GUMZO la wiki hii katika michezo ni picha ya beki wa Ruvu Shooting,
George Michael akimkaba kwa nguvu zake zote mshambuliaji wa Yanga, Amissi
Tambwe raia wa Burundi.
Picha pekee mali ya gazeti hili, inaonyesha Tambwe akitokwa damu
mdomoni wakati Michael akimkaba kwa nguvu bila ya huruma.
Muonekano wa picha hiyo umeonyesha kuwashitua wadau wengi wa soka
kama ambavyo iliwashitua wahariri wa gazeti hili kwa mara ya kwanza walipoiona.
Haionyeshi uungwana, haionyeshi kama soka ni mchezo, inaonyesha soka
ni vita au mchezo wa chuki na kulenga kuumizana.
Rekodi zinaonyesha katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara kati ya Simba
dhidi ya Ruvu Shooting msimu uliopita, Tambwe alifunga mabao matatu.
Maana yake hii ni mara ya tatu Tambwe anakutana na Ruvu Shooting
hakufunga bao. Inawezekana Michael alifanikiwa kumzuia, lakini njia alizotumia,
hakika si sahihi kimchezo.
Baada ya picha hiyo kutumiwa na Gazeti la Championi Jumatatu,
mjadala mkubwa ulizuka katika vijiwe, kwa viongozi wa soka na wadau wengine
mbalimbali. Wengi wamekuwa wakipinga.
Kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kama Facebook na Instagram
kulikuwa na gumzo kubwa ingawa wako walitanguliza ushabiki wakidai hata
wachezaji wa Ruvu Shooting waliumizwa siku hiyo.
Kwenye matangazo ya vipindi vya michezo hasa juzi, gumzo la picha
hiyo lilikuwa kubwa zaidi na ilifikia hadi Mwenyekiti wa Chama cha Wanasoka
Tanzania (Sputanza), Mussa Kisoki kukemea tukio hilo akisisitiza Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) wanapaswa kuchukua hatua.
Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, kama ilivyo kawaida yake,
alizungumza mengi kuhusu suala hilo, lakini mara nyingi alijikanganya.
Mfano, alisema hofu yake picha hizo zilikuwa ni za kutengenezwa,
hasa alipozungumza na Redio ya E FM, alipozungumza na Redio One Stereo, akasema
picha anazikubali, lakini anataka ushahidi wa video, halikadhalika Clouds FC,
alisema hivyo.
Picha hiyo bora katika michezo tokea kuanza mwaka 2015, inatufunza
mengi sana wadau wa soka na tukikubali, tutapiga hatua.
Moja:
Watanzania wengi hasa wadau wa soka si watu wa kukubali makosa.
Mfano Masau ambaye anadiriki kusema picha hiyo ni ya kutengenezwa au vipi
wachezaji wake nao walipigwa lakini haikuonekana.
Picha zilizopigwa ni nyingi, hiyo ni kati ya iliyoaminika ni bora zaidi
na hilo limedhihirika. Championi ndilo gazeti bora zaidi la michezo nchini na
linasomwa na watu wengi zaidi kuliko jingine kwa sasa, halina sababu ya kuweka
vitu vya kutengeneza kwa nia ya kupotosha.
Masau ni kati ya wadau wetu, tunajua hakosi Championi na hata
amewahi kufika kwenye chumba chetu cha habari kututembelea na kuona tunafanyaje
kazi zetu.
Hivyo, kwa mara nyingine tunamkaribisha ili aje kuiona picha hiyo
naye awe huru kuthibitisha na kuiambia jamii kama kweli iligushiwa au la, sisi
tunachoweza kuthibitisha, picha hiyo ni sahihi na ilipigwa kwa ubora wa juu na
ndiyo kiwango cha Championi.
Pili:
Ushabiki usiokuwa na msingi, wako ambao waliendelea kusema kwa kuwa
Tambwe yuko Yanga, ndiyo maana Championi wametoa.
Si sahihi, Championi halina itikadi. Hata kama wafanyakazi wake wana
timu zao, lakini hawauweki kwenye kazi.
Siku chache zilizopita, tulitoa picha za mwamuzi akipigwa huku
anakimbizwa. Siku chache baadaye Mwanaspoti nao wakafuatia na kuendelea
kudhibitisha ubaya wa kupiga waamuzi kama tulivyoanza.
Kwanza niwapongeze Mwanaspoti kwa kutuunga mkono kulaani vitendo
hivyo vibaya vya kupiga uamuzi lakini ni sehemu ya uthibitisho kwa hatuungi
mkono mtu kuonewa bila ya kujali anatokea timu ipi. Championi ni lako wewe
msomaji.
Tatu:
Watu wa michezo hatupendani, hili limethibitishwa kuanzia uwanjani
wakati Michael akimkaba Tambwe hadi kwa viongozi na wadau.
Aliyemkaba vile Tambwe unafikiri ana ndoto ya kucheza zaidi ya Ligi
Kuu Bara? Wapi atacheza zaidi ya hapa Tanzania aachiwe kufanya alichokifanya?
Kumfanyia vile Tambwe ni kuonyesha chuki, hakuna upendo.
Kiongozi kama Masau kutetea ni sehemu nyingi ya kuonyesha kiongozi
anaweza kumtetea hata anayelenga kuua au kuumiza akisahau kesho pia inaweza
kumtokea mchezaji wake.
Mashabiki, wanaangalia tu Tambwe anachezea wapi, hawajali aliumizwa
vipi! Wakati akiwa Simba, Championi liliwahi kuandika pia akilalamika kuhusu
beki huyo ambaye alipewa jina la ‘beki katili’.
Nne:
Waamuzi nao wana tatizo, siku kadhaa zimepita tumepiga kelele
kuhusiana nao kupigwa kila wakati ambalo si jambo sahihi.
Wakati tunawatetea kuna kila sababu ya kuwa imara zaidi na kufanya
kazi yao kwa ufasaha. Mechi kati ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting ilikuwa na
taswira ya mechi ya ndondo.
Aliyesababisha ifikie pale ni mwamuzi Mohamed Teofili kutoka
Morogoro na huenda alikuwa mwoga kwa kuwa anachezesha timu ya jeshi ambao wana
sifa za kupiga waamuzi kama ngoma kipindi hiki.
Teofili hakuwa sahihi kwa kuwa hakupaswa kuwa mwoga. Anatakiwa kufuata
sheria 17 za soka na kutenda haki.
Waamuzi wanatakiwa kuwa imara na kufanya kazi yao kwa ufasaha,
kuchekacheka kama alivyofanya Teofili hakuwezi kuwa suluhisho.
Mwamuzi anapokuwa makini, lazima mchezo unakwenda vizuri. Bila ya
kujali mchezaji wa Yanga au Ruvu Shooting ndiye aliyekosea. Mwamuzi alitakiwa
kutokuwa mwoga na kuchukua hatua kwa wakosefu.
SOURCE: CHAMPIONI
0 comments:
Post a Comment