pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com
Showing posts with label Matukio. Show all posts
Showing posts with label Matukio. Show all posts

New Force Dar - Songea Laua na Kujeruhi


Basi la New Force kutoka Dar es salaam kwenda Songea
limepata ajali baada ya kupinduka eneo la Kifanya kilomita kadhaa kutoka mkoani Njombe.
Ajali hiyo imetokea Septemba 19,2016 majira ya saa moja na dakika 40 usiku.
Inaelezwa kuwa watu 12 (wanawake 8,wanaume 4) wamepoteza maisha huku 9 wakijeruhiwa.
Abiria wa basi hilo wanasema basi lilikuwa katika mwendo kasi na kwamba lilinusurika kupinduka mara mbili na mara ya tatu ndipo likapinduka.
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe ACP Prudenciana Protas amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Tetemeko lawalaza mapadri kwenye magari Bukoba

Ni kutokana na nyumba zao kuathiriwa vibaya, ibada ya Jumapili Kashozi yafanyika nje

17: Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

2,063: Nyumba zilizoanguka kutokana na tetemeko hilo.

5.7: Kipimo cha ritcher kilichotajwa katika tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

*******************************
Bukoba. Mapadri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kashozi, Jimbo la Bukoba wanalala kwenye magari baada ya nyumba walizokuwa wakiishi kuharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea wiki iliyopita.
Magari hayo mawili ambayo baada ya shughuli za kutwa huegeshwa kando ya nyumba zilizoharibika, yanatumiwa na mapadri wanne kulala huku wafanyakazi wengine wakipata hifadhi kwenye majengo machache yaliyonusurika.
Akizungumzia adha hiyo, Paroko wa Kanisa hilo, Padri Philbert Mutalemwa alisema tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi na kuharibu kanisa la kihistoria la Kashozi na nyumba za mapadri, wao waliamua kulala kwenye magari.

Miaka 30 Jela kwa Kumlawiti Msichana juu Ya Kaburi

Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi imemuhukumu Ally Rashid maarufu Ally Mwizi kifungo cha miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti kwa nguvu makaburini juu ya kaburi msichana (25) jina limehifadhiwa mkazi wa mtaa wa Kotazi Mjini Mpanda.
Hukumu hiyo iliyovuta hisia za watu wengi wa manispaa ya Mpanda ilitolewa jana na hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Chiganga Ntengwa baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Upande wa mashtaka ulikuwa ukiongozwa na mwanasheria wa serikali wa mkoa wa Katavi Jamila Mziray.
Awali katika kesi hiyo mwendesha mashtaka mwanasheria wa serikali wa mkoa wa Katavi Jamila Mziray alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Ally Mwizi alitenda kosa hilo Juni 17 mwaka huu majira ya saa mbili usiku huko katika Makaburi ya Kashaulili yalioko katika mtaa wa Kotazi Mjini Mpanda.
Ilidaiwa kuwa mshtakiwa kabla ya kutenda kosa hilo alimfuata msichana huyo ambaye alikuwa ameibiwa vitu vyake vya ndani ya nyumba hivyo Ally Mwizi alimdanganya kuwa yeye anao uwezo wa kumsaidia kuvipata vitu vyake vilivyoibiwa.
Mziray aliiambia mahakama kuwa baada ya msichana huyo kuahidiwa na mshitakiwa kuwa vitu vyake alivyoibiwa vitapatikana ,aliambiwa amlipe ujira Ally Mwizi kiasi cha shilingi 30,000/= ili aende akamwonyeshe vitu vyake alivyoibiwa na alifanya hivyo.
Alieleza kuwa siku hiyo ya tukio mshitakiwa alimpigia simu msichana huyo majira ya saa mbili ili akamuoneshe vitu hivyo alivyoibiwa .
Mziray alisema baada ya kumpigia simu mshitakiwa alikwenda nyumbani kwa msichana huyo na kumchukua na kisha alikwenda naye kwenye makaburi ya Kashaulili kwa lengo la kwenda kumwonesha vitu alivyoibiwa.
“Baada ya kufika makaburini mshitakiwa alimpiga ngwala msichana huyo na kisha kuanza kumlawiti juu ya kaburi huku akimtishia kumuua endapo angepiga kelele”…
“Baada ya kumaliza haja yake mshitakiwa alimwomba dada huyo waende kwenye nyumba ya kulala wageni inayoitwa King Paris ili wakaendelee kufanya mapenzi zaidi kwa kile alichodai kuwa eneo la King Paris panafaa zaidi kufanyia tendo la ndoa kuliko juu ya kaburi”,alieleza Mziray.
Kufuatia kitendo hicho, msichana huyo alipoamua kupiga mayowe ya kuomba msaada na watu walifika kwenye eneo hilo na waliweza kumkamata mshitakiwa .
Akisoma hukumu hiyo hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Chiganga Ntengwa aliambia mahakama kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo pasipo shaka yoyote mahakama imemwona mshitakiwa Ally Mwizi kuwa amepatikana na hatia ya kifungu cha sheria Namba 154 kidogo cha kwanza ya makosa ya adhabu sura na 16.
Alisema kutokana na kupatikana na kosa hilo mahakama imemuhukumu Ally Mwizi kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ili akitoka gerezani awe na tabia njema kwenye jamii ya watu.

Maisha ya madereva 10 waliotekwa DRC hatarini

DAR ES SALAAM
SERIKALI imeingilia kati na kuanza mazungumzo ya kuwaokoa madereva 12 wa malori kutoka Tanzania waliotekwa nchini Kongo (DRC) na kundi la waasi wa Mai Mai.
Waasi hao mbali na kuwateka madereva hao wametoa saa 24 kuanzia juzi saa 10 jioni walipwe fedha kiasi cha Dola za Marekani 4,000 kwa kila dereva ili waweze kuwaachia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga, alisema waasi hao wametishia kuwaua mateka hao endapo hawatalipwa kiasi hicho cha fedha hadi kufikia jana saa 10 jioni.
Mindi alisema katika tukio hilo, madereva wawili wa Kitanzania walifanikiwa kutoroka na ndiyo waliosaidia kutoa taarifa kuhusu tukio hilo.
“Serikali imepokea taarifa za kutekwa kwa malori 12 katika eneo la Namoyo Jimbo la Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jana (juzi) Septemba 14, 2016. Kati ya malori hayo manane yanamilikiwa na mfanyabiashara wa Kitanzania, Azim Dewji na mengine yanamilikiwa na wafanyabiashara kutoka Kenya.
“Kwa taarifa zilizopatikana watekaji ni kikundi cha waasi cha Mai Mai ambao baada ya kuyateka magari hayo, waliwashusha madereva na kuwapeleka porini na kisha kuteketeza kwa moto malori manne ambayo yote ni ya Dewji.
“Waasi hao wametoa saa 24 kuanzia jana saa 10 jioni walipwe fedha kiasi cha Dola za Kimarekani 4,000 kwa kila dereva ili waweze kuwaachia,” alisema Mindi.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeshachukua hatua za awali za kuwasiliana na Serikali ya DRC ili kuhakikisha kuwa madereva hao wanaachiwa haraka iwezekanavyo wakiwa salama kabisa.
Alisema tukio la aina hiyo ni la pili kutokea ambapo katika mwaka jana masheikh kutoka Tanzania walitekwa nchini DRC lakini kwa ushirikiano wa Serikali hizo mbili juhudi ziliweza kuzaa matunda na masheikh hao kuachiwa huru bila madhara yoyote.
“Serikali ingependa kuushauri umma wa Watanzania hususan wafanyabiashara kuomba taarifa ya hali ya usalama kwa maeneo yenye matatizo ya kiusalama kama Mashariki ya Kongo hususan Kivu ya Kusini kabla ya kusafiri kwenda maeneo hayo,” alisema Mindi.
Kauli ya Azim
Akizungumza na MTANZANIA jana Mkurugenzi wa Kampuni ya Simba Logistics, Azim Dewji alithibitisha kutekwa kwa madereva wake.
Alisema tayari ubalozi wa Tanzania nchini Kongo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wanashughulikia suala hilo.
Alisema tukio hilo limetokea sehemu inaitwa Kasebebena na Matete, wastani wa kilomita 30 kutoka mji wa Namoya nchini humo.
Aliyataja majina ya madereva waliotekwa na waasi hao wa Kundi la Mai Mai kuwa ni Hamdani Zarafi, Athuman Fadhili, Juma Zaulaya, Adam James, Issa Idd Omary, Bakari Shomari, Hussein Mohamed na Mwamu Mbwana Twaha.
Kauli ya ACT-Wazalendo
Kutokana na hali hiyo Chama cha ACT -Wazalendo, kilisema kimepokea kwa mstuko taarifa ya kutekwa kwa Magari 12 ya kusafirisha mizigo yaliyokuwa safarini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Taarifa ilitolewa na Katibu wa Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mbozu, ilieleza kuwa moja ya malengo makuu ni kuhakikisha Watanzania wanakuwa salama popote waendapo.
Taarifa ya Tatoa
Taarifa iliyotolewa na Chama cha Wamiliki wa Magari ya Mizigo Tanzania (Tatoa), ilieleza kwamba waasi wa Mai Mai wa Kongo, wamewateka nyara madereva hao wa Tanzania na kuchoma baadhi ya magari ya mizigo.
Katika tukio hilo inaelezwa kuwa magari manne ya Tanzania yamechomwa moto na madereva wote walichukuliwa na waasi ambapo tukio hilo limetokea sehemu inayoitwa Kasebebena na Matete, wastani wa kilomita 30 kutoka Mji wa Namoya.
“Tatoa inawashauri wanachama waliopakia mzigo kuelekea huko kuwasiliana na madereva wao ili wasitishe safari, kusubiri taarifa ya hali ya usalama kutolewa,” ilieleza taarifa hiyo ya Tatoa.
Historia ya kundi la Mai Mai
Mai Mai Kata ni kundi la waasi nchini DRC ambalo linadai kupigania uhuru wa Jimbo la Katanga linaloongozwa na Gedeon Kyungu Mutanga, ambaye aliunda kundi hilo kutoroka gerezani mwaka 2011.

