NDEGE mpya ya kwanza iliyonunuliwa na serikali kwa ajili ya kutumiwa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), imetua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA), ikitokea nchini Canada ilikotengenezwa.
Ndege hiyo ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere majira ya saa 6:15 mchana jana. Baada ya kutua ndege hiyo, ilipatiwa heshima maalumu ambayo hutolewa kwa ndege yoyote mpya inayotua katika nchi yake (Water Salute) na kisha kuegeshwa katika eneo la ndege za jeshi (Airwing Ukonga).
Akizungumza baada ya kuwasili kwa ndege hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Leonard Chamriho alisema ndege ya pili inatarajiwa kuwasili baada ya wiki moja.
“Baada ya kuwasili ndege ya pili ndipo yatafanyika mapokezi rasmi, yatakayoongozwa na Rais Magufuli kwa tarehe itakayotangazwa baadaye,” alisema Chamriho.
Taarifa ya awali iliyotolewa na ATCL mwishoni mwa wiki, ilieleza kuwa ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 76 ikiwa na marubani wanne kutoka Canada, ilianza safari ya kuja nchini tangu wiki mbili zilizopita ikipitia miji ya Reykjavík, Southampton, Malta, Luxor na Addis Ababa Ethiopia. Ilieleza kuwa ndege hizo, zitaanza kufanya safari zake mara tu baada ya kukamilisha mchakato wa kusajiliwa na Mamlaka ya Usalama wa Anga Tanzania (TCAA).
“Kwa kuwa zitakuja zikiwa na usajili wa nchini Canada, tutalazimika kutumia siku mbili hadi tatu kuziingiza kwenye usajili wa TCAA pamoja na kukamilisha taratibu nyingine za kisheria ili ziweze kupata ruhusa ya kufanya safari za hapa kwetu,” ilieleza.
Iliongeza kuwa safari ya kwanza ya ndege hiyo, inatarajiwa kufanyika Septemba 27, mwaka huu kwenda jijini Mwanza.
“Tutakuwa na madaraja mawili yaani daraja la uchumi (Economy Class) litakalohusisha abiria 70 na daraja la biashara (Business Class) litakalohusisha abiria sita kwa kila ndege,’’ ilibainisha. Ilitaja baadhi ya maeneo ambayo shirika hilo litaboresha zaidi safari zake kuwa ni Dodoma, Mwanza, Arusha, Mbeya, Kigoma, Tabora, Mpanda, Kilimanjaro, Mtwara, Zanzibar, Pemba, Bukoba na Visiwa vya Comoro. Ujio wa ndege hizo unatajwa kuwa utaleta mapinduzi makubwa kihuduma na kiutendaji kwa shirika hilo.
Tayari kampuni hiyo imebainisha kwamba imeunda kikosi kazi, kinachosimamia masuala mbalimbali likiwemo suala la mafunzo ya watendaji wake mbalimbali ili kuendana na matakwa ya biashara hiyo kwa sasa likiwemo suala la kufanya biashara kwa ushindani. Ujio wa ndege hizo ni ahadi ya Rais John Magufuli aliyoitoa mara baada ya kuingia madarakani, ambapo kupitia bajeti ya wizara hiyo ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ilitenga pia kiasi cha fedha kwa ajili ya ununuzi huo.
Kwa mujibu wa Waziri wake, Profesa Makame Mbarawa wakati akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2016/17, serikali imejipanga kukamilisha ununuzi wa ndege mbili aina ya Bombardier Q400 kwa ajili ya ATCL ili kufufua safari za ndani za kampuni hiyo.
Hadi sasa ATCL ina ndege moja aina ya Bombadier Q300, hivyo ujio wa ndege hizo utaifanya kuwa na ndege nne zinazotoa huduma ya usafiri wa anga nchini.