pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Hongera: Makinda Rais mpya Bunge la SADC

MKUTANO wa 36 wa Bunge la nchi
wanachana wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),
umemchagua kwa kishindo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda kuwa Rais wa Bunge hilo kwa kipindi cha miaka miwili ijayo. Mbunge wa Malawi, Njovya Lema
amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais.
Makinda, ambaye hakuwa na mpinzani katika uchaguzi huo uliofanyika juzi, aliungwa mkono na wajumbe wote wa mkutano huo, ambao ni Maspika na Wabunge kutoka mabunge ya nchi wanachama wa SADC. Alichaguliwa wakati wa kuhitimisha Mkutano wa 36 wa Jukwaa la Mabunge ya SADC,
uliokuwa ukifanyika mjini hapa. Msimamizi wa uchaguzi, ambaye ni Katibu Mkuu wa Bunge la SADC, Dk Esau Chiviya alisema kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za Bunge hilo Kanuni ya 42 (2) inatamka wazi kuwa endapo kutakuwa na mgombea mmoja pekee, basi atawahoji wajumbe na endapo watamkubali basi atamtangaza
rasmi kuwa amechaguliwa kushika nafasi hiyo.
“Kwa kuwa Spika wa Bunge la Tanzania Mheshimiwa Anne Makinda hana mpinzani na kwa kuwa nimewahoji na wote mmemuunga mkono, basi natangaza kuwa ndiye Rais mpya wa Bunge la SADC kwa miaka miwili ijayo,” alitangaza Dk Chiviya. Awali, kwa mujibu wa utaratibu wa uongozi ndani ya chombo hicho, Makinda alitakiwa kugombea nafasi hiyo pamoja na Spika wa Ushelisheli na Msumbiji, ambao hawakushiriki uchaguzi huo na badala yake walimuunga mkono Makinda. Akisoma hotuba yake ya shukrani kwa wajumbe wa Mkutano huo, Makinda alisema:
“Ninalo deni kubwa kwenu kwa jinsi
mlivyoniunga mkono na kama mnavyojua jukumu letu kubwa mbele yetu ni kuwa na Bunge imara la SADC, jambo ambalo nawahakikishia kwa pamoja tutafanikiwa. “Kama mnavyojua, malengo makuu ya SADC
PF ni kuwa na Bunge la kikanda
litakalowakilisha mawazo ya pamoja kutoka kila Bunge la Nchi wanachama wa SADC, hili ndilo lengo kuu la waasisi wa umoja huu walilokusudia wakati wa kuanzisha chombo hiki mwaka 1997 hivyo na sisi lazima tulienzi na kulitekeleza.”

0 comments:

Post a Comment