Akatwa Ulimi Kwa Meno Akila Denda

Katika hali isiyokuwa ya kawaida kijana aliyejulikana kwa jina Said Juma amelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida baada ya kung’atwa hadi kunyofolewa zaidi ya theluthi moja ya ulimi wake na mwanamke anayetuhumiwa kufanya naye mapenzi hali iliyomfanya apoteze uwezo wa kuongea zaidi ya kutoa maelezo kwa njia ya maandishi.
Akizungumza kwa njia ya maandishi kijana huyo aliyelazwa katika chumba cha wagonjwa wa kinywa na meno amesema kuwa siku ya tukio akiwa njiani kutoka kwenye
sherehe za Idd El Hajj alikutana na mwanamke jirani akinywa pombe katika glocery moja ambaye alimuomba amsindikize nyumbani kwake.
Kijana huyo anaeleza kuwa akiwa njiani,mwanamke huyo alimtaka kijana huyo wafanye mapenzi na baada ya kumkatalia alimuomba amuage kwa kumpa ulimi “kula denda” ndipo alipomng’ata hadi kumnyofoa kipande cha ulimi na kutoweka nacho.
Madaktari wanaomtibu kijana huyo wanasema kidonda hicho baada ya kuacha kutoa damu kilitengeneza maambukizi kukawa na harufu inatoka mdomoni na kwamba hali yake inaendelea vizuri.
Wamesema ingawa amepata ulemavu lakini kijana huyo anaweza kuongea tena baada ya kupona japo matamshi yake ya maneno hayatakuwa kama alivyokuwa anaongea mwanzo.
Mama mzazi wa kijana huyo tayari ameripoti tukio hilo kituo cha polisi kwani mbali na mtoto wake kupata ulemavu pia alipata kipigo kutoka kwa mwanamke huyo.
Bado mtuhumiwa hajakamatwa na polisi wanafanya ufuatiliaji.
Chanzo- Kipindi cha Matukio Radio Free Africa

Abiria watozwa viingilio feki Kituo cha Ubungo

ABIRIA wa mabasi ya kwenda mikoani na nchi jirani katika Kituo cha Ubungo (UBT), wa- natozwa viingilio batili kiny- ume cha utaratibu.
Utaratibu unaojulikana abiria anapokuwa na tiketi hairuhisiwi kumtoza fedha za kiingilio ambayo ni Sh 300. Hata hivyo, hali ni tofauti kwani watu wote wamekuwa wakitozwa fedha za viingilio. Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, abiria hao walisema wameshangazwa na utaratibu huo,kwani siku zote wanaposafiri huingia katika kituo hicho kwa kutumia tiketi za mabasi wanayosafiria.
Mmoja wa abiria  hao Angela Yoredi aliyekuwa akisafiri kuelekea Dodoma na basi la ABC alisema ilimpasa kulipia kiingilio cha Sh 200, licha kuonesha tiketi yake mlangoni.
“Nashangaa imebidi nilipie Sh 200 wakati siku zote nikiwa na tiketi ya basi ninapita bila kulipia, waliniambia huo ni utaratibu mpya unaotumika kwa sasa,” alisema Angela.
Naye Mohamedi Issa ambaye alikuwa anasafiri na basi la Hood kwenda Morogoro alisema kwa sasa utaratibu wa kuingia katika kituo hicho haueleweki, kwani awali watu waliokuwa wanalipa ni wale waliokuwa wakiingia kituoni kwa ajili ya kupokea au kusindikiza abiria.
“Utaratibu wa humu sasa haueleweki pale mlangoni kuna abiria wanalipa Sh 200 lakini mimi nililipa Sh 300 in- gawa nilikuwa tayari na tiketi yangu ya basi,” alisema.
Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Ofisa Uzalishaji, Uratibu na Ushuru kituoni hapo, Novat Francis, alisema kitendo hicho ni kinyume cha sheria na uta- ratibu ambao umepangwa katika kituo hicho.

Ajifungua salama bwenini, walimu wamsaidia

Dodoma. Mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari Mbabala, Manispaa ya Dodoma, Helena Mpondo amejifungua mtoto ndani ya bweni.
Mwanafunzi huyo amejifungua mtoto mwenye afya njema kwa usaidizi wa walimu na baadaye aliitwa mganga wa zahanati ya jirani kwa ajili ya kumkata kitovu na msaada mwingine.
Helena, Ijumaa ya Septemba 2 saa tatu asubuhi alizidiwa na uchungu akiwa peke yake bwenini, lakini matroni na mwalimu mwingine wa kike waliwahi kufika eneo hilo na kumsaidia kujifungua salama.
Mkuu wa shule hiyo, Joram Mkwawa amesema siku ya tukio, saa tatu asubuhi aliitwa na walimu wenzake bwenini na alikuta binti huyo amejifungua.
“Nilichofanya niliwaambia waende zahanati na nilituma pikipiki ya kumfuata mzazi wake ambaye alipofika, nilimkabidhi mwanawe kwa kuwa ni kosa kukaa na mtoto mwenye mimba,” amesema.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme alitoa taarifa kuwa manispaa hiyo ilikuwa na wanafunzi 51 wenye mimba na kati yao, 45 walikuwa wa shule za sekondari na sita wa shule za msingi.

Kizimbani kwa udhalilishaji mitandaoni

Dar es Salaam. Sheria ya mitandao imeendelea kung’ata, baada ya wakazi wa Dar es Salaam kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusomewa mashtaka tofauti ya kumdhalilisha Rais na Jeshi la Polisi kwenye mitandao.
Katika kesi ya kwanza, Dennis Temu (26), ambaye ni fundi magari anayeishi Tabata, alisomewa mashtaka ya kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwenye mtandao wa WhatsApp.
Wakili wa Serikali, Salum Mohammed alidai mbele Hakimu Mkazi Mkuu, Emilius Mchauru kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 30, 2016 akiwa Tabata Bima, wilayani Ilala kwa kutumia mtandao wa WhatsApp kusambaza ujumbe usemao; “Nipo tayari kwa Ukuta naomba wanikabidhi askari 10 nipambane nao wakinishinda Mungu anihukumu. Tupigane mkono kwa mkono ‘pumbav’... zao”.
Temu amekana shtaka hilo na upande wa mashtaka ulidai upelelezi haujakamilika.
Mshtakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao walisaini dhamana ya Sh500,000. Kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 12.
Katika kesi nyingine, Suleiman Nassoro (20), fundi umeme anayeishi Kigogo Mbuyuni, amesomewa mashtaka ya kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kuandika ujumbe usemao; “safi sana aisee, mi naona wangekufa kama 20 hivi. Halafu Simon Sirro tumuulize mazoezi wanafanyia wake zao au” ambao aliutuma Agosti 25.
Lakini Nassoro amekana kutenda kosa hilo na upande wa mashtaka ulisema haujakamilisha upelelezi, jambo lililofanya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 27 itakapotajwa tena.
Mwingine ni dereva Juma Mtatuu (19) anayedaiwa kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwa kutumia WhatsApp kwa kuandika; “huyu hata akifa ataenda peponi na kufanya mazoezi kote kule wamekufa Mbagala. Mimi nitakuwa  wa kwanza kuandamana kule Kahama. Tarehe 1 Naelekea Kahama kwa Ukuta mimi nitakuwa namba moja kushika bendera ya Ukuta. Kifo kipo tu, usiogope kwani mawe na mapanga yameisha?”
Pia, mkazi wa Tegeta kwa Ndevu, Shakira Abdallah Makame amefikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na shtaka la kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwa kutumia WhatsApp.
Katika ujumbe wake, Shakira anadaiwa kusema; “wakati tunajiandaa na Ukuta, wao wanajiandaa na ujambazi safi sana majambazi”.
Denis Wilson Mtegwa (27), alikuwa mmoja waliopandishwa kizimbani na kushtakiwa kwa kumdhalilisha Rais John Magufuli katika ujumbe wa WhatsApp alioutuma Agosti 24 akiwa Ubungo External wilayani Ubungo.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Kisutu, Dk Yohana Yongolo, ujumbe usemao; “JPM sijui anawaza nini kichwani, hata samahani hajui au nilikosea hajui. Nchi imefika hapa kwa sababu ya mtu mmoja aliyeamua kujilipua ufahamu wake.

