pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Vigogo TPDC watiwa mbaroni

VIGOGO wawili wa Shirika la Maendeleo ya Mafuta na Petroli (TPDC) jana walijikuta wakisota rumande kwa saa kadhaa baada ya kushikiliwa na Polisi, kwa kile kilichoelezwa ni kukiuka agizo la Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyokuwa imeagiza ikabidhiwe mikataba 26 ya gesi iliyofikiwa kati ya Serikali na wawekezaji. Waliokumbana na adha hiyo na kujikuta wakifikishwa katika rumande ya Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, eneo la Stesheni, ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya
TPDC, Michael Mwanda na Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo James Andilile.
Amri ya kukamatwa kwa viongozi hao
walioondolewa eneo la Ofisi Ndogo ya Bunge kwa gari la Polisi, ilitolewa jana saa sita mchana na viongozi wa PAC kutokana na viongozi hao wa TPDC kushindwa kutekeleza agizo la kuwasilisha mikataba na taarifa za
mikataba 26 ya gesi ambayo kamati ilitoa agizo hilo miaka mwili iliyopita.
Kutokana na hatua hiyo ya kukamatwa kwa vigogo hao, PAC imeiandikia ofisi ya Spika wa Bunge kuhakikisha wanaandaa mashitaka na kuyapeleka Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) ili aweze kuwafungulia mashitaka vigogo hao.nHii ni mara ya kwanza kwa Bunge kuagiza maofisa wa juu wa taasisi za umma kukamatwa kwa kushindwa kutekeleza maagizo ya kamati hizo ambazo zinafanya kazi ya kuisimamia Serikali. Januari 2012, PAC iliitaka TPDC kuwasilishanmikataba 26 ya gesi, taarifa ya mapitio ya mikataba ya gesi na taarifa ya ujenzi wa bomba la gesi, agizo pekee ambalo shirika
hilo limelitekeleza. Mapema wiki iliyopita katika kikao cha PAC kilichokuwa kinapitia hesabu za shirika hilo kwa mwaka 2012/13, viongozi hao wa TPDC walipewa siku mbili kutekeleza agizo hilo, lakini walishindwa kufanya hivyo. Ijumaa iliyopita, Katibu wa Bunge aliiandikia
TPDC na kuitaka kuhakikisha kufikia jana saa nne asubuhi wanawasilisha mbele ya kamati mikataba 26 ya gesi na taarifa ya mapitio ya mikataba hiyo, jambo ambalo pia halikutekelezwa.
Baada ya kukutana na kamati hiyo jana, viongozi hao wa juu wa TPDC waliongozwa na Mwanasheria wa Bunge, Nenelwa Mwihamba kula kiapo cha kusema ukweli kwa kamati hiyo.
Mwihamba alielezea taratibu sheria ya kinga na Mamlaka ya Bunge sura 296 inatoa haki kwa Bunge na kamati zake kuomba taarifa na nyaraka mbalimbali ambazo kamatininazihitaji kwa ajili ya utekelezaji.
Alisema mamlaka hayo yameainishwa katikanKifungu cha 10 cha sheria hiyo kinachoelezea mbunge mmoja mmoja na kifungu cha 13 kinachoongelea Bunge na Kamati zake. Mwihamba alisema kifungu cha 18 (2) cha sheria hiyo kinamzuia mtumishi wa umma
kutoa taarifa zinazohusu masuala ya kijeshi na usalama wa taifa isipokuwa kwa kibali cha Rais.
“Januari 26, 2012 Kamati ya Bunge ilitaka TPDC kuwasilisha mikataba na taarifa ya mapitio ya mikataba, kwa kipindi chochote katika mawasiliano TPDC hakuna maelezonyoyote kuwa mikataba hiyo inahusu masuala ya kijeshi au usalama, hivyo tunaona kamati ina haki ya kupewa mikataba hiyo.” Mwihamba alisema kwa kosa hilo, adhabu inayowakabili ni faini isiyozidi Sh 500,000, au kifungo kisichozidi miaka mitatu jela au adhabu zote mbili kwa pamoja. Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alitoa nafasi kwa Kaimu Mkurugenzi wa TPDC kutoa maelezo yao, ambapo Andilile alisema
ofisi yake imelifanyia kazi agizo ambalo kamati hiyo iliagiza. “Kwa sababu mikataba yote inasimamiwa na
Mwanasheria Mkuu na masuala ya kisekta yanasimamiwa na Wizara ya Nishati na Madini, hivyo tuliona tuwasiliane na vyombo husika ili kupata mwongozo,” alisema. Aliongeza kuwa walimwandikia Mwanasheria
Mkuu kuomba mwongozo, na Oktoba 29, mwaka huu alijibu kuwa ni lazima
