pagead2.googlesyndication.com pagead2.googlesyndication.com

TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU BARAZA LA MAASKOFU WA KIPENTEKOSTE TANZANIA (PENTECOSTAL COUNCIL OF TANZANIA) KUTOKUWA NA UWALIKILISHI KATIKA BUNGE MAALUM LA KATIBA

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898                              PRESIDENT 'S OFFICE.
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com                                  THE STATE HOUSE,
press@ikulu.go.tz                                                                  P.O.BOX 9120,
Fax: 255-22-2113425                                                           DAR-ES-SAALAM
                                                                                              Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU BARAZA LA MAASKOFU WA
KIPENTEKOSTE TANZANIA (PENTECOSTAL COUNCIL OF
TANZANIA) KUTOKUWA NA UWALIKILISHI KATIKA BUNGE
MAALUM LA KATIBA

1. Uteuzi wa Wajumbe wa Bunge la Katiba unafanywa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura, 83 (The Constitutional Review Act, Cap 83). Sheria hii inaweka mamlaka ya uteuzi, masharti, taratibu, vigezo na mambo mengine yote yanayopaswa kuzingatiwa katika uteuzi wa Wajumbe wa Bunge la Katiba. Kwa mujibu wa Kifungu cha 22 (2A) na (2B) vigezo hivi vinajumuisha umri, jinsia, uzoefu, sifa na mahali anapotoka mjumbe husika.
2. Sheria hii imeainisha aina tatu za Wajumbe wa Bunge la Katiba kama ifuatavyo:
(i) Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
(ii) Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar; na
(iii) Wajumbe 201 kwa mujibu wa Kifungu Na. 22(1c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inaonyesha makundi mbalimbali 10 yanayohusika.
3. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, wajumbe 201 wanatakiwa kuteuliwa kutoka katika       makundi yafuatayo:
(i) Taasisi zisizokuwa za Kiserikali (20)
(ii) Taasisi za Kidini (20)
(iii) Vyama vyote vya Siasa vyenye Usajili wa Kudumu (42);
(iv) Taasisi za Elimu (20);
(v) Watu wenye Ulemavu (20);
(vi) Vyama vya Wafanyakazi (19);
(vii) Vyama vinavyowakilisha Wafugaji (10);
(viii) Vyama vinavyowakilisha wavuvi (10);
(ix) Vyama vya Wakulima (20); na
(x) Vikundi vya Watu wenye Malengo yanayofanana (20).
4. Mchakato wa uteuzi ulianza kwa kutoa Tangazo la Mwaliko katika Gazeti la Serikali, Tangazo la Serikali Na. 443 la tarehe 13 Desemba, 2013. Tangazo hilo lilitolewa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza ili kuyaalika makundi yaliyotajwa kisheria kuwasilisha mapendekezo ya majina kwa ajili ya uteuzi katika Bunge Maalum la Katiba. Aidha, Tangazo hilo lilitangazwa pia katika magazeti mbalimbali yanayosomwa hapa nchini. Pamoja na mambo mengine, Tangazo hilo lilitamka ukomo wa muda wa taasisi na makundi kuwasilisha mapendekezo ya majina ya wajumbe kuwa ni tarehe 02 Januari 2014.
5. Mapendekezo hayo yalitakiwa kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au kwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Mapendekezo hayo yalitakiwa kuwasilishwa kwa njia ya barua ya posta au barua inayoletwa kwa mkono. Sheria haikutoa njia nyingine ya kuwasilisha mapendekezo. Ninafahamu, wengine wangeweza kutumia barua pepe au hata ujumbe mfupi wa maneno. Sheria haisemi hivyo!