Majambazi 10 yateka magari, yaua dereva


Sumbawanga. Wafanyabiashara waliokuwa wakitoka mnadani wamevamiwa na m ajambazi yapatayo 10 ambayo na kumuua kwa risasi dereva aliyegoma kuwapa fedha na simu.
Dereva huyo, Chrispin Inyangwe (40) alipigwa risasi ya mgongoni alipojaribu kupambana nao.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana eneo la katikati ya vijiji vya Miula na Kalundi vilivyopo Kata ya Kipande wilayani Nkasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando amesema wafanyabiashara hao walikuwa wakitokea mnadani na walipofika eneo hilo walikuta mawe yamepangwa barabarani kuzuia magari.
Amesema baada ya kuona mawe hayo, magari hayo yalilazimika kusimama na ndipo majambazi hao waliokuwa na silaha za moto, mapanga na marungu walipoibuka na kufyatua risasi hewani na baadaye kutaka wafanyabiashara hao wasalimishe fedha na simu zao za mkononi.

Mabilioni yakusanywa tetemeko la Bukoba


WAKATI vifo vya waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera vikiongezeka na kufikia 17, uongozi wa mkoa huo umesema zinahitajika zaidi ya Sh bilioni 2.3 kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya waathirika, na tayari serikali jana imehamasisha na kupatikana zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Kati ya fedha hizo zilizopatikana, Sh milioni 700 zilikuwa ahadi, fedha taslimu Sh milioni 646, Dola za Marekani 10,000, Euro 10,000 na mifuko 2,800 ya saruji.
Kampuni za mafuta ya Oilcom, GBP na Moil, zimejitolea kujenga shule mbili za sekondari zilizoathiriwa na tetemeko hilo. Shule hizo zimefungwa. Jumamosi iliyopita, saa 9.27 alasiri mji wa Bukoba ulikumbwa na tetemeko la ardhi, ambalo nguvu ya mtetemo wake ulikuwa ni 5.7 kwa kutumia skeli ya “Ritcher”.
Ukubwa huo ni wa juu kiasi cha kuleta madhara makubwa ikiwemo kuanguka nyumba, nyingine zimepata nyufa, watu 17 wamekufa, na mamia wawamejeruhiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu alisema, baada ya Kamati ya Maafa ya Mkoa na Kamati ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, wamefanya tathmini ya haraka na kubaini mahitaji kwa wananchi walioathirika.
Kijuu aliwaomba wananchi, wadau na marafiki walioguswa na janga hilo katika mkoa na nje ya mkoa, wachangie michango yao kupitia akaunti ya maafa iliyopo katika benki ya CRDB yenye namba 0152225617300 na kwa walioko nje watumie Swift code:CORUtztz, huku akiomba watakaowiwa kutoa wawasiliane na ofisi yake kwa maelezo zaidi.
Alitaja mahitaji ya muhimu ambayo yanahitaji kwa haraka ni dawa, tiba na vifaa tiba, vifaa vya ujenzi mabati 90,000 yenye gharama ya Sh bilioni 1.7, saruji mifuko 9,000 yenye thamani ya Sh milioni 162, mbao zenye thamani ya Sh milioni 450 na misumari yenye thamani ya Sh milioni 12 ambapo jumla ni Sh bilioni 2.3. Majaliwa achangisha bil 1.4/- Wakati Kijuu akisema hayo, Majaliwa amehamasisha wafanyabiashara pamoja na mabalozi, kuchangia na kuchangisha zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kuwa kutokana na tetemeko hilo kubwa, imelazimu serikali kuzifunga shule mbili za sekondari zilizoharibiwa vibaya za Nyakato na Ihungo. Waziri Mkuu alisema tetemeko hilo ni kubwa ambalo halijawahi kutokea nchini, hivyo haikutarajiwa na wala hakukuwa na maandalizi ya kukabiliana na hali kama hiyo.
Alisema mpaka jana watu 17 walikuwa wamefariki dunia huku 253 wakijeruhiwa na 145 walikuwa wako katika hospitali huku vitu vingi pamoja na miundombinu vikiharibika.
Katika miundombinu ya shule nne za Nyakato, Ihungo, Kashenge na Buhembe, zimeharibika ikiwemo vyoo, nyumba za walimu, kumbi za shule na mabweni yameharibika kabisa pamoja na hospitali na vituo vya afya navyo vimeharibika.
Alisema kuna baadhi ya sehemu hali ni mbaya na wanahitaji msaada ambapo nyumba 840 zimeanguka kabisa chini huku nyumba na majengo 1,264 yakiwa na nyufa na kamati ya maafa katika mkoa pamoja na viongozi wake wanaendelea kufanya tathmini ya kiasi cha hasara iliyopatikana.
Alisema serikali imefanya juhudi katika kukwamua maisha ya wananchi wake na mawaziri watatu wako mkoani humo kuangalia namna ya kukabiliana na majanga hayo ambao ni Waziri wa Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa, Elimu Profesa Joyce Ndalichako na Waziri wa Nchi katika ofisi yake, Jenista Mhagama.
Alisema kupitia kitengo cha maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu wamefungua akaunti hiyo katika benki ya CRDB huku wakiendelea na maandalizi ya kupata namba za kuchangia kwa simu ya mkononi huku akiwashukuru wabunge walioamua kuchangia maafa hayo kwa kutochukua posho zao za siku ya jana.
Mabalozi, Wafanyabiashara Mkuu wa Jumuiya ya Mabalozi, Balozi wa Zimbabwe nchini, Edzai Chimonyo alisema kutokana na tarifa hiyo kuwa ya ghafla na wako sehemu mbalimbali duniani watakusanyika na kuwasilisha michango yao. Lakini, hata hivyo, balozi mbalimbali zilijitokeza kuwasilisha michango yao ikiwemo Ubalozi wa China, uliotoa Sh milioni 100, wafanyabiashara wa Kichina walitoa Sh milioni 100 na Ubalozi wa Kuwait Sh milioni 50.
Pia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilitoa mchango wa wafanyakazi wake Sh milioni 10 huku ikiandaa matembezi ya kuchangisha fedha zaidi kwa waathirika wa tetemeko hilo yatakayofanyika Jumamosi wiki hii. Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Azizi Mlima alisema wameanza kwa kukabidhi fedha hizo ambazo ni mchango wa wafanyakazi, lakini Jumamosi wamealika wadau mbalimbali katika matembezi hayo watakayochangia zaidi.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald Mengi alisema wafanyabiashara wako pamoja katika kuhakikisha wanakabiliana na tatizo hilo na kuipongeza serikali kwa hatua za haraka walizochukua kukabili majanga hayo.
Mengi alichangia Sh milioni 110, Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL) kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Mohamed Dewji ilitoa Sh milioni 100, Kampuni ya Bia (TBL) Sh milioni 100, Chama cha Wauzaji Mafuta kwa Rejareja Sh milioni 250 huku Umoja wa Waagizaji Mafuta ukiahidi kuchangia baada ya kikao watakachokaa leo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alishukuru kwa wafanyabiashara na mabalozi kwa michango hiyo na kuomba ipatikane kwa haraka ili kusaidia wananchi wa mkoa huo kurejea katika maisha yao ya kawaida.
RC afafanua zaidi
Kijuu alisema shule za sekondari Ihungo na Nyakato zimefungwa kwa muda wa wiki mbili kutokana na miundombinu yake kuharibika, ambayo ni madarasa, vyoo na mabweni baada ya kuta kuanguka au kupata nyufa kubwa na kuonekana haifai kutumika tena, huku wanafunzi wakiruhusiwa kurudi katika familia zao baada ya kuonekana kuathirika kisaikolojia.
Alisema Kamati ya Maafa kuanzia sasa, inajenga miundombinu hiyo ndani ya muda wa wiki mbili ili irudi katika hali yake ya kawaida na wanafunzi warudi shuleni na kuendelea na masomo yao kama kawaida.
Pia serikali imefanya juhudi za kuleta wataalamu wa afya ambao ni madaktari bingwa sita kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyoko jijini Mwanza ili kutoa msaada kwa wagonjwa wanaohitaji msaada zaidi wa kitabibu huku Ubalozi wa nchi ya China ukileta waganga wa kusaidia matibabu kwa waathirika hao.
Aidha, katika uchunguzi uliofanywa na wataalamu kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kuhusu tetemeko hilo, walibainisha sababu kuwa ni kitovu cha tetemeko hilo kuwa kiko chini sana ya ardhi kwa kutafsiri umbile la tetemeko hilo lililonakiliwa na vituo vya kupima matetemeko ya ardhi ambapo inaonekana kuwa limetokana na misuguano ya mapande makubwa ya ardhi iliyopasuliwa mithili ya mipasuko kwenye Bonde la Ufa.
Pia Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hasa wataalamu kutoka GST wameandaa vituo mbalimbali katika mkoa ili kutoa elimu jinsi ya kufanya mazoezi ya kuchukua tahadhari kabla ya tetemeko, wakati wa tetemeko na baada ya kutokea ili kujizoesha kwani mara nyingi wakati wa matukio kama ya majanga kama hayo watu huchelewa kuchukua uamuzi wa haraka kujinusuru kwamba wafanye nini. Taarifa ya serikali bungeni