wawasiliane na upande wa pili wa wadau walioingia mikataba ili kulinda maslahi ya kibiashara na kuwa watu hao waridhie mikataba hiyo kwenda kwa kamati. Alisema Oktoba 28 walimwandikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kuomba ridhaa ya kutoa taarifa za mapitio ya mikataba 26 ya gesi. Andilile alisema kutokana na muda waliopewa kuwa finyu, TPDC ilimuandikia Katibu wa Bunge kumwomba waongezewe muda wa kutekeleza agizo la kamati, lakini Ijumaa saa 10 jioni walipokea barua ya
Bunge inayowataka kuhakikisha
wanatekeleza agizo hilo ifikapo jana saa nne asubuhi, barua ambayo ilijibiwa na TPDC Oktoba 31 mwaka huu.
“Nia ya TPDC ni kutii sheria na mamlaka, lengo la kuomba mwanasheria mkuu ilikuwa ni kujiridhisha kabla ya kutoa mikataba hiyo ili kuiepusha Serikali isiingie kwenye kesi ambazo zinaweza kuigharimu,” alisema. Naye Mwanda aliyeulizwa kwanini wameshindwa kupeleka mikataba na taarifa, alisema anakubaliana na maelezo ya mkurugenzi na kuwa sheria inawabana wao kutekeleza agizo hilo na kuwa si lengo lao kukataa na kushindwa kutekeleza sheria na mamlaka zilizopo.
Aidha, akinukuu Barua kutoka kwa Mwanasheria Mkuu inayotaka mikataba ya biashara kama ilivyo ya uzalishaji na ugawaji wa mapato inatakiwa kuhakikishwa maslahi ya kibiashara yanalindwa. Kutokana na kauli hiyo ndipo mwenyekiti wa kamati hiyo, Kabwe Zitto alihoji maslahi ya
wananchi yanalindwa na nani katika
mikataba hiyo. Mbunge huyo alimtaka Andilile kutoa mfano mmoja wa mkataba ambao umeigharimu
Serikali kwa mkataba kupelekwa kwenye kamati ya bunge, jambo ambalo mkurugenzi huyo alishindwa kulitolea ushahidi. Alisema mikataba hiyo ambayo inaonekana kuwa na usiri hapa nchini, imekuwa wazi kwenye nchi zinazotoka makampuni hayo na
kuwa baadhi yao imeweka wazi mikataba hiyo kwenye soko la hisa ikiwemo kampuni ya Swala.
“Ni kilio cha muda mrefu cha usiri wa
mikataba na sisi tunaamini bunge au kamati zake, ina mamlaka ya kufahamu kile ambacho Serikali imeingia kwa niaba ya wananchi ili kuona maeneo ambayo mikataba ni mibovu irekebishwe,” alisema. Zitto alitolea baadhi ya hoja zilizoainishwa
na Mdhibiti na Mkaguzi wa Fedha za Serikali (CAG) ni Pan African Energy ambapo mkataba wa awali ilitaka wapate asilimia 20 na Serikali asilimia 80 lakini sasa mgawo ni asilimi 55 wao na 48 ni za Serikali. Pia kampuni ya Statol ambayo mkataba ilikuwa wao wapate asilimia 20 na serikali asilimia 80, lakini mkataba wa sasa mgawo
ni asilimia 50-50. Muhongo aishangaa PAC Naye Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amelalamikia kitendo cha viongozi hao
kukamatwa na kusema kuwa ni kinyume na sheria kwani kamati hiyo haina mamlaka ya kuagiza kukamatwa watumishi hao. “Kuna mihimili mitatu ya Serikali, Mahakama, Serikali na Bunge. Ni suala la kusikitisha na la ajabu kwa muhimili mmoja kufanya kazi za muhimili mwingine. Kamati haina mamlaka ya kuagiza kitu kama hicho,” alisema kwa njia ya simu. Aidha, Muhongo amesisitiza kuwa hakuna namna yoyote kwa mikataba inayotakiwa na kamati hiyo kuwekwa wazi. Alisema PAC imekuwa na ajenda ya siri na kwamba hatua ya kukamatwa kwa viongozi hao inatakiwa kulaaniwa kwa nguvu zote.
“Kwa tukio kama hili, ni dhahiri kuwa
wawekezaji watakimbia.Hatuwezi kuacha hali kama hii kuendelea kama ilivyo,” alibainisha. Muhongo aliongeza kuwa amewasiliana na Spika wa Bunge, Anne Anne Makinda kuhusu
suala hilo na amemhakikishia kuwa
kilichofanywa na kamati hiyo ya bunge ni ‘kinyume na sheria na hakikubaliki’.
Kauli ya Muhongo imethibitishwa pia na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam baada ya kuwaachia Mwande na Andilile bila masharti kwa kuwa kukamatwa kwao kumetajwa hakukufuata utaratibu unaotakiwa, ambao ni kupata kibali cha Spika wa Bunge.
Kufikia jana jioni Andilile alirejea ofisini
kwake kuendelea na majukumu ndani ya taasisi nyeti ya TPDC. Hakuwa tayari kuzungumzia lolote juu ya tukio la kukamatwa kwao.

0 comments:

Post a Comment