6. Kufuatia mwaliko huo, taasisi 554 kutoka Tanzania Bara na 178 kutoka Zanzibar ziliwasilisha   mapendekezo yao. Mapendekezo hayo yalijumuisha majina 2,762 kwa upande wa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar mapendekezo hayo yalihusisha watu 874. Hivyo basi, taasisi na makundi mbalimbali yalipendekeza jumla ya majina 3,636. Aidha, watu 118 walijipendekeza wenyewe kinyume na matakwa ya kisheria na kufanya idadi ya majina yaliyopendekezwa kuwa 3,754.
7. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imeweka masharti katika uteuzi wa wajumbe 201 wa Bunge Maalum la Katiba. Masharti hayo, ni pamoja na wajumbe wasiopungua theluthi moja wanatakiwa kutoka Zanzibar na
theluthi mbili kutoka Tanzania Bara. Kwa sababu hiyo, katika wajumbe 201, wajumbe 67 wanatakiwa kutoka Zanzibar na wajumbe 134 wanatakiwa kutoka Tanzania Bara. Aidha, uteuzi huo unatakiwa kuzingatia idadi ya wajumbe kutoka katika kila kundi kama ilivyoainishwa kisheria. Vilevile, mgawanyo wa wajumbe wanawake na wanaume unatakiwa uwe nusu kwa nusu. Pamoja na hayo, wajumbe hao wawakilishe sura ya wananchi wa Tanzania kwa ufuasi wa vyama vya siasa, dini, umri, na maeneo anayotoka.
8. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishirikiana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar walikamilisha uteuzi wa wajumbe 201 na majina ya walioteuliwa yalitangazwa tarehe 7
Februari 2014. Majina hayo yalitangazwa kupitia taarifa kwa vyombo vya habari na pia Gazeti la Serikali kwa Tangazo la Serikali Na. 29 la tarehe 7 Februari 2014.
BARAZA LA MAASKOFU WA KIPENTEKOSTE TANZANIA
9. Tarehe 11 Februari 2014, Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu uteuzi wa Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba. Baraza liliomba vyombo vya habari lifikishe masikitiko ya Baraza kwa viongozi na waamini wa Kipentekoste wote na jamii ya wapenda haki hapa nchini, kutokana na kitendo cha Serikali wanayoiheshimu, wanayoipenda na kuiombea, kwa kulibagua na kulitenga
Baraza lisihusike na Bunge Maalum la Katiba. 
10. Katika Taarifa yake kwa vyombo vya habari, Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania limeeleza kuwa kwa …”utaratibu tuliojiwekea katika utawala wa Baraza letu, hakuna Kanisa moja, mchungaji binafsi,
mwamini, anaweza kujitwalia heshima, kuchukuliwa au kupewa haki na chombo chochote cha Serikali katika nchi yetu kwa nia ya kuwakilisha wapentekoste, bila kupata idhini toka kikao halali cha Kamati Kuu ya
Utendaji ya PCT-Taifa”.
11. Kwa kuzingatia utaratibu huu “Kamati Kuu ya Utendaji ya PCT-Taifa katika kikao chake cha tarehe 5/12/2013 ilipendekeza kwa Mheshimiwa Rais majina ya wajumbe wake iliowaona kuwa wanafaa kuchaguliwa katika Bunge Maalum la Katiba, lakini cha kusikitisha kati ya hao hakuna jina la mjumbe hata mmoja ambaye alichaguliwa na Mheshimiwa Rais katika Bunge Maalum la Katiba”.
12. Taarifa hiyo imeeleza pia, “… Serikali imeona hatufai na hatuna sifa za kuweza kuchaguliwa katika Bunge Maalum la Katiba, na badala yake ikaamua kuteua majina ya wajumbe toka katika taasisi nyingine za kidini zenye hadhi kama yetu za Waislamu, Wakatoliki, Waprotestanti na Wajumbe wengine binafsi kwa Tanzania Bara na Visiwani na kuwaacha Wapentekoste…”