Akisoma taarifa ya serikali bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - Tamisemi), George Simbachawene kwa niaba ya Waziri Mkuu, alisema tetemeko hilo lenye ukubwa wa 5.7 katika vipimo cha “Ritcher”, kufikia jana lilisababisha vifo vya watu 17 na kujeruhi watu 252, kati yao 169 wakiwa wamelazwa hospitalini.
Alisema nyumba za makazi zilizoanguka ni 840 huku nyumba za makazi zenye nyufa zikiwa 1,264 na majengo ya taasisi yaliyoripotiwa kuanguka ama kupata nyufa ni 44. Kutokana na athari hizo, serikali imetangaza kuchukua hatua kadhaa, ikiwemo ya kuokoa na kuwapeleka hospitalini waathirika kwa ajili ya matibabu.
Imewapatia pia makazi ya muda baadhi ya wananchi ambao nyumba zao zimeathirika. Serikali pia imeongeza nguvu ya madaktari bingwa 15 kutoka mkoani Mwanza ili wasaidie kutoa huduma za haraka kwa waathirika, huku ikiwahamasisha wananchi wasaidiane kila inapowezekana.
Alisema serikali pia imeelekeza wanajiolojia kutoa maelekezo ya kisayansi ili kuwatoa hofu wananchi kuhusu hali hiyo.
Taarifa hiyo imesema Serikali inaendelea kuhakikisha hatua za dharura zinachukuliwa kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha kuwa hatua za muda mfupi na muda mrefu zinatambuliwa na kutekelezwa ili kuwasaidia waathirika.
Wakati hayo yakiendelea, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya athari zilizosababishwa na tetemeko la ardhi. Kutokana na janga hilo, serikali imewaomba wadau wa ndani na nje wanaotaka kuchangia waathirika, wawasiliane moja kwa moja na Ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Kagera, huku ikionya watu kuacha kutumia maafa hayo kujinufaisha.
“Wananchi mnaombwa kuwa wavumilivu na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua tatizo ambalo limeipata nchi ili wananchi waendelee kupata huduma kulingana na athari za tetemeko,” alisema Simbachawene.
Wabunge waunga mkono
Kutokana na kuguswa na tukio hilo, wabunge jana waliunga mkono juhudi za Serikali na wameridhia kwa kauli moja kukatwa posho yao ya siku moja, sawa na Sh 220,00 kila mmoja ili kuchangia maafa hayo.
Bunge lina wabunge 389.
Uamuzi huo ulitokana na hoja ya Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi (CCM) aliyeomba Bunge liahirishe mjadala uliokuwa mezani wa Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu 2016 na Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wataalamu wa Kemia 2016 ili kujadili tukio la tetemeko la ardhi Kagera ambalo ni la dharura.
Alipendekeza pia wabunge wajadili kwa muda wa nusu saa suala hilo pamoja na kuchangia posho yao ya siku moja. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alipokea ombi la Shangazi na kusema kuwa ataruhusu mjadala huo kwani kanuni zinaruhusu.
Hata hivyo, alisema kitakachojadiliwa ni hoja ya dharura na mchango wa wabunge, lakini sio kujadili Kauli ya Serikali kuhusu tetemeko hilo iliyotolewa na Waziri Simbachawene kwa niaba ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) alionesha utovu wa nidhamu mbele ya Bunge na Naibu Spika kwa kumnyooshea kidole Dk Tulia jambo lililofanya avunje Kanuni ya 74 inayomtaka mbunge kutoonesha dharau yoyote kwa aliyekalia kiti cha uongozi bungeni.
Mdee atia doa Naibu Spika alimkanya Mdee, akisema, “Mheshimiwa Halima Mdee acha kuninyooshea kidole, acha kunyoosha vidole, huo ni utovu wa nidhamu kwa kiti… hebu Halima Mdee uwe na heshima kidogo, hebu kuwa na heshima kidogo.”
Baada ya kauli hiyo ya onyo, Halima alionekana kususa na kutoka nje ya Bunge wakati wabunge wakianza kujadili hoja ya dharura iliyoletwa mezani na Shangazi. Akichangia Shangazi alianza kwa kupendekeza wabunge kuchangia posho yao ya siku hiyo ambayo ni Sh 220,000 ili kuwafariji wananchi waliopatwa na tatizo la tetemeko hasa manispaa ya Bukoba.
“Tunamshukuru Mungu tukio limetokea mchana, kama ingekuwa usiku huenda maafa yangekuwa makubwa zaidi. Tukio hili litufunze kuweka kanda maalumu zinazoshughulikia maafa ili tatizo linapotokea litatuliwe haraka,” alisema.
Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) alisema tukio hilo la tetemeko liwaunganishe wabunge wa kambi zote, kwani Bunge ni chombo cha wananchi na kutaka wabunge bila kujali itikadi kusaidia kuielekeza serikali nini cha kufanya kukabiliana na maafa hayo.
Aliunga mkono hoja kuchangia posho ya siku ya jana, ingawa alisema tayari kwa upande wao wapinzani walishachangishana Sh 100,000 kila mmoja kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tukio hilo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Vullu (CCM) naye aliunga mkono hoja ya kuchangia posho yao ya siku na kuongeza suala hilo limegusa hisia za watu na kuonya wanasiasa kutotumia maafa hayo kujiinua kisiasa.
Vullu aliipongeza serikali kwa juhudi zake tangu kutokea kwa tukio hilo, lakini alisisitiza haja ya kutolewa elimu zaidi ya kukabiliana na maafa na njia za kuokoa watu yanapotokea matukio ya dharura kama hilo la tetemeko la ardhi.
Mbunge wa Muleba, Profesa Anna Tibaijuka (CCM) alisema ametoka Bukoba na kwamba ameshuhudia hali ilivyo mbaya katika maeneo yaliyoathirika na tetemeko hilo na kuongeza kuwa ni mkono wa Mungu tu ndio umeepusha maafa kuwa makubwa zaidi.
Alisema suala hilo sio la kisiasa na kwamba wananchi wanahitaji faraja na kutaka kama taifa Watanzania wawe wamoja bila kujali itikadi zao na kutaka tathmini ifanywe kitaalamu zaidi.
Alitaja baadhi ya maeneo aliyotembelea na kujionea athari kubwa ikiwemo Manispaa ya Bukoba, ambapo alisema kati ya nyumba 10 tatu zimeharibika kabisa, hivyo inahitajika tathmini ya kitaalamu sana ili kubaini iwapo eneo husika linafaa tena kujenga au watu wanatakiwa kuhama.
Mbunge wa Buchosa ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alisema tetemeko limeleta uharibifu mkubwa katika mkoa wa Kagera ingawa maeneo mengine yameguswa ikiwemo Mwanza, Geita na Shinyanga.
Mara baada ya wabunge hao kumaliza kuchangia, Naibu Spika Dk Tulia alilihoji Bunge ambalo kwa pamoja liliunga mkono kutoa posho kwa ajili ya kuchangia waathirika wa tetemeko Bukoba.
Akishukuru kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwashukuru wabunge kwa kutoa mkono wa faraja na kuungwa mkono na Bunge zima.
“Hili ni jambo letu sote, kwani ni utamaduni wa Watanzania kusaidiana na kuchangiana yanapotokea majanga kama haya. Serikali inaahidi mchango wenu utawafikia walengwa kama ilivyokusudiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali inalichukulia suala hilo kwa ukubwa wake na ndio maana, Rais John Magufuli aliahirisha safari ya kikazi Lusaka, Zambia na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yuko Dar es Salaam akikutana na wataalamu na wadau wa ndani na kimataifa kuona namna gani walikabiliana na maafa ya tukio hilo.
Athari Bukoba
Alisema Manispaa ya Bukoba ndiyo iliyoathiriwa zaidi, kwani imepoteza watu 15 waliokufa kutokana na tetemeko hilo, huku majeruhi wakiwa 142 kati ya 252. Aidha, nyumba 753 zimeanguka katika Manispaa ya Bukoba pekee, huku nyumba 1,037 zikipata nyufa.
Kwa upande wa taasisi alisema, shule kongwe ya Sekondari Ihungo imelazimika kufungwa kutokana na uharibifu mkubwa, kwani tetemeko limeangusha ukumbi wa shule, bweni moja huku mengine sita yakitajwa kuharibika vibaya na kutofaa kukaliwa na wanafunzi.
Aidha, madarasa 16 yamebomoka, huku vyoo 25 vikiharibiwa sambamba na mabafu mawili. Nyumba tatu za walimu zimeanguka na nyingine 17 zikipata nyufa.
Taarifa hiyo imeeleza kanisa na msikiti shuleni hapo vimebomoka, wakati maabara tatu zimepata nyufa ilhali mtego wa Radi moja umeanguka. Shule nyingine iliyofungwa ni Nyakato ambayo mabweni yake sita yameharibika na hayawezi kukaliwa huku mengine manane yakipata nyufa.
Aidha, vyumba vitano vya madarasa vimeharibika na vingine 15 vikipata nyufa. Pia tetemeko limeharibu jengo moja la utawala, nyumba nane za walimu ambazo hazifai kutumia wakati nyingine 17 zimepata nyufa. Athari za tetemeko zimezikumba pia halmashauri za wilaya ya Bukoba, Missenyi, Muleba, Karagwe na Kyerwa.

