Dar es Salaam. Watoto pacha,
Elikana na Eliud waliokuwa wameungana wamerejea nchini jana wakitokea
India walipokuwa kwa ajili ya kutenganishwa, tayari kwa kusherehekea
kumbukumbu yao ya kutimiza mwaka mmoja leo.
Waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Julius
Nyerere saa 10:30 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Oman, wakiwa na mama
yao, Grace Joel (20) ambaye muda wote alionekana mwenye furaha.
Elikana na Eliud walizaliwa Februari 20, mwaka
jana wilayani Kyela, Mbeya wakiwa wameungana na baadaye kuhamishiwa
katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya ambako walipata rufaa ya kwenda
Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Juni mwaka jana, Serikali iliwapeleka Hospitali ya
Chennai, India ambako Desemba 16, mwaka jana walifanyiwa upasuaji
mkubwa wa kuwatenganisha.
Akizungumza baada ya kutua jana, Grace alisema:
“Nina furaha ya ajabu, sijui nimshukuru vipi huyu Mungu wangu, ni mkuu
mno. Ninawashukuru sana madaktari wa India, ninawashukuru madaktari wa
Muhimbili na sana naishukuru Serikali yangu kwa kunipa msaada huu
mkubwa. Siamini kama leo ningekuwa narudi salama na watoto wangu kila
mmoja akijitegemea,” alisema Grace.
“Kesho (leo) ni birthday yao, wanatimiza mwaka
mmoja, ni furaha ya ajabu niliyo nayo, siwezi kuelezea. Siku
nilipoambiwa watoto wangu watafanyiwa upasuaji mkubwa na watapumulia
mashine kwa wiki moja, nilichanganyikiwa kwa kweli, sikutamani tena hata
hiyo operesheni ifanyike ila sikuwa na jinsi zaidi ya kumwomba Mungu.”
Akizungumza uwanjani hapo, Dk Glory Joseph kutoka
Hospitali ya Rufaa Bugando ambaye aliongozana na watoto hao kurudi
nchini alisema: “Watoto wamerejea salama na wanaendelea vizuri ila
watakuwa Moi (Hospitali ya Mifupa Muhimbili), kwa uangalizi maalumu
mpaka hapo madaktari watakapoona inafaa ndipo watapewa ruhusu ya kurudi
nyumbani kwao Mbeya.
“Agosti watarudishwa tena India kwa ajili ya
upasuaji katika njia ya mkojo na kufunga sehemu ya utumbo,” alisema.
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Nsachris Mwamwaja alisema upasuaji wa watoto hao ulichukua saa 18.
Katika muda huo, saa 13 zilitumika kutenganisha viungo vilivyoungana
sehemu ya chini ya uti wa mgongo, sehemu ya utumbo mpana, njia ya mkojo,
kibofu na sehemu ya uume, wakati saa tano zilitumika kuunganisha sehemu
zilizotenganishwa.
Pacha hao walifanyiwa upasuaji na madaktari 20 na
wataalamu wengine wa afya ambao walitumia saa 18 kuwatenganisha. Kiasi
cha Sh100 milioni kilitumika.
Meneja wa Huduma za Wagonjwa wa Kimataifa wa
hospitali hiyo, Senu Sam alizungumza na gazeti dada la Mwananchi, The
Citizen juzi na kusema wamefanya sherehe kwa ajili ya mafanikio ya
upasuaji huo.
Sam alisema pacha hao wameonana ana kwa ana kwa
mara ya kwanza, wiki tatu baada ya upasuaji... “Imekuwa faraja kuwaona
wakitazamana. Eliudi alivishika vidole vya mkono wa Elikana na
kuvichezea. Wanaonekana kufurahia mazingira mapya,” alisema Sam.
Mwanachi
0 comments:
Post a Comment