UFAFANUZI WA SERIKALI
13. Kwanza kabisa, napenda kuwahakikishia watanzania na hasa wale waliolengwa na taarifa ya Baraza, kwamba Serikali haikuupuzia kundi lolote lililoanishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuwasilisha mapendekezo ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Serikali inaliheshimu Baraza na tunalishukuru sana katika juhudi inazozifanya kwa pamoja na Serikali katika kuwaendeleza wananchi wa Tanzania.
14. Kutokana na umuhimu wa makundi mbalimbali, jumla ya makundi 850 yaliwasilisha mapendekezo ya majina 3,636. Katika makundi haya 850, kulikuwa na mapendekezo kutoka taasisi au makundi ya kidini 72 ambayo yalipendekeza jumla ya majina 429. Kwa upande wa Tanzania Bara, taasisi za kidini 55 ziliwasilisha mapendekezo yenye jumla ya majina 344. Aidha Serikali ilipokea mapendekezo 118 kutoka kwa waliojipendekeza wenyewe! Hivyo, siyo kweli kuwa Serikali ilipuuza mapendekezo kutoka kundi fulani ikiwa ni pamoja na Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania. Serikali hii ni kwa ajili ya watu na makundi yote. Aidha, Katiba yetu haibagui watu au makundi ya watu kwa lengo la kuwanyima au kuwakosesha haki.
15. Kufuatia taarifa ya Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania kwa vyombo vya habari kuwa mapendekezo yao yamepuuzwa, kwa kuanzia Serikali imefuatilia kama kweli Baraza hilo liliwasilisha mapendekezo. Kwa kuwa mapendekezo yote yaliyowasilishwa yaliwekwa katika kanzi data ya msingi (primary data base) kwa ajili ya uchambuzi, utafutaji kwa kutumia kompyuta (computer search or find) ulifanywa ili kubaini kama kulikuwa na mapendekezo kutoka Baraza kati ya mapendekezo 850 yaliyowasilishwa.
16. Kwa kuwa hakukuwa na taarifa za majina ya waliopendekezwa, jina la taasisi na majina ya maaskofu watano (5) walioshiriki katika utoaji taarifa kwa vyombo vya habari yalitumika katika kubaini kama wao pia walikuwa miongoni mwa waliopendekezwa. Utafutaji wa huu haukubaini kuwa Baraza ilikuwa moja ya taasisi zilizowasilisha maombi. Aidha, hapakuwa na jina hata moja la viongozi wa Baraza walioitisha vyombo vya habari kutoa taarifa.
17. Pamoja na kwamba haikutarajiwa kuwa viongozi wa taasisi hii kujipendekeza wenyewe, na hivyo kuwa miongoni mwa watu 118 waliojipendekeza wenyewe, juhudi za Serikali zilijielekeza kutafuta endapo kulikuwa na mapendekezo kundi hili. Hata hivyo, utafutaji haukubaini majina ya viongozi hawa kuwepo katika orodha hiyo.
18. Kulikuwa na uwezekano pia, Baraza liliwasilisha mapendekezo ambayo yalifika kwa Katibu Mkuu Kiongozi nje ya muda uliopangwa kisheria wa tarehe 2 Januari 2014. Uchambuzi wa mapendekezo 52 ambayo yaliwasilishwa nje ya muda haukubaini kuwepo kwa mapendekezo kutoka Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania.
19. Hivyo, juhudi za Serikali katika kufuatilia uwepo wa mapendekezo kutoka Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania hazikuweza kuthibitisha kuwa Baraza lilituma mapendekezo yake kama ilivyokuwa imeagizwa na Sheria ya mabadiliko ya Katiba!
UWAKILISHI WA MADHEHEBU YANAYOUNDA BARAZA LA
MAASKOFU WA KIPENTEKOSTE TANZANIA
20. Kwa kufahamu umuhimu wa makundi mbalimbali ya kidini ikiwa ni pamoja na Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania unaoundwa na Maaskofu Wakuu wa madhehebu ya kipentekoste yapatayo 75, uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ulihakikisha kuwa makundi ya kidini yanawakilishwa ipasavyo.
21. Mgawanyo wa idadi ya wajumbe 20 kutokana na makundi ya kidini baina ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuzingatia uwiano wa moja ya tatu ya wajumbe kutoka Zanzibar ulimaanisha kuwa katika kundi hili, wajumbe 7 wangekuwa wanatoka Zanzibar na wajumbe 13 wangekuwa wanatoka Tanzania Bara. Uteuzi wa wajumbe katika kundi hili umezingatia kigezo hiki.
22. Kufuatia uteuzi uliofanywa tarehe 7 Februari 2014, uchambuzi wa majina ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba umebaini kuwa kati ya wajumbe 13 kutoka taasisi za kidini wa Tanzania Bara walioteuliwa, mjumbe mmoja (1) aitwaye Bibi Respa Miguma Adam ameteuliwa kutoka Evangelistic
Assemblies of God Tanzania (EAGT), Patmos Vision, Kigamboni Church. Evangelistic Assemblies of God Tanzania ni moja ya madhehebu ambayo maaskofu wake wakuu wanaunda Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania.
23. Hivyo, tamko la Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste kuwa wanabaguliwa halina ukweli kwa kuwa uchunguzi tulioufanya haujathibitisha kuwa Baraza lilileta mapendekezo. Ni vyema Baraza likafanyia kazi kwa nini kama kulikuwa na mapendekezo, hayakufikishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi
(Dar es Salaam) au Katibu Mkuu Kiongozi (Zanzibar). Ninaamini kabisa kama mapendekezo hayo yangekuwa yamewasilishwa, Mhe. Rais angechagua mwakilishi kutokana na mapendekezo hayo.
HITIMISHO
24.Uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba uliofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar tarehe 7 Februari 2014, kwa namna yoyote ile haukuwa na nia ya kulibagua Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania.
25. Kuna kila sababu ya kuamini kuwa mapendekezo ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania hayakuwasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi kama sheria ilivyohitaji.
26. Pamoja na kuwa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania hawakuweza kuwasilisha mapendekezo yao kama ilivyotakiwa, tunaamini kuwa Baraza, kama ilivyo kwa wananchi wote, litawakilishwa vyema na wajumbe walioteuliwa ambao wanajumuisha mjumbe aliyeteuliwa kutoka
moja ya madhehebu yanayounda Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Februari 2014

0 comments:

Post a Comment