Mitambo ya kupima tetemeko yaibwa

WAKATI taifa likiwa katika majonzi kutokana na vifo 16 vilivyotokana na tetemeko la ardhi na kuacha majeruhi zaidi ya 253 mkoani Kagera wiki iliyopita, siri ya kushindwa kupimwa matetemeko nchini imebainika.
Imeelezwa kuwa vituo vitatu vikubwa vya kupima matetemeko vimefungwa baada ya kuhujumiwa na vingine vidogo 38 navyo vimefungwa baada ya wafadhili kujitoa.
Hayo yalielezwa jana na Jiolojia Mwandamizi wa Wakala wa Jiolojia Tanzania, Gabriel Mbogoni alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.
“Kwa kweli wanajiolojia tunapata changamoto kubwa katika kupima na kujua iwapo tetemeko litatokea katika eneo fulani na hiyo inatokana na kuhujumiwa baadhi ya mashine katika vituo vyetu.
“Tulikuwa na vituo zaidi ya 10 vya kupima matetemeko, hivi sasa vimebaki tisa pekee na ili kupata uhakika kama kuna tetemeko kwenye eneo fulani lazima uwe na vituo zaidi ya vitatu,” alisema.
Alisema vituo vilivyofungwa baada ya kuibwa vilikuwa katika mikoa ya Morogoro, Dodoma (Ntuka) na Arusha eneo la Longido.
“Ili tuweze kusimika mashine za kupima tetemeko tunahitaji kupata eneo ambalo lina mwamba mgumu.
“Zamani tulikuwa tukitafuta maeneo yenye miamba migumu huko vijijini, tukipata tunawasiliana na viongozi wa kijiji na tunaweka walinzi wa kulinda mashine hizo.
“Lakini zimeibwa hali iliyosababisha kufungwa vituo hivyo…tulipeleka kesi mahakamani mwisho tukaona ni vema sasa tuanze kuzifunga mashine hizo katika maeneo ya magereza kwa usalama wake isipokuwa kile cha Mtwara na Dodoma,” alisema.
Alisema wezi hao, wamekuwa wakiiba mashine hizo wakidhani wanaweza kunufaika, wakizifananisha na madini.
“Wengi wanadhani zinamilikiwa na Wizara ya Nishati na Madini kwamba wakiziiba watauza wapate faida. Unajua mashine hizi zipo kama sanduku, wanapoziiba huwa hawawezi kuziuza popote kwa sababu zinatambulika,” alisema.
Mbogoni alisema vituo vikubwa vilivyobakia vipo katika mikoa ya Mtwara, Dodoma, Geita, Arusha, Babati, Singida, Mbeya na Manyara.
Akizungumzia vituo vidogo 38 vilivyofungwa, alisema hiyo ilitokana na kumalizika mradi wa kupima matetemeko uliokuwa ukifanywa na wakala huo kwa kushirikiana na Chuo cha Pennyslvania State cha Marekani.
“Siwezi kutaja tumepata hasara kiasi gani kwa sababu sijui mashine hizo zilinunuliwa kiasi gani na sasa zinauzwa kiasi gani. Huwa tunazipata kutoka kwa ufadhili wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“Awamu ya kwanza wa mradi ulianza 2007 hadi 2008 halafu ukaanza tena 2013 hadi April 2015 ambako uliisha,” alisema.
Mbogoni alisema matetemeko mengine madogo yataendelea kutokea kwa muda.
“Ni hali ya kawaida linapotokea tetemeko kubwa huwa baadaye yanatokea mengine madogo madogo, yanaweza yakadumu hata kwa wiki au hadi miezi minne.
“Hii ni kwa sababu ile nguvu ya mgandamizo inayotokea ambayo husababisha miamba kumeguka huwa bado haijaisha na ndiyo maana tetemeko huendelea kutokea,” alisema.
Juzi, tetemeko kubwa lilitokea katika maeneo ya Kanda ya Ziwa hususan mkoani Kagera lilisababisha zaidi ya vifo 15 huku likiacha majeruhi zaidi ya 253.
Tetemeko hilo limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 kupata nyufa, yakiwamo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.
WANANCHI
Wakati huohuo, baadhi ya wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi mkoani Kagera wiki iliyopita wameiomba Serikali kuwasaidia kujenga mahema haraka weweza kujihifadhi kutokana na nyumba zao kuanguka
Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti mjini Bukoba jana, wananchi hao walisema hivi sasa wanalazimika kulala nje bila kuwa na kitu chochote cha kuwahifadhi.
Mmoja wa wananchi hao, Evodius Gozbert mkazi wa Bukoba mjini, alisema anakabiliwa na hali ngumu kutokana na nyumba yake yote kubomoka.
“Nimepoteza nyumba zangu, tunahitaji msaada wa haraka kutoka serikalini, wasiwasi wetu hapa mvua ikianza kunyesha tutakimbilia wapi.
“Kama ulivyosikia juzi saa 4.00 usiku na jana asubuhi tetemeko lilijirudia, hii inaonyesha wazi bado lipo, lazima tuwe na sehemu za kijikinga ndugu yangu,”alisema
Naye Joyce Ndukeke alisema tangu kutokea tetemeko hadi jana jioni alikuwa hajapata msaada kutoka serikalini.
“Mimi ni mzazi wa watoto wanne, nyumba zote zimeanguka, nasikitika mume wangu yuko safarini, hatuna pa kulala hapa si umeona limejirudia tena, hapa tumetawaliwa na hofu,”alisema.
Mutalemwa Emmanuel alisema wamekumbwa na hofu kubwa kwa sababu hata wanashindwa kutafuta vyumba vya kupanga katika nyumba nyingine, kwa sababu nazo zinaweza kuanguka.
Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Rwome, Ashiraph Alphonce alisema wameanza kuzungukia maeneo yote kuorodhesha nyumba zoye zilizobomoka na zile zenye nyufa.
“Tunapita kwenye mtaa wangu kuona nyumba zilizoanguka, mpaka leo (jana) nimehakiki kaya 58.
“Naiomba Serikali ilete msaada wa haraka kwa wananchi kwa sababu hadi sasa hakuna msaada wowote, wananchi wanaangaika wenyewe, tunaomba angalau wapatiwe mahema wapate pa kuishi,” alisema Alphonce.
DC
Akijibu malalamiko ya wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro, amewataka wawe watulivu wakati huu ambao Serikali inaendelea na kazi ya kuhakiki ili wapate msaada haraka iwezekanavyo.
“Nimeunda kamati ya kufuatilia wananchi walioathirika wale walengwa kabisa, mpaka sasa kwenye wilaya yangu kuna watu kama 3,000 hawana makazi,” alisema.
RC KIJIU
Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Meja Jenerali Salum Kijuu alisema mpaka jana mchana hakuna vifo vilivyoongezeka ingawa majeruhi waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wamepungua kutoka 253 hadi 61.
Alisema hakuna upungufu wa dawa na vifaa tiba vingine vinavyohitajika na huduma inaendelea kutolewa.

