Kundi la watu wenye misimamo ya
chuki dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu nchini Ufaransa wameuvunjia
heshima Msikiti katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo. Gazeti la Le
Figaro linalochapishwa nchini Ufaransa limeandika kuwa, mfanyakazi wa
msikiti ulioko katika eneo la Pontarlier mashariki mwa Ufaransa, jana
aliushuhudia mzoga wa nguruwe uliotupwa kwenye mlango wa kuingilia
msikitini. Taasisi kadhaa za Kiislamu nchini Ufaransa zimetoa tamko la
kulaani vikali kitendo hicho, kinachokinzana na uhuru wa kuabudu. Polisi
ya Ufaransa imeshaanza uchunguzi kuhusiana na kitendo hicho
kinachoonyesha wazi kuwepo chuki dhidi ya dini ya Kiislamu nchini humo.
Kiongozi wa serikali katika eneo hilo amelaani kitendo hicho na
kusisitiza kwamba, serikali ya Paris itaendeleza juhudi za kuwasaka na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wahusika wote wa kitendo hicho.
Naye mmoja kati ya viongozi wa Baraza la Waislamu wa Ufaransa CFCM
amesema kuwa, tokea yaliposhadidi machafuko katika eneo la Mashariki ya
Kati, vitendo vya chuki na uadui dhidi ya dini ya Kiislamu vimeongezeka,
katika hali ambayo Waislamu wanataka kuishi na wafuasi wa dini nyingine
nchini humo kwa amani.
0 comments:
Post a Comment