Gazeti la The Guardian
linalochapishwa nchini Uingereza limeandika katika toleo lake la
karibuni kuwa askari wa Ufaransa waliotumwa Jamhuri ya Afrika ya Kati
waliwabaka na kuwalawiti watoto wadogo wa kiume katika mji mkuu wa nchi
hiyo Bangui. Kwa mujibu wa gazeti hilo, katika kipindi cha kati ya
Disemba mwaka 2013 hadi Juni 2014 wakati wa operesheni ya kijeshi katika
mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, askari wa Ufaransa waliokuwa
wametumwa nchini humo waliwafanyia vitendo vichafu vya kuwabaka na
kuwalawiti watoto wadogo wa kiume wenye umri hata wa miaka tisa ili
kuwagaia pesa na chakula. Ripoti hiyo imefichuliwa na afisa mwandamizi
wa Umoja wa Mataifa anayehusika na misaada ya kibinadamu, katika
kulalamikia kimya cha umoja huo na kushindwa kuwafuatilia na
kuwachukulia hatua kisheria askari hao waliofanya unyama huo. Anders
Kompass, ambaye amefichua kadhia hiyo kwa kuwapatia taarifa maafisa wa
serikali ya Ufaransa amesimamishwa kazi kwa madai ya kuvujisha ripoti za
siri za Umoja wa Mataifa na kukiuka itifaki. Kwa mujibu wa ripoti hiyo
askari wa Ufaransa waliwalaiti watoto hao wa kiume ambao baadhi yao ni
mayatima waliokuwa wamepewa hifadhi kwenye kituo cha watu waliopoteza
makaazi yao katika uwanja wa ndege wa M’Poko mjini Bangui.
Uingiliaji rasmi na usio na kificho wa
kijeshi wa Ufaransa katika nchi za Kiafrika ambazo nyingi zao zilikuwa
makoloni ya nchi hiyo umeshuhudiwa kwa uwazi zaidi katika miongo kadhaa
ya karibuni, ambapo kwa kutumia kisingizio cha kutoa msaada na kurejesha
amani na utulivu, Paris imekuwa ikituma askari wake katika nchi hizo
ambazo nyingi zao zimeonekana kukumbwa na migogoro ikiwemo Ivory Coast,
Libya, Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Tangu mwezi Machi mwaka 2013
wakati aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize
alipoondolewa madarakani na waasi wa zamani wa Seleka waliokuwa
wakiongozwa na Michel Djotodia, nchi hiyo imegubikwa na wingu la
mapigano na machafuko yaliyosababisha raia wengi kuuawa au kukimbilia
nchi nyengine na kuishi maisha ya ukimbizi. Wakati mapigano na machafuko
yaliposhtadi, Umoja wa Mataifa uliruhusu vikosi vya askri wa kigeni
kuingilia kati mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, na ndipo Ufaransa
ilipotumia fursa hiyo kutuma askari wake nchini humo. Rais Francois
Hollande wa Ufaransa aliongeza idadi ya askari wa nchi hiyo huko Jamhuri
ya Afrika ya Kati kwa kisingizio cha kulinda maisha ya raia. Lakini kwa
mtazamo wa wachambuzi wa mambo Ufaransa haikujiingiza kijeshi Jamhuri
ya Afrika ya Kati ili kuokoa maisha yaliyokuwa hatarini ya raia wa nchi
hiyo bali ilifanya hivyo kulinda satua yake katika eneo hilo la bara la
Afrika na kupora utajiri wake mkubwa wa maliaasili. Lakini si hayo tu
kuwepo kwa askari wa Ufaransa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati
kumeandamana na tuhuma kadha wa kadha ambazo wamehusishwa nazo askari
hao zikiwemo za ripoti iliyofichuliwa hivi karibuni ya kuhusika kwao na
vitendo vya kuwabaka na kuwalawiti watoto wadogo wa kiume katika nchi
hiyo. Hivi sasa kuna askari wapatao elfu moja wa Ufaransa nchini Jamhuri
ya Afrika ya Kati, na bila ya shaka kufichuliwa kwa kashfa hiyo
kutawaweka askari hao kwenye mazingira magumu ya kuendelea na
utekelezaji wa kazi waliyotumwa nchini humo. Kufuatia kufichuliwa ripoti
hiyo, Wizara za Ulinzi na Sheria za Ufaransa zimetangaza kuwa
zimeanzisha uchunguzi juu ya suala hilo. Taarifa iliyotolewa na Wizara
ya Ulinzi imesisitiza kuwa itachukua hatua zote zinazohitajika ili
kuhakikisha ukweli kuhusiana na tuhuma hizo unajulikana. Hayo yanajiri
wakati siku chache zilizopita Rais Francois Hollande wa Ufaransa
alitangaza kuwa ili kukabiliana na vitisho vya usalama, bajeti ya ulinzi
ya nchi hiyo itaongezwa kwa kiwango cha yuro bilioni nne. Aidha alisema
askari elfu saba wa nchi hiyo wanaofanya kazi za ulinzi katika maeneo
nyeti na muhimu wataendelea kuhudumu katika maeneo hayo. Imeelezwa kuwa
kudhamini usalama wa askari wa Ufaransa walioko katika nchi za Afrika ni
miongoni mwa malengo na sababu za kuongezwa bajeti ya ulinzi ya nchi
hiyo. Pamoja na yote hayo wataalamu wa mambo wanaeleza kuwa endapo
ukweli juu ya vitendo vya kuwatumia vibaya kijinsia watoto wadogo nchini
Jamhuri ya Afrika ya Kati utathibitika, kashfa hiyo itaongeza idadi ya
changamoto zinazoikabili Ufaransa pamoja na serikali ya Hollande…/
0 comments:
Post a Comment