Taarifa Rasmi Juu Ya Tetemeko Kagera


WAKALA wa Jiolojia Tanzania (GST), umetoa ufafanuzi juu ya tetemeko lililotokea mkoani Kagera na kusema kuwa kitovu cha tetemeko hilo, kiko chini ya ardhi urefu wa kilometa 10. Aidha umetoa tahadhari kwa wananchi kwa kuzingatia na kuepuka madhara, yanayoweza kusababishwa na tetemeko la ardhi kabla ya tukio, wakati wa tukio na baada ya kutokea tukio ili kupunguza madhara yanaweza kutokea.
Katika taarifa yake jana, wakala huyo alisema kuwa tetemeko hilo lililonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi, limetokana na misuguano ya mapande makubwa ya ardhi iliyopasuliwa na mipasuko ya ardhi mithili ya mipasuko kwenye bonde la ufa.
“Tetemeko hilo lililotokea Septemba 10 mwaka huu majira ya saa 9:27, mchana kitovu chake kilikuwa kati ya latitudo 10 06’ na longitudo 31055’ eneo ambalo ni kilomita 20 Kaskazini Mashariki mwa kijiji cha Nsunga na kilomita 42 Kaskazini Magharibi mwa mji wa Bukoba, alisema Mtendaji Mkuu wa GST.
“Nguvu za mtetemeko wa ardhi wa tetemeko hilo ni 5.7 kwa kutumia skeli ya “Richter” ukubwa ambao ni wa juu sana kiasi cha kuleta madhara makubwa,” alisema Mtendaji Mkuu wa GST, Profesa Abdulkarim Mruma.
Alisema kutokana na ukubwa huo maeneo mengi ya Mkoa wa Kagera, ikijumuisha mji wa Bukoba yamepatwa na madhara makubwa ikiwa ni kusababisha vifo vya watu 16 kuharibika kwa nyumba nyingi, watu wengi kujeruhiwa kwa kuangukiwa na vifusi na kuta za nyumba.
Aidha taarifa hiyo ilisema kuwa eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi liko karibu na mkondo wa Magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki inakisiwa kuwa mtetemo huo ulisababishwa na kuteleza na kusuguana kwa mapande ya miamba juu ya mipasuko ya ardhi ya bonde hilo la ufa.
Aidha alisema mpaka sasa Tanzania na duniani kote, hakuna vifaa au taratibu za kuweza kutabiri utokeaji wa matetemeko ya ardhi na vifaa vyote na taratibu zote za kuratibu au kupima matetemeko ya ardhi vinapima ukubwa na tabia ya tetemeko baada ya tetemeko kutokea.
Alisema wakala huyo tayari umepeleka wataalamu katika eneo la tukio ili kuendelea kufanya utafiti wa kina juu ya tetemeko hilo na kwamba miongoni mwa vituo vya jiolojia vilivyorekodi tukio hilo la tetemeko ni kile cha Geita ambacho ndicho kilicho karibu sana na eneo la tetemeko hilo.
Mtendaji Mkuu alisema jamii inapaswa kupewa elimu ya tahadhari ili kila mmoja aelewe nini cha kufanya linapotokea tetemeko la ardhi ikiwa ni pamoja na kupata mafunzo kutoka kwa watu wa msalaba mwekundu kuhusu namna ya kuhudumia majeruhi ama wahanga na pia jeshi la zima moto ili kupata elimu kuhusu namna ya kutumia kizimamoto.
Alisema wananchi wanashauriwa kujenga nyumba bora na imara kwa kuzingatia viwango halisi vya ujenzi, kuweka misingi imara wakati wa ujenzi, kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya majengo yanayofaa kujengwa katika eneo husika kulingana na ardhi ya mahali hapo.
Wakati wa tetemeko mamlaka hiyo imesema kuwa wananchi wanashauriwa kukaa mahali salama kama vile sehemu ya wazi isiyo na majengo marefu, miti mirefu na miinuko mikali ya ardhi. Pia ilisema watu wanashauriwa kukaa nje ya nyumba katika sehemu za uwazi.
“Endapo tetemeko litakukuta ukiwa ndani ya nyumba unashauriwa ukae chini ya uvungu wa meza imara, ama kusimama kwenye makutano ya kuta na pia ukae mbali na madirisha na makabati ya vitabu, vyombo au fenicha ili kuepuka kuangukiwa na vitu hivyo,” ilieleza taarifa hiyo ya Profesa Mruma.
Aidha ilisema baada ya kutokea tukio la tetemeko wananchi wanashauriwa kuzima umeme katika majengo ili kuepuka kutokea kwa hitilafu ya umeme kama mitetemo itaendelea.
Pia wametakiwa kukagua majengo kwa uangalifu ili kuhakikisha kama hayakupata madhara na kama yanaweza kuendelea kutumika na ikibidi uwaita wataalamu wa majengo ili wayafanyie ukaguzi. Waathirika waomba msaada Katika hatua nyingine waathirika wa tetemeko hilo wameiomba serikali kuwasaidia kuwajenga mahema kwa ajili ya kujihifadhi, baada ya nyumba zao kuanguka kutokana na tetemeko hilo.
Mmoja wa waathirika hao, Joyce Ndukeke alisema kuwa tangu wamepatwa na janga hilo hawajapata msaada na kuwa wanachokifanya ni kujikusanya pamoja na kulala nje. Ndukeke ambaye ana watoto wanne alisema kuwa wakati tetemeko hilo likitokea alikuwepo nyumbani pamoja na watoto wake huku mumewe akiwa safarini kikazi.
"Nyumba zetu zimeanguka hatujapata msaada, hatuna pa kulala tunalala nje na watoto, lakini sasa tuna hofu zaidi maana hata jana (Jumapili) limepita tena, tunaomba tusaidiwe kujengewa mahema maana huu ni msimu wa mvua inaweza kunyesha wakati wowote tukanyeshewa pamoja na vitu vyetu tulivyofanikiwa kuokoa vikaharibika," alisema.
Pia muathirika mwingine, Mutalemwa Emmanuel alisema kuwa kutokana na janga hilo wanaendelea kuogopa hata kwenda kutafuta vyumba vya kuishi katika nyumba nyingine maana nyumba nyingi zina nyufa na kutokana na tetemeko kupita kwa mara nyingine, wanahofia hata nyumba hizo zinaweza kuanguka.
Alisema hata kwa wale ambao nyumba zao bado zimesisimama hawawezi kwenda kuomba hifadhi humo maana nyingi zina nyufa, tetemeko limepita tena mara mbili baada ya lile la Jumamosi ingawa ni kwa kiwango kidogo si kubwa kama la kwanza, kwa hiyo wanahofia na nyumba zenye nyufa zinaweza kuangua. Alimwomba Rais John Magufuli kuwasaidia kupata msaada wa haraka angalau kuwapatia mahema ya kuishi maana sasa wanalala nje.
Wakati wananchi hao wakitoa malalamiko hayo ya kutopata msaada wowote, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro aliwataka wananchi hao kuwa na subira kidogo maana serikali inaendelea kufanya kila jitihada ili kuhakikisha wanapata msaada wa haraka.
"Sasa imeundwa kamati ya kufuatilia wananchi waliopatwa na janga hilo, ili kujua hasara iliyotokana na tetemeko hilo lakini pia kubaini misaada ya haraka inayohitajika kwa kila mmoja, tunaendelea na vikao lakini katika wilaya yangu tunakadiria watu zaidi ya 3,000 ndiyo hawana makazi," alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu alisema kuwa hakuna vifo vilivyoongezeka, na kwamba majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wamepungua kutoka 253 hadi 61. Kuhusu dawa na vifaa tiba vingine vinavyohitajika alisema hakuna upungufu na kuwa huduma zinaendelea kutolewa kwa majeruhi wote.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye alisema kuwa watu hao wanahangaika sana kwani wanalala nje kwahiyo ni vizuru serikali kwa kushirikana na wadau mbalimbali na taasisi wakatoa msaada huo wa halaka ili kuondoa adha hiyo.
Pia aliwashauri wananchi na wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia damu katika hospitali ya rufaa ili kuifanya benki ya damu kuwa na damu ya kutosha kwani majeruhi wanahitaji damu na kwamba viongozi wa chama hicho wamejitoa kwa ajili ya kuchangia damu katika Hospitali ya Mkoa huo pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Omumwani ambayo inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM.

