kwa hiyo
mtu kukuua kwa sababu ya mawe ni jambo la kawaida,” alidokeza polisi
huyo.
Habari
za kipolisi zinaeleza kuwa wauaji wa mfanyabiashara huyo walilipwa kati
ya Sh3 milioni milioni na Sh5 milioni baada ya kukodiwa mahususi
kutekeleza mauaji hayo.
Bunduki
aina ya SMG inayodaiwa kutumika katika mauaji hayo ilinunuliwa kwa Sh4
milioni katika mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga kutoka kwa watu wenye
asili ya Somalia.
Mauaji
mengine yanayofanana na hayo yalitokea Januari 26, 2006 saa 2:30 usiku
nje ya klabu maarufu ya Peters Club iliyopo Majengo katika Manispaa ya
Moshi mkoani Kilimanjaro.
Siku
hiyo watu waliokuwa na SMG walimmiminia risasi mfanyabiashara wa magari
ya ‘dili’, Aristarik Msacky (34) na kutochukua chochote isipokuwa simu
yake ya mkononi.
Kabla
ya kuuawa, mfanyabiashara huyo alikuwa akinywa pombe na marafiki zake
ndipo alipopigiwa simu ili atoke nje kuna ‘biashara’ na alipotoka nje ya
baa ili kukutana nao ndipo alipouawa.
Tukio
jingine ni lile la mkazi wa Kijiji cha Nyichoka wilayani Serengeti,
Mara ambaye alituhumiwa kumuua mwendesha pikipiki (bodaboda), Julai 5
mwaka huu ambaye kwa mujibu wa polisi, alikiri kufanya mauaji hayo kwa
kukodiwa.
Polisi
walisema mtuhumiwa huyo (jina tunalihifadhi) alikiri kwamba yeye na
mwenzake ambaye aliuawa na wananchi wenye hasira kali, walikodiwa na
mkazi wa Park Nyigoti kutekeleza mauaji hayo kwa Sh500,000 kwa madai
kuwa bodaboda alikuwa na uhusiano na wake zake.
Hata
hivyo, mpaka wanatekeleza mauaji hayo kwa kumkatakata na kumtumbukiza
mtoni, walikuwa wamelipwa Sh40,000 tu na kati ya fedha hizo Sh20,000
zilikuwa za kukodi pikipiki na zilizobaki kwa ajili ya chakula. Hadi
mmoja alipouawa na yeye kukamatwa walikuwa wakimdadisi ‘bosi’ wao
Sh460,000.
Msemaji wa Polisi
Msemaji
wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema polisi wapo kwa ajili ya
kulinda usalama wa raia na mali zao na hivyo ndivyo wamekuwa wakifanya
kila wakati, kutimiza wajibu huo.
Senso
alisema kwamba endapo wakibaini kuwa kuna watu wanafanya uhalifu wa
namna hiyo huwakatama na kuwafikisha mahakamani, huku akitoa mwito kwa
wananchi na jamii nzima kutimiza wajibu wao wa kutoa taarifa za makundi
kama hayo katika maeneo wanayoishi.
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment