MWENYEKITI
Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, ameshinda tuzo ya
Mwaka ya Mfanyabiashara Bora Afrika (AABLA), kundi la Afrika Mashariki.
Sherehe za tuzo za AABLA, kundi la Afrika Mashariki zilifanyika
Septemba 20 mjini Nairobi, Kenya na kurushwa hewani moja kwa moja na
runinga barani Afrika.
Kwa mujibu wa runinga ya masuala ya fedha na biashara Afrika (CNBC
Africa), ambao ndio waandaji wa sherehe hizo, tuzo hizo za kila mwaka
zimebuniwa kwa ajili ya kutambua utendaji uliotukuka katika biashara,
wenye mafanikio makubwa kwenye sekta zao za biashara na vilevile kwenye
jamii, ambako biashara hizo zinaendeshwa.
Mengi ambaye alikuwa akichuana na wafanyabiashara wengine wanne wa
ukanda huu wa Afrika Mashariki, mbali ya kushinda tuzo hiyo pia alipata
tuzo ya mafanikio katika maisha na kusaidia huduma mbalimbali za jamii
nchini.
Dk. Mengi amekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma mbalimbali
za jamii kama vile kwa wasiojiweza, harakati za kupambana na kuondoa
umasikini, kusaidia vikundi katika kuinua uchumi na mengine.
Tuzo ya mfanyabiashara bora wa kike Afrika, imechukuliwa na Tabitha
Karanja ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni yake ya Keroche
Breweries Limited inayotoa ajira kwa zaidi ya watu 300.
Karanja amekuwa akitoa sehemu kubwa ya faida yake kusaidia jamii na kutoa elimu kwa vijana nchini Kenya.
Watanzania wengine waliopata tuzo hizo ni Ofisa Mtendaji wa Helvetic
Solar Ltd, Patrick Ngowi, (EA Young Business Leader) na Ofisa Mtendaji
wa Techno Brain Ltd, Manoj Shanker (Entrepreneur of the Year).
0 comments:
Post a Comment