pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

Ukosefu wa makazi unachochea hatari ya kupata magonjwa ya akili


Iwapo unaishi ndani ya nyumba yenye ua mzuri, kuta, paa na vitanda vizuri lakini bado unapata maradhi, je? Wanaishije wale waliokosa makazi kabisa?
Wale ambao wanalala katika vibaraza, shuka zao ni maboksi, wanakula kwenye majaa na wanakunywa maji yoyote wanayoyapata na kujisaidia popote.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha kuwa ukosefu wa makazi unasababisha maradhi  hasa ya kuambukiza kama kifua kikuu, nimonia, kuhara na ukimwi   kutokana na mazingira duni. Si hivyo tu, bali watu wasio na  makazi hukosa huduma za afya hivyo kuhifadhi mzigo wa maradhi.
 Watu wasio na makazi pia wapo hatarini zaidi kupata magonjwa ya akili.  Utafiti wa mwaka 2010 uliochapishwa katika Jarida la Development Southern Africa, ulibaini kuwa asilimia 50 ya watu wasio na makazi wanaugua magonjwa ya akili.
Kwa mfano, Noah Mjengwa anayeishi katika mitaa na kulala katika vibaraza vya Kariakoo anasema alitoka mkoani Mbeya na kuja Dar es Salaam kutafuta maisha, lakini amekutana na ugumu zaidi wa maisha uliomfanya aishi kama kunguru.
“Nilidhani itakuwa rahisi kupata riziki lakini kumbe nilikutana na ugumu wa kuzimudu gharama za maisha, kila kitu nanunua,”anasema
Mjengwa akiwa amejikunyata kwa kuweka mikono ndani ya fulana yake kuukuu, anasema  hana anuani maalumu ya pale anapoishi.  Nyakati za mchana atatembea, huku na kule akibahatisha mtu wa kumbebea mzigo. Usiku unapofika atatafuta kibaraza na kulala juu ya maboksi na wakati mwingine chini. Mbu huwa ni chakula chake cha usiku na baridi inamkomesha pia.
Huku mdomo wake ukionyesha dhahiri kubadilika rangi na kuwa mweusi kutokana na uvutaji wa sigara, Mjengwa anaendelea kuvuta kipisi cha sigara ambacho kimerushwa na mwanaume aliyepita barabarani hapo dakika chache zilizopita.
Tabia hizi ndizo zinazomfanya Mjengwa kuwa katika hatari ya kupata maradhi kama ya Kifua Kikuu. “zamani nilikuwa sivuti wala situmii kilevi cha aina yoyote, lakini tangu nianze maisha haya mapya huku Kariakoo nimejifunza kuvuta. Ni lazima nipate kitu cha kunichangamsha,” anasema.
Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Johannesburg, umeonyesha kuwa ukosefu wa makazi na magonjwa ya akili vinahusiana. Watafiti hao walibaini kuwa ingawa magonjwa ya akili yanasababisha na kuchangia mtu kukosa makazi, lakini kuishi mitaani kunachangia kwa kiasi kikubwa kupata maradhi.
WHO ilifanya utafiti  katika nchi zinazoendelea  na ilibainika kuwa asilimia 45 ya watoto na 48 ya watu wazima  wanaoishi mitaani, walipata msongo wa mawazo uliochangia asilimia tatu ya watu hao kupata magonjwa ya akili.
Wataalamu wa afya wanasema kuwa mtu anapokosa makazi  hawezi kuzingatia mlo kamili, chakula kisafi au hata kuandaa chakula katika hali ya usalama. Hiki ndicho kinachochoea zaidi watu wasio na makazi kupata maradhi
Mtaalamu wa Afya ya Mazingira, Mtwara, Dk Henricko Makibisa, anasema  hata inapotoea mafuriko watu wakakosa makazi, ni rahisi zaidi  magonjwa ya mlipuko kama kuhara na malaria vikalipuka pia.
“Ukosefu wa makazi ni chanzo cha magonjwa kama malaria. Unakuwa chakula cha mbu kwa sababu huna neti, unapata wapi maji yaliyochemshwa na unakula wapi chakula salama?” anahoji Dk Makibisa.
Nakutana tena na mtoto wa miaka 13 anayejitambulisha kwa jina la Suma Lee. Yeye anaishi  ndani ya eneo la kibiashara la Kariakoo, mtaa wa Swahili ndipo malazi yake yalipo.
“Naweza kukaa hata siku mbili sijaoga kwa sababu kuoga hadi nilipie Sh300. Lakini  siku nikiombaomba na kupata pesa, naenda kuoga kwenye bafu la kulipia au Mto Msimbazi,” anasema
Hali hiki ndicho chanzo cha maradhi, kwani wataalamu wa afya katika Jarida la Modern Health la Afrika Kusini wanasema kuwa  kuoga ni dawa inayowezesha kustarehesha misuli, kupunguza maumivu ya kichwa, kupunguza maumivu ya tumbo la hedhi, kuondoa sumu mwilini na kusawazisha mfumo wa tezi za limfu.
Hivyo, mtu asipooga anahifadhi msongo wa mawazo, maumivu na sumu  mwilini. Mtu huyo akiendelea kuishi bila kuliona bafu kwa siku nyingi si ajabu akapata homa kali au hata uchovu uliokithiri.
 Msongo wa mawazo nao unatajwa kusababisha magonjwa ya akili kwa asilimia kubwa kwa wale wasio kuwa na makazi.
Lakini  ukosefu wa makazi, tatizo linalowakabili watoto wengi, huchangia kujiingiza katika makundi mabaya ambako hujifunza uvutaji wa sigara,  bangi na hata pombe.
 Kama ilivyo kwa Suma Lee ambaye akiwa na miaka 12 tu, tayari ameshaanza kuvuta petroli ambayo anadai inamsaidia kupata  faraja na kumchangamsha.
Chuo Kikuu cha Kwa Zulu Natal kilifanya utafiti mwingine mwaka 2012 na kugundua kuwa watu wasio na makazi ni rahisi kufanyiwa ukatili.
Kama ilivyo kwa watu wenye ulemavu,  aghalabu huwa maskini  hali kadhalika ni rahisi kwa mtu asiye na kipato na aliyekosa makazi kupata magonjwa na kunyanyaswa.

0 comments:

Post a Comment