Dar es Salaam. Wakati maofisa wa Serikali za Tanzania
na China wakipuuza tuhuma zinazohusisha ziara ya Rais wa China, Xi
Jinping na utoroshaji wa meno ya tembo, ripoti hiyo imeanika madudu
mengi ikionyesha jinsi nyara hizo zinavyotoroshwa nchini.
Juzi taasisi iitwayo Environmental Investigation
Agency (Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira– EIA) ilitoa hadharani ripoti
ambayo inataja maofisa na wanausalama wa China kwamba walitumia fursa ya kidiplomasia kusafirisha meno ya tembo kwa ndege ya Rais Jinping ambaye alitembelea Tanzania Machi 2013.
Ikulu ya Dar es Salaam na Ofisi ya Mambo ya Nje ya
China kwa nyakati tofauti zilisema taarifa hizi siyo za kweli na jana
Serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, ilitoa taarifa bungeni na kuziita taarifa hizo kuwa ni za
“kupikwa”.
Wakati hayo yakiendelea, ripoti hiyo ya EIA iliyopewa jina la Vanishing Point: Criminality, Corruption
and Devastation of Tanzania’s Elephants (Hatua ya kutoweka: Uhalifu,
Rushwa na Kuangamizwa kwa tembo wa Tanzania), inafichua madudu zaidi
yanayoweka bayana jinsi uhalifu wa utoroshaji wa meno ya tembo
unavyofanyika.
Ripoti hiyo inalitaja pori la akiba la Selous kuwa
kituo cha mauaji ya tembo, kwani matukio ya ujangili hupangwa katika
vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo, kisha kutekelezwa kwa msaada wa
polisi na baadhi ya wananchi.
Inavitaja vijiji vilivyopo katika maeneo ya Mloka,
Tunduru, Namtumbo, Liwale na Kilwa ambako wafanyabiashara wadogo kutoka
Dar es Salaam hukodishwa silaha na wawindaji, kisha kuingia katika
hifadhi hiyo na kufanya uhalifu.
“Wakati mwingine wawindaji kutoka nje ya eneo hilo
hutumiwa na baadhi ya maofisa kutoka serikalini,” inasomeka sehemu ya
ripoti hiyo.
Katika tukio la aina yake, ripoti hiyo imeeleza
tukio la katikati ya mwaka huu ambapo kundi la wawindaji kutoka Arusha
lilitumwa na maofisa wa polisi waliokuwa Mloka na kuingia katika hifadhi
hiyo kwa ajili ya kuwinda.
Inadaiwa kuwa maofisa hao wa polisi walitoa silaha
kwa kundi hilo la wawindaji na baada tu ya mauaji ya tembo wapatao
watano walichukua meno kutoka kwa wawindaji.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tembo akishauawa, meno
yake hukatwa kisha kufukiwa hadi pale mnunuzi anapowasili ambapo
hufukuliwa na kupewa.
EIA katika ripoti hiyo inabainisha kuwa meno mengi
ya tembo kutoka Selous husafirishwa kwenda Dar es Salaam, ama kwa
kutumia barabara kwa maana ya magari ambayo yametengezwa maalumu kwa
ajili ya kazi hiyo, au kwa kupitia majini wakitumia mitumbwi ya asili.
“Wakati mwingine pikipiki hutumika kupitia njia za
vichakani kukusanya meno hayo kule ambako zimefichwa hadi kufikia
barabara kuu,” inasema sehemu ya ripoti hiyo. Kutoka kwenye njia kuu
husafirishwa kwa magari binafsi ambayo yanakuwa sehemu maalumu kwa ajili
ya kuficha pembe hizo au kupitia mabasi ambayo husafirisha meno ya
tembo zaidi kuliko abiria kutokana na malipo makubwa ambayo hutolewa kwa
kazi hiyo.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa: “Kwa kawaida meno ya tembo mabichi
yanapofikishwa jijini Dar es Salaam kutoka Kusini huwekwa katika mafungu
madogo na kuhifadhiwa katika baadhi ya maeneo kwenye vitongoji vya jiji
hilo. Pindi anapotokea mteja anahitaji kununua hukusanywa na kuuziwa”.
Inaelezwa kuwa kawaida hifadhi hizo huwa katika
maeneo ya viwanda kama vile Chang’ombe karibu na bandari, lakini pia
wakati mwingine katika viwanja vilivyopo mbali na makazi ya watu.
Selous hatarini
Kutokana na hali hiyo, ripoti hiyo inasema Hifadhi
ya Selous ipo katika hatari ya kupoteza hadhi yake kutokana na
kukithiri kwa matukio ya ujangili, huku Serikali ikionekana kwamba
haijali.
Ripoti hiyo inadai kuwa hifadhi kongwe yenye
maeneo makubwa yapatayo kilomita za mraba 50,000 haina ulinzi wa kutosha
hali inayotoa mianya kwa makundi ya uhalifu wa wanyamapori kufanya
vitendo hivyo.
EIA inasema idadi ya tembo katika Hifadhi ya
Selous imeshuka kutoka 70,406 mwaka 2006 hadi kufikia 13,084 mwaka 2013.
Hiyo ikimaanisha kwamba idadi ya tembo 57,322 wameuawa katika kipindi
cha miaka saba.
Mauaji hayo yamethibitishwa kwa kipimo cha
vinasaba (DNA) na kubainisha kuwa asilimia kubwa ya mauaji ya tembo
yanahusishwa na ukataji wa pembe za ndovu.
Kwa mujibu wa EIA mwaka 2000 tayari kulikuwa na
ishara za wazi zilizoonyesha kuwapo kwa mauaji ya tembo na kwamba baadhi
ya vyombo vya habari
viliripoti juu ya hali hiyo hasa baada ya mizoga ya tembo kuonekana
ikiwa imezagaa katika hifadhi ya Selous. “Lakini, mkurugenzi wa
wanyamapori alipoulizwa kuhusiana na hali hilo, alisema kuwa matukio ya
ujangili yapo chini,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo yenye kurasa 36.
Inaendelea kueleza kuwa, mwaka 2010, EIA
walitembelea eneo la Selous na kufanya mahojiano na wanakijiji ambao
walifichua siri juu ya maeneo yanayotumika kufanyia biashara haramu ya meno ya tembo.
Njia za magendo zinazotumika kusafirisha meno hayo
zinawahusisha polisi na askari wanyamapori ambao taarifa hiyo inawataja
kwamba wao ndio waliopaswa kuwa mstari wa mbele kulinda hifadhi hizo,
hali inayoifanya EIA kuitupia lawama Serikali ya Tanzania.
“Licha ya ishara hizi za wazi, Serikali ya
Tanzania imeshindwa kupambana na ujangili katika Hifadhi za Selous.
Zaidi ya tembo 25,000 waliuawa kati ya mwaka 2010 na mwaka 2013. Sababu
kuu iliyosababisha vifo vya tembo hao ni ujangili.
“Mwaka 2011, theluthi mbili ya mizoga ilionekana
katika Hifadhi ya Selous. Sababu inayochangia ni ukosefu wa rasilimali
kwa ajili ya kulinda hifadhi kwa umakini,” inasomeka sehemu ripoti hiyo.
0 comments:
Post a Comment