Kampuni 35,000 hatarini kufutwa


ZAIDI ya kampuni 35,000 ziko hatarini kufutiwa leseni na wahusika kufikishwa mahakamani kwa kutofuata sheria za uendeshaji biashara nchini.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA), Frank Kanyusi, amesema jana mjini Mwanza baada ya miezi mitatu kuanzia sasa kampuni hizo zitaanza kufutwa.
"Tunatoa miezi mitatu kuanzia sasa kwa wamiliki wa kampuni kuhakikisha wanakamilisha taratibu za uendeshaji wa kampuni zao," amesema.
Ametoa mwito kwa wanaoziendesha kuwasilisha taarifa za kampuni zao kila mwaka pamoja na nakala ya mkaguzi wa fedha, na kwamba kutofanya hivyo kusababisha kufungwa kwa kampuni na kufikishwa mahakamani kwa kukiuka sheria.
"Zaidi ya kampuni 35, 000 zitafutwa na kufunguliwa kesi kwa kutotii sheria na kanuni za uwasilishaji wa taarifa za kampuni kila mwaka," Kanyusi aliwaeleza waandishi wa habari wakati wa usajili wa majina ya biashara na kampuni mkoani hapa.
Amewataka wafanyabiashara na wajasiriamali nchini kutumia fursa ya uwepo wake kurasimisha biashara zao ili serikali iwatambue na kutoa ushirikiano katika kufanya biashara.
Kwa mujibu wake, mwitikio wa watu katika zoezi hilo ni mkubwa kwani wameweza kusajili majina ya biashara 150 na kampuni 100 kwa siku sita kutokana na semina elekezi iliyotolewa kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara.
Alisema wakala unatambua changamoto iliyopo ya upatikanaji wa elimu ya huduma wanazotoa na ndio sababu wameanza ziara ya kutembea mikoa kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi juu ya huduma za Brela na umuhimu wa kurasimisha biashara.
Alifafanua kwa sasa vyombo vya fedha vinaweza kupata taarifa za uhalali wa biashara ya mteja anayetaka kufungua akaunti kupitia mtandao wa Brela.
"Hii itasaidia kuboresha mazingira ya biashara nchini kwani itampa nafuu mteja muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo," alisema Kanyusi.
Alisisitiza kuwa Brela itazindua mfumo wa usajili wa kampuni Machi mwakani ambao utahusisha taasisi nyingine za serikali kama Mamlaka ya Mapato (TRA) ili kurahisisha urasimishaji wa kampuni, ikiwa ni jitihada za kuweka mazingira bora ya biashara nchini.
Alifafanua kuwa mteja atakapowasilisha maombi ya kufungua kampuni, mfumo utamuunganisha na TRA kupata namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) kwa muda mfupi na mteja atakuwa amekamilisha taratibu na kuendelea na biashara.
Mmoja wa wajasiriamali aliyejitokeza, Gerald Malamba aliwataka wajasiriamali wenzake kurasimisha biashara zao ili kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara na pia serikali kuweza kutambua walipa kodi wake.
Mjasiriamali, Anitha Samson alisema ni faraja kwake kwa Brela kufika Mwanza kwani wamepata elimu juu ya umuhimu wa kurasimisha biashara na kutoa mwito kwa wakala kufungua ofisi za kanda ili kutoa huduma kwa ufanishi zaidi.

Kama Movie Vile: Majambazi walivouliwa Vikindu

Dar es Salaam. Siku kadhaa baada ya ofisa wa juu kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, Jeshi la Polisi limetoa taarifa ya kuthibitisha tukio hilo, huku likibainisha kuwa limekamata idadi kubwa ya bunduki, risasi, pingu na vifaa vingine katika msako wa wahusika wa mauaji hayo.
Jeshi hilo pia limesema watu watatu wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi waliuawa wakati wa msako huo uliofanyika baada ya askari wanne kuuawa wakati wakibadilishana lindo la tawi la benki ya CRDB lililoko Mbande Agosti 23, na siku nne baadaye ofisa huyo wa cheo cha kamishna msaidizi wa polisi, Thomas Njuki, kuuawa katika mapambano yaliyotokea Mtaa wa Vikindu Mashariki mkoani Pwani.
Baada ya mauaji hayo ya ofisa huyo, Jeshi la Polisi liliahidi kuwa lingetoa taarifa kamili ya tukio hilo siku iliyofuata lakini halikufanya hivyo hadi jana.
Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa jeshi lake limekamata bunduki 23, risasi 835, fulana maalumu za kuzuia risasi (bullet proof) tatu, sare moja ya polisi, pingu 48 na redio 12 za mawasiliano ambazo alisema zilikuwa zikitumiwa na majambazi katika kufanya uhalifu.
Alisema zaidi ya watuhumiwa saba wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya askari polisi hao watano.
Kamanda Sirro alisema Septemba 3, majira ya saa 8:00 mchana askari wake waliweka mtego na kufanikiwa kukamata majambazi watatu ambao wanaishi maeneo ya Mbagala, Keko na Kawe.
Alisema waliweka mtego huo wakati wakifuatilia tukio la ujambazi lililotokea Agosti 29 kwenye jengo la Sophia House lililoko Barabara ya Chang’ombe karibu na Veta ambako majambazi kumi walivamia ofisi za kampuni ya Matrix International na kupora Sh35 milioni.
Amesema walipowahoji, watu hao watatu walikiri kuhusika katika matukio tofauti ya ujambazi wa kutumia silaha na kueleza kuhusu silaha walizo nazo na nyingine zilizofichwa msitu wa Vikindu.
“Majambazi hawa walikiri kuwa na silaha kwenye nyumba waliyokodi eneo la Mbezi Beach, ndipo askari walienda kufanya upekuzi na kupata silaha mbalimbali,” alisema Kamanda Sirro.
Amesema katika nyumba hiyo wamekuta silaha 23 kati ya hizo, tatu ni za kivita na 16 ni bastola. Pia alisema walikuta risasi 835, fulana tatu za kuzuia risasi (bullet proof) tatu, sare ya polisi, pingu 48, redio 12 za mawasiliano na magazini tisa. Vitu vingine vilivyokutwa ni panga, nyundo kubwa, mtambo wa kuchukulia matukio (CCTV), mtarimbo mmoja ambao Sirro alisema hutumika kuvunjia milango, gari aina ya Toyota Noah na jingine aina ya Toyota Alphard.
Sirro pia amesema katika mahojiano nao, majambazi hao walisema silaha nyingine walificha Msitu wa Vikindu wilayani Mkuranga, ndipo askari hao walipoambatana na watuhumiwa hao kwenda eneo hilo.

Mjane auawa, anyofolewa viungo


MJANE mwenye umri wa miaka 46, Veronica Dala ameuawa na watu wasiofahamika kwa kukatwa na mapanga mwilini. Aidha mjane huyo amenyofolewa baadhi ya viungo vya mwili wake.
Tukio hilo limetokea alfajiri ya Septemba Mosi mwaka huu katika kijiji cha Ilagaja, kata ya Mwangoye wilayani Nzega mkoani Tabora baada ya wahalifu hao kuvamia nyumba ya mjane huyo kisha kuanza kumshambulia kwa mapanga.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya majirani na ndugu wa mjane huyo walisema walipata taarifa ya kuwa ameuawa na watu wasiofahamika asubuhi ya tukio hilo.
Luhaga Jilala ambaye ni ndugu wa mjane huyo, alisema taarifa hizo alizipata asubuhi kuwa ndugu yake ameuawa. Hata hivyo, chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Juma Seleli alisema tukio hilo ni la pili kutokea miaka kadhaa iliyopita alivamiwa na wahalifu na kumjeruhi vibaya.
Alisema kijiji hicho kimejipanga kuhakikisha wanafanya doria za mara kwa mara ili kuimarisha ulinzi wa kijiji na wananchi wake.
Diwani wa kata hiyo, Henerico Kanoga alisema atahakikisha wananchi wanafanya uchunguzi kwa kupiga kura za maoni ili kuwapata watu wanaoshiriki kufanya uhalifu huo wa kikatili.
Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla alisema Serikali ya Wilaya imeandaa mpango mkakati wa kuhakikisha wananchi wanatoa ushirikiano wa kutosha ili kukomesha mauaji.
Alisema wilaya ina mpango wa kuanza kupiga kura za maoni kwa wananchi ili kuwabaini wote wanaoshirikiana na wahalifu hao na kuongeza kuwa mwananchi atakayetoa taarifa dhidi ya wahalifu hao, siri zote zitatunzwa ili kulinda usalama wake.
Polisi mkoani Tabora imekiri mauaji hayo na kuahidi kufanya msako mkali kwa ajili ya kuwakamata na inawashikilia watu wawili kwa ajili mahojiano

Mkulima (54) adaiwa kunajisi mtoto (6)


MKAZI wa wilayani Igunga mkoani Tabora ,Shimba Kanyala (54) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya hiyo akidaiwa kunajisi.
Mwananchi huyo anakabiliwa na mashitaka ya kumnajisi mtoto mwenye umri wa miaka sita. Kanyala (54) ni mkulima wa kijiji cha Nkinga, tarafa ya Simbo.
Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi, Wilaya ya Igunga, Frank Matiku ameieleza mahakama kuwa, Agosti 23, mwaka huu saa 10 jioni katika kijiji cha Nkinga, mshitakiwa alimnajisi mtoto na kumsababishia maumivu sehemu zake za siri.

