UNYAMA wa
kutisha! Bwana mmoja ambaye ni imamu, aliyefahamika kwa jina la Mustafa
Omar Mustafa, mkazi wa Ghana, Kata ya Nyamanoro jijini Mwanza,
amefanyiwa unyama wa hali ya juu kwa kumwagiwa tindikili na watu
wanaosadikiwa kuwa ni waumini wenzake, kisa kulinda mali za msikiti wao
uliopo katika mtaa huo wa Ghana. Uwazi linakupa habari kamili.
Mustafa Omar Mustafa, anayedaiwa kumwagiwa tindikali.
ILIKUAJE?
Akizungumza na mwandishi wetu kwa masikitiko Mustafa
alisema kuwa, tukio hilo la kinyama alifanyiwa majira ya saa mbili
kasorobo usiku, Jumapili ya Agosti 31, mwaka jana akiwa nyumbani kwake
Ghana.
“Nilikuwa katika hali ya furaha na familia yangu, sikuhisi kabisa hatari
ambayo ilikuwa inakuja kutokea katika maisha yangu. Tukiwa hatuna hili
wala lile, tulishitukia kundi la watu likivamia nyumba yangu ndipo
waliponitendea unyama huu na kutoweka,” alisema.
AKIMBIZWA HOSPITALI YA MKOA SEKOU-TOURE
“Baada ya unyama huo familia
yangu na jamaa wa karibu kwa haraka walinikimbiza katika kituo kidogo
cha polisi cha kata hiyo ambapo nilipata kibali cha matibabu (PF3) na
kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou-toure, ambapo
nilipokelewa na kuingizwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.“Katika
chumba hicho nilikaa kwa muda wa siku sita nikahamishiwa katika chumba
cha wodi za kawaida.”
Mustafa akionyesha jeraha alilolipata mkononi.
MATIBABU YASHINDIKANA AHAMISHIWA CCBRT
“Baada ya hali yangu kuzidi
kuwa mbaya, madaktari wa hospitali hiyo walinishauri kufanya utaratibu
wa kwenda kupata matibabu zaidi katika Hospitali ya CCBRT Dar ambayo
inasifika kwa kutoa huduma nzuri ya matibabu ya macho.
“Kama unavyoona sehemu kubwa niliyoathirika na tindikali ni usoni,
kifuani na mgongoni! Mwanzoni kabisa macho yote hayakuwa yanaona ndipo
nilipohamia CCBRT, ambapo angalau nimeweza kupata matibabu, namshukuru
Mungu sasa jicho moja la kulia linaweza kuona kwa mbali.
KISA CHA KUMWAGIWA TINDIKALI
“Kabla ya tukio hilo katika msikiti wetu kulikuwa na mgogoro kati ya waumini na viongozi wa msikiti.
Hatukuwa
tunawataka ambapo baada ya mvutano wa muda mrefu uliosababisha
kufikishwa mahakamani baadhi ya watu, uchaguzi wa viongozi wengine
ulifanyika chini ya uangalizi maalumu wa mahakama, baada ya kupatikana
viongozi wapya nilipendekezwa kuwa imamu na nikawa naongoza sala za
asubuhi.
Jeraha la kifuani.
“Kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele, nilianza kujihusisha na shughuli
mbalimbali za msikiti ikiwemo kufanya usafi wa mazingira na kutunza
baadhi ya rasilimali jambo ambalo lilionekana kutolifurahisha kundi la
baadhi ya watu ambao hawakuwa wanaupenda huo uongozi mpya, ambapo kwa
kile walichokiita kunikomesha ndipo walipoamua kunimwagia tindikali.
MSAADA
“Kutokana na hali mbaya ya kiuchumi niliyonayo, nawaomba
Watanzania watakaoguswa na matatizo yangu kunisaidia ili niweze kupata
huduma ya matibabu zaidi kwani hali yangu kiuchumi kwa sasa ni mbaya
sana.
“Nawashukuru sana wote ambao wamenisaidia mpaka angalau nimekuwa katika
hali hii, japo hali yangu bado haijawa vizuri sana hasa kimaisha, maana
nimeshatumia fedha zangu zote kwa ajili ya matibabu na leo hii nafikia
hatua ya kuomba kwa kuwa familia inanitegemea na haina namna tena, mtaji
wangu wote umeishia katika matibabu.
“Kabla ya kufanyiwa unyama huu nilikuwa wakala wa mitandao ya simu na
sasa changamoto yangu kubwa ni hali ya hewa ya jijini Dar es Salaam kuwa
ya joto sana, hivyo napata maumivu sana kwenye majeraha yangu.
Jeraha la mgongoni.
MACHO
“Hivi sasa matibabu ya macho bado yanaendelea ingawa
nimeambiwa nirudi tena mwezi ujao (Juni) ambapo nimepewa uhamisho kwenda
katika Hospitali ya Ocean Road kwa ajili ya kushughulikia tatizo la
ngozi ambayo nayo imeharibika vibaya.
“Nilikwenda katika hospitali hiyo nikaambiwa kumuona daktari tu,
natakiwa kutoa shilingi elfu hamsini, kiasi ambacho kwa sasa ni kikubwa
sana kwangu maana nakosa hata shilingi mia mfukoni.“Ninayoyasema hapa ni
rahisi kwa asiye jua hali yangu kuona kama natania ila ukweli ni kwamba
hata fedha ya kwenda hospitali kumuona huyo daktari sina.
“Nawaomba Watanzania wanisaidie ili niweze kumuona daktari kisha nipate
nauli ya kurudi Mwanza kukaa na familia yangu japokuwa siwezi
kuihudumia. Changamoto ni kwamba baada ya mwezi natakiwa kurudi Dar kwa
matibabu ya macho na ngozi.
“Nampongeza sana Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Global Publishers
Ltd, Eric Shigongo kwa kuwa nami bega kwa bega tangu nipate tatizo hili
na hakika yeye ni mtu mwenye upendo wa dhati, pia nawashukuru wote ambao
wanaendelea kunijulia hali,” alisema Mustafa huku akilengwalengwa na
machozi.
Aliyeguswa na habari hii awasiliane naye kwa namba 0752 362 221, kutoa ni moyo.
0 comments:
Post a Comment