
Kenya inatazamiwa kuanza kuuza mafuta ghafi ya petroli katika soko
la kimataifa mwaka ujao na hivyo kuitangualia nchi jirani ya Uganda
ambayo iligundua bidhaa hiyo miaka tisa iliyopita.
Ripoti zinasema kuwa shirika la uchimbaji mafuta na gesi la
Uingereza, Tullow linatekeleza mkakati wa kuanza kuzalisha mafuta ya
petroli katika eneo la Lokichar kaskazini mwa Kenya. Awali shirika hilo
lilikuwa limesema lingeanza kuuza nje mafuta ya Kenya mwaka 2018 lakini
sasa limezidisha kasi ya uchimbaji wa mafuta na hivyo kutoa msukumo
mkubwa wa uchumi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Shirika la Tullow
limesema linataraji bomba kutoka Lokichar hadi bandarini eneo la pwani
litakuwa tayari ili kuwezesha mafuta ghafi ya Kenya kufika katika soko
la kimataifa kabla ya kumalizika mwaka 2016. Inatazamiwa kuwa Kenya
itaanza kwa kuuza mapipa laki moja ya mafuta ghafi ya petroli ya siku.
Kwa bei ya sasa ya dola 50 kwa pipa, nchi hiyo inaweza kupata pato la
takribani dola bilioni 1.825 au shilingi bilioni 166 kwa mwaka. Kuanza
kuzalishwa mafuta ya Petroli mwisho wa mwaka 2016 kutasadifiana na
wakati ambao Wakenya watakuwa wakijirayarisha kwa uchaguzi wa mwaka 2017
na hivyo mafanikio hayo yanatazamiwa kupigiwa debe na serikali ya
Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.
0 comments:
Post a Comment