Chadema wadaiwa kuhonga vijana Sh 40,000


POLISI Kanda ya Dar es Salaam imekituhumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwalipa fedha kiasi cha Sh 40,000 baadhi ya vijana ili washiriki katika maandamano ya Ukuta ya Septemba Mosi yaliyopigwa marufuku.
Aidha, imesisitiza imejipanga kikamilifu kukabiliana na watu watakaovunja sheria kwa kufanya maandamano hayo ambayo yamepigwa marufuku kwa lengo la kutaka kuvuruga amani ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro wakati akizungumza jijini Dar es Salaam ambapo alisema, kwa sasa jiji hilo liko shwari na hata baada ya Septemba Mosi, litaendelea kuwa shwari.
“Naomba niwasihi Wana Dar es Salaam hasa vijana wasiingie barabarani hiyo tarehe moja, tuwaachie wachache ambao nia yao ni kuleta fujo, wote tunajua madhara ya fujo, wote tunajua hasara ya fujo, siku hiyo imetolewa katazo hakuna maandamano,” alisema Sirro.
Alisema kwa taarifa za intelijensia walizonazo zinaonesha kuna watu wanapewa fedha kwa ajili ya kuandamana na kufanya fujo, ambapo alitoa rai kwa wazalendo wa nchi wasiopenda kupambana na Jeshi la Polisi ambalo linawalinda wao na mali zao wasithubutu kuingia barabarani.
Akizungumzia tuhuma hizo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema, chama hicho hakina fedha za kuwalipa vijana ili kufanya maandamano na kusisitiza; “Tukutane tarehe moja Septemba.”
Julai 27, mwaka huu Chadema ilizindua operesheni iliyopewa jina la Ukuta ikiwa na lengo la kupambana na kile ilichokiita udikteta nchini, huku ikitangaza kushirikiana na wale watakaoona umuhimu wa kuwepo kwa haki na demokrasia nchini.

Hawa Ndo Vigogo wanne waliosimamishwa TPDC


BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imethibitisha kumsimamisha Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Dk James Mataragio na kuongeza kuwa pia imewasimamisha wakurugenzi wanne kutokana na tuhuma za ukiukwaji wa taratibu za utendaji kazi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo, Profesa Sufian Bukurura, kusimamishwa kazi kwa watendaji hao kunatokana na tuhuma za awali zikiwemo za ukiukwaji wa sheria na kanuni za manunuzi ya umma.
Aliwataja wengine wanne waliosimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili ni Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu, Kelvin Komba, Mkurugenzi wa Fedha, George Seni, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani, Gabriel Mwero na Mkurugenzi aliyekuwa anasimamia ugavi na manunuzi, Edwin Riwa.
Akizungumzia tuhuma za awali zinazowakabili watendaji hao, Profesa Bukurura alisema ni pamoja na ukiukwaji wa sheria na Kanuni za Utumishi hususan mgongano wa kimaslahi, kubadili matumizi ya fedha za bajeti bila idhini ya mamlaka ya juu na kutokutoa taarifa muhimu na nyeti hususan za shughuli za shirika hilo.
Alisema hatua hiyo ya kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi imekuja baada ya bodi hiyo kukutana kwenye kikao cha dharura kilichofanyika Agosti 24, mwaka huu.
Aidha, alisisitiza kusimamishwa kazi kwa watajwa hao hakuna maana kuwa wamepatikana na hatia kwa sasa, bali ni hatua ya awali ya kuwezesha uchunguzi kufanywa katika mazingira rafiki ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo kama zina uzito kisheria au la. Alisisitiza watapewa nafasi ya kujieleza na kujitetea kulingana na kanuni za utumishi wa uma

Maneno Ya Mtandaoni Juu Ya Jengo Jipya la Bakwata hayatutishi - Mufti

MUFTI wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar Zubery (pichani), amesema Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) halitishwi na maneno yanayoendelea mitandaoni kuhusu kujengewa jengo katika Makao Makuu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye ni Mkristo.
Mufti alisema kumekuwa na maneno mengi, yanayozungumzwa katika mitandao ya kijamii baada ya Makonda kusema atajenga jengo hilo katika makao makuu ya Bakwata, Kinondoni jijini humo, huko wengi wakisema kwa nini baraza hilo limekubali kujengewa na mtu ambaye sio Muislamu.
Alitoa kauli hiyo jana wakati Mkuu wa Mkoa huyo, akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo hilo ambalo litatumia Sh bilioni tano hadi kukamilika kwake.
Mufti Zubery alisema maneno hayo, hayawasumbui na wapo Wakristo wengi waliowahi kuchangia maendeleo kwa Waislamu, lakini hayakutokea maneno kama yanayotokea sasa.

“Kwa nini Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa alipotupa Chuo Kikuu hamkusema? Wapo wadau wengi tu Wakristo walitoa… leo Makonda katoa maneno yamekuwa mengi.
Acheni jamani, mbona hayo ni maneno ya husda na choyo, Waislamu wametoa na sasa Wakristo. Hata Mtume amewahi kupokea misaada kama hiyo,” alisema Mufti.
Kwa upande wake, Makonda alisema hashangazwi na maneno yanayoendelea, kwani Watanzania wamekuwa wakibeza kila jambo zuri linalofanywa na viongozi. Alisema jengo hilo linatarajiwa kujengwa kwa udhamini wa Kampuni ya GSM Foundation, ambao walikubali kujenga kwa gharama zao mpaka kukamilika.
“Wengi waliuliza fedha nitatoa wapi, lakini wanasahau mimi ni mtu wa watu, nimezungumza na wadau wangu, wamekubali kujenga jengo hilo ambalo nimewataka wajenge kwa muda wa miezi kumi na nne,” alifafanua Makonda na kuwataka viongozi wa serikali kutoa kipaumbele kwa viongozi wa dini wanaotaka kupata huduma katika ofisi zao kwani ni watu muhimu na wanapaswa kuwa mbele wanapohitaji huduma.

HII NDO STORI KUHUSU WALIOKAMATWA NA MADAWA YA KULEVYA KWENYE MELI ILIYO NA USAJILI WA TAZANIA


Meli iliyomatwa huko Glosgow
Watu wawili raia wa Uturuki walionaswa mwaka jana kwenye ufukwe wa Aberdeen, Scotland na meli iliyokuwa imebeba tani tatu za dawa za kulevya aina ya cocaine huku ikiwa na usajili wa nchini Tanzania, wamekutwa na hatia mahakamani nchini Scotland.
Mahakama Kuu ya Glasgow, mji mkuu wa Scotland imewakuta na hatia watu hao ambao ni Mumin Sahin na Emin Ozmen kwa kukutwa na dawa hizo za kulevya daraja A zenye thamani ya Paundi milioni 500 za Uingereza ambazo ni sawa na Shilingi trilioni 1.49 za Tanzania. Aidha mahakama hiyo haikuwakuta na hatia washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ambao ni, Kayacan Dalgakiran, Mustafa Guven, Umit Colakel na Ibrahim Dag. Kwa mujibu wa habari hiyo, dawa hizo za kulevya tani 3.2 aina ya cocaine na zilifichwa ndani ya meli ya MV Hamal iliyokuwa inapeperusha bendera ya Tanzania. Inaarifiwa kuwa, kabla ya hapo meli hiyo, inayomilikiwa na kampuni ya Kiev Shipping and Trading Corporation, ilitia nanga kwa muda nchini Guyana, Amerika ya Kusini ambayo hutumiwa kupakia cocaine kuelekea Amerika Kaskazini na Ulaya. Taarifa zaidi zinasema kuwa meli hiyo iliyokamatwa Aprili 23, mwaka jana, ilikuwa imetia nanga maili 100 kutoka ufukwe wa Aberdeen, Uingereza baada ya kuzuiwa kuingia nchini humo. Hiyo ni meli ya tatu kukakamatwa ikiwa imebeba mzigo mkubwa wa dawa za kulevya baada ya ile iliyokamatwa nchini Italia ikiwa na usajili wa Tanzania ikiwa na tani 30 za cocaine na nyingine ya Canada iliyokamatwa katika Bahari ya Hindi nchini Tanzania ikiwa na kilo 283